Prime
Oluoch: Visasi, uchu wa madaraka vinaitesa CWT
Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch amesema chama hicho kwa sasa kiko mahututi au imekufa kabisa kwa kushindwa kuwatetea walimu.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Oluoch alisema viongozi wa CWT wameondoka kwenye mstari kwa wameacha kutumia Katiba na wanaendeshwa na wanasiasa na sio kama taasisi ya wafanyakazi.
“Kazi kubwa ya vyama vyama vya wafanyakazi ni mbili, kwanza ni kuwatetea wanachama ili wapate masilahi na ndio maana wanatoa michango yao. Pili ni kuwatetea wanapopata changamoto kazini, kama ameshitakiwa kosa la jinai.
“CWT ya wakati wetu, viongozi wetu hatukuwa tukilipiza visasi, na hatukuwa tiukipigania madaraka yasiyo kuwa yako. Kwa mfano, mimi nilikuwa Naibu Katibu Mkuu, sikuwa na ndoto ya kuwa Katibu Mkuu,” alisema.
Aliendelea kusema kuwa wakati wao, viongozi walikuwa na ushawishi kwa walimu kwa kuwatembelea na kusikiliza shida zao.
“Lakini uongozi sasa kwa sababu nadhani hawana nia ya kuwapigania walimu, hawafanyi, wamebakia kugombania madaraka.
“Kwa mujibu wa katiba, Chama cha Walimu kinapaswa kuwa huru, kisiwe chini ya mwajiri wala Serikali. Sisi tulikuwa huru, hatukuruhusu Serikali kutuingilia,” alisema.
Hata hivyo, Rais wa CWT, Leah Ulaya alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema: “Kila zama na kitabu chake, kwa hiyo mtu asichukulie enzi za kule anazileta leo anafikiri sisi hatufanyi kazi. Tuko ‘serious’ (makini) na kazi.
“Yeye ni kiongozi wa wakati ule na sisi ni viongozi wa wakati huu, yale tunayofanya wakati huu shukrani yake ni kwa walimu wahusika, wala si yeye ambaye kwa sasa ni mwalimu hawezi kujua,” alisema.
Hoja ya Oluoch
Akijenga hoja yake kuhusu kukengeuka kwa CWT, Oluoch alisema viongozi wa sasa hawafuati katiba ya chama wala sheria za kazi na ndio sababu ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Japhet Maganga ameondolewa kwenye uongozi pasipo kufuatwa kwa utaratibu.
“Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi, alisema kuwa hamtambui Katibu Mkuu aliyechaguliwa na wanachama, halafu kiongozi wa chama anasema kwa sababu msajili amekukataa na sisi tunakuondoa.
“Kisheria msajili haruhusiwi kuingilia masuala ya vyama vya wafanyakazi, kazi yake ni kusajili vyama vya wafanyakazi, katiba na kanuni, ili vyama viendeshwe kwa katiba na kanuni hizo.
“Kazi ya pili, ikiwa chama kimekiuka katiba yake, basi yeye aende mahakamani,” alisema.
Alitaja pia kazi ya tatu ya Msajili huyo ni ukaguzi wa hesabu za vyama.
“Akiona hesabu hazijakaa sawa, anakiandikia chama cha wafanyakazi watoe maelezo. Wasipotoa maelezo, anapeleka mkaguzi kukagua, akishakagua, hapeleki popote, anarudisha kwenye chama,” alisema.
Alisema kuondolewa kwa Maganga madarakani ni dalili ya CWT kuingiliwa.
“Tunao ushahidi wa kuingiliwa, kwa sababu yule katibu ameondolewa kwa barua ya Msajili, jambo linalokiuka ibara ya 1, 2 na 3 ya mikataba namba 87 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo Tanzania imerdhia.
“Hiyo ni sehemu ya kifungu cha 37 cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini inayosema vyama vya wafanyakazi viko huru na kiongozi wa chama cha wafanyakazi, haruhusiwi kufukuzwa kwa sababu ameshiriki kwenye uchaguzi,” alisema.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo, Ulaya alisema, pamoja na Msajili kumwandikia barua Maganga, taratibu nyingine ziko ndani ya chama cha Walimu na wao kama chama wanafuata taratibu zao
“Viinginevyo sisi tunachojua ni kwamba utaratibu unaotumika ni halali.Kama kuna mtu anaona sio sawa, zipo sheria za nchi, zipo sheria za kazi, zipo sheria mbalimbali ambazo mtu anaweza kuzifuata akapata haki haki yake. Kikao ndio kinamwondoa na wala sio mtu,”alisema.
Kupigania masilahi ya walimu
Oluoch aliendelea kuwananga viongozi wa CWT akisema wamekosa ushawishi kwa walimu, na kwamba wameshindwa kutetea masilahi yao zikiwemo nyongeza za mishahara.
“Tangu nimetoka mwaka 2017 sijawahi kuona mikutano ya viongozi ikifanyika ngazi ya mikoa wala wilaya na tangu nimeondoka, chama cha walimu hakijawahi kukaa na kujadiliana juu ya mishahara ya walimu. Mshahara huu wanaoupata ni ule nilioujadili mwaka 2013.
“Kazi ya chama cha wafanyakazi ni kupigania masilahi ya wanachama, sasa kama una miaka 11 hujapigania mishahara ya wafanyajazi, sidhani kama maisha yako yataendelea,” alisema.
Pia Oluoch alisema kutokana na kukosa ushawishi, baadhi ya walimu wameamua kuondoka CWT na kujiunga na vyama vigine vya walimu vilivyoanzishwa.
“Ukiangalia takwimu, unaweza kukuta walimu 600 wamejiunga na chama kingine cha walimu, ukiangalia hata idadi ya wanachama inaanza kupungua.
“Nguvu pekee waliyonayo viongozi ni kwamba ada za wanachama zinakatwa na Serikali kutoka Hazina moja kwa moja, halafu wanapewa. Hiyo ndio jeuri yao, kwa sababu wana fedha. Lakini sio kwamba wamekonga mioyo ya wanachama,” alisema.
Lakini alipoulizwa suala hilo, Ulaya alisema: “Wewe unavyoona CWT imekufa au ipo? Swali la pili, hii nyongeza ya mshahara na mambo yote yanayoendelea sasa yanatokea wapi, Urusi (Russia) au Tanzania? Wewe unajuaje kama walimu hawaongezwi?” alihoji.
Aliendelea: “Wewe unafikiri hayo madaraja mserereko yanatokana na nini? Tumekaa kwenye vikao na kama unataka ushahidi utaona tulivyokaa mfululizo kwa tarehe, kwa muda kwa mwezi na watu gani tuliokaa nao.”
Kuhusu walimu kukatwa michango moja kwa moja na Serikali alisema: “Walimu waliopo hawakatwi tu hivi mishahara yao, wanajaza fomu. Hivyo wanaokatwa fedha zao ni wale waliojaza fomu kuridhia kwamba wao ni wanachama.”
Alijibu pia kuhusu walimu kuikacha CWT, akisema: “Muulize huyo Oluoch wakati alipokuwepo aliacha wanachama wangapi na sasa kuna wanachama wangapi? Wakati wa uongozi wao kulikuwa na chama cha Chakamwata (Chama cha Kutetea Haki na Masilai ya Walimu Tanzania), kina Oluoch walikosea nini?”
Alivyofukuzwa CWT
Oluoch pia amesimulia jinsi alivyofukuzwa CWT mwaka 2017 akidaiwa kuiba Sh15 bilioni.
“Kilichofanya nikafukuzwa ni kwamba, tulikwenda kwenye baraza kuu la walimu, baraza likaamua kwamba, sisi tutoe notisi ya siku 60 ili Serikali ilipe madeni ya walimu, kama sheria inavyotaka.
“Tulipotoka kikaoni Katibu Mkuu akaniambia anakwenda likizo, hivyo nitekeleze maelekezo ya baraza. Kwa hiyo mimi nikasaini ile barua, ikaenda, Rais (hayati) John Magufuli. Aliposoma ile barua akasema najaribu kucheza na Serikali yake,” alisema.
“Kwa hiyo Rais (John Magufuli) akamtuma Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja kukagua hesabu za chama, lakini kwa bahati mbaya yule aliyenituhumu ndiye aliyepatikana na hatia, mimi sikuiba hata senti tano,”alifafanua.
Sera ya Elimu na Mafunzo
Alipoulizwa kuhusu mabadiliko ya Sera ya elimu na Mafunzo na mitalaa nchini, Oluoch alisema suala hilo limecheleweshwa, hivyo linapaswa kuharakishwa.
“Sera ya Elimu na Mafunzo ilipitishwa mwaka 2014 na mwaka huo, iliamuliwa kuwa mtoto akimaliza darasa la sita aingie kidato cha kwanza, mitalaa ikaandaliwa, vitabu vikachapishwa, walimu wakafundishwa.
“Sasa ilipoingia Serikali ya awamu ya tano wakafuta kila kitu, hata vile vitabu vilivyochapishwa. Kwa hiyo nchi ikaingia hasara.
“Wakati ule sisi CWT tulipendekeza kwamba ili sera hii ianze kufanya kazi, Serikali ianze kuwapeleka walimu waliomaliza kidato cha nne waanze kufanya stashahada ya walimu kwa miaka mitatu na tukaomba wapewe mikopo,” alisema.
Pamoja na kutaka kuharakishwa kwa sera hiyo, Oluoch alisema kuna changamoto mbili.
“Sera haisemi kwamba hivi kila shule ya msingi itakuwa sekondari au wanafunzi wote watakwenda kusoma shule za sekondari zilizopo? Huyo mwanafunzi atakwenda kusoma shule ipi? Kwa sababu hizo shule za sekomdari hazitoshi,” alisema.
Alifafanua kuwa, wanafunzi watakaoingia sekondari mwaka 2027 ni wale walioanza mwaka 2021 watakuwa 1,500,000, hivyo yanahitajika madarasa mapya 34,000 na walimu wapya 30,000, kwa sababu waliopo ni zaidi ya 84,000.
Alitaja changamoto ya pili ni sera kutobainisha elimu bila malipo itatekelezwaje. “Huku waraka unasema wazazi wachangie chakula, huku Serikali inasema elimu bila malipo. Nadhani tuko vizuri, lakini hayo yatatuliwe,” alisema.
Uwekezaji katika elimu
Kuhusu uwekezaji katika elimu, alisema Serikali bado haijabainisha vizuri kwamba inawekeza kiasi gani kwenye elimu msingi.
“Sasa hivi tunaelekeza asilimia 3.4 ya GDP (pato la Taifa), hatujafikia kiwango cha kimataifa cha asilimia 3.8.
“Unesco Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni na Elimu) wanasema ili tuwekeze vizuri kwenye elimu msingi lazima tuwekeze asilimia sita na Benki ya Dunia wanasema asilimia tano. Je, uwekezaji wetu unahakikisha tunanunua vifaa, madarasa, vyakula maana hao ni watoto wadogo wanahitaji kukua,” alisema.
Alishauri pia walimu watakaotumika kuwafundisha kidato cha kwanza wawe wamendaliwa.
“Mimi ningekuwa kwenye uamuzi, ningeajiri walimu wenye stashada. Hawa wanaotoka chuo kikuu wanasoma masomo ya kufundisha na jinsi ya kufundisha, lakini msingi wa ualimu unafanywa kwa wanafunzi wa stashahada,” alisema.
Kuhusu mitalaa, alishauri kuwepo na mafunzo ya muda mrefu kwa wanafunzi.
“Sisi kwenye ualimu tuna kitu kinaitwa CPD yaani Continuous professional Development (Mafunzo endelevu ya utalaamu), ndio maana hivi vyuo vya walimu vimejengwa kwa mikakati na vimewekwa kwenye mikoa, kwamba walimu wa mkoa huu waende kwenye chuo mkoa fulani kwa mwezi mmoja.
“Lakini hii ya kuwapa mafunzo walimu ya siku moja ni kufunika kombe mwanaharamu apite,” alisema.
Walimu kuajiriwa kwa usaili
Akizungumzia kauli ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliyoitia Juni 2023 kwamba walimu wanaoomba ajira watafanyiwa usaili, Oluoch alisema:
“Huko ni kudhalilisha taaluma ya ualimu.Shida iliyopo, mawaziri wetu wa elimu hawajahi kuwa walimu. Hii nchi wanadhani profesa ndiye anayefaa kuwa mwalimu.
“Utaratibu wetu unataka kuwa, mwalimu akishaajiriwa anatakiwa kuwa chini ya mwalimu mzoefu yaani ‘mentor’ angalau ndani ya mwaka mmoja. Baada ya miaka mitatu mwalimu anakwenda mafunzo ya kazini (CPD),”alisema.