Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kushirikiana na Canada kuondoa vikwazo kijinsia katika elimu

Dk Charles Mahera akifungua kongamano hilo la wadau wa uwezeshaji kupitia ujuzi.

Muktasari:

  • Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Canada kupitia mradi wa ‘Empowerment through Skills Program (ESP)’ unaolenga kuondoa vikwazo vya kijinsia katika elimu ya ujuzi kwa wasichana, unatekelezwa kwa kushirikiana na Jumuiya ya Vyuo vya Canada (CiCan) na kufadhiliwa na Serikali ya Canada. Lengo ni kuwawezesha wasichana kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki shughuli za kiuchumi.

Arusha. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada imeanzisha jitihada madhubuti za kuondoa vikwazo vya kijinsia vinavyokwamisha ushiriki wa wasichana katika elimu ya ujuzi, kupitia Mradi wa Uwezeshaji Kupitia Ujuzi (ESP).

Mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Jumuiya ya Vyuo vya Canada (CiCan), unafadhiliwa na Serikali ya Canada kwa lengo la kutoa fursa sawa kwa wanawake na wasichana katika kupata elimu ya ujuzi na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa nchi.

Akifungua kongamano la siku tatu la wadau wa mradi huo, leo Mei 20, 2025 jijini Arusha, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2024, ambayo inalenga kuhakikisha upatikanaji sawa wa elimu na mafunzo jumuishi kwa wananchi wote.

“Mradi huu unaweka msingi thabiti wa mabadiliko ya kweli katika jamii. Lengo letu ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi kupitia elimu ya ujuzi, ili waweze kuzalisha bidhaa, kujiajiri, na kuchangia maendeleo ya familia na Taifa,”amesema.

 Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Charles Mahera ambaye amemwakilisha Profesa Mkenda kwenye mkutano huo, amesema mradi wa ESP, wenye thamani ya zaidi ya Sh48.4 bilioni, unatekelezwa katika vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDCs) na mashirika ya kijamii 12 nchini, kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii na kuimarisha upatikanaji wa elimu kwa makundi yaliyoko pembezoni, hususan wasichana waliokosa fursa ya elimu ya kawaida.

Kwa upande wake Mkuu wa ushirikiano kutoka ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Carol Mundle amesema kuwa mafanikio ya elimu ya ujuzi nchini Canada yamewahamasisha kuleta mfano huo Tanzania hasa baada ya kuona changamoto za vijana na wasichana zinavyofanana.

“Changamoto za vijana wetu zinafanana na hizi za vijana wa Tanzania, tunaamini kuwa ujuzi ni chombo cha kuwawezesha wanawake na wasichana kufikia malengo yao,” amesema.

Ameongeza kuwa moja ya mafanikio ya mradi huo ni kuanzishwa kwa kozi fupi zinazozingatia mahitaji ya jamii, pamoja na mafunzo ya kina kuhusu jinsia na haki za binadamu yaliyotolewa kwa jamii ili kupunguza vikwazo vya kijinsia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi, Dk Fredrick Salukele amesema kuwa zaidi ya walimu 9,700 wamefundishwa mbinu bunifu za ufundishaji wa elimu ya ujuzi, huku vifaa vya Tehama vyenye thamani ya Sh240 milioni vikitolewa kwa baadhi ya FDCs ili kuongeza ubora wa mafunzo.