Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UDSM yapanda chati ajira duniani, ikiiweka Tanzania kwenye rekodi

Muktasari:

  • Yashika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki na ya nne Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipengele cha matokeo ya ajira kwa wahitimu (Employment Outcomes) kwenye viwango vya vyuo vikuu duniani vya QS (QS World University Rankings).

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea na jitihada za kuboresha ubora wa elimu ya juu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeweka rekodi mpya baada ya kuibuka kinara Afrika Mashariki katika maandalizi ya wahitimu kwa soko la ajira duniani.

Hatua hiyo imekuja baada ya UDSM kushika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki na ya nne Kusini mwa Jangwa la Sahara katika kipengele cha matokeo ya ajira kwa wahitimu (Employment Outcomes) kwenye viwango vya vyuo vikuu duniani vya QS (QS World University Rankings).

Katika kipengele hicho, UDSM imepata alama 85.3 na kushika nafasi ya 131 duniani kati ya vyuo vikuu 1,504 vilivyofuzu kuingia kwenye orodha hiyo, huku taasisi zaidi ya 8,800 zikifanyiwa tathmini duniani.

Tofauti na viwango vya jumla vya vyuo vikuu vinavyopima maeneo mbalimbali kama utafiti, ufundishaji na sifa za kitaaluma, kipengele cha matokeo ya ajira hupima uwezo wa chuo kuwaandaa wanafunzi kwa mazingira ya kazi, mafanikio ya wahitimu wake pamoja na mchango wao katika jamii.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayeshughulikia Tafiti, Profesa Nelson Boniphace. 

Kwa mujibu wa wataalamu wa elimu, mafanikio hayo yanaashiria kuwa wahitimu wa UDSM wanaendelea kuonekana kuwa na ushindani zaidi katika soko la ajira la ndani na kimataifa, kutokana na uwekezaji katika ubora wa ufundishaji, utafiti, ubunifu na ushirikiano na sekta mbalimbali.

Akizungumza leo Jumatano, Julai 15, 2026, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo wa UDSM anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniphace, amesema chuo hicho kilipata taarifa za kutambuliwa kwake wakati wa mkutano wa QS World University Rankings uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Profesa Boniphace amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za muda mrefu za chuo hicho katika kuhakikisha kinazalisha wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la dunia.

“Tunajivunia kutambuliwa huku kwa sababu inaonesha juhudi zetu za kuboresha ufundishaji, utafiti na ushirikiano wa kimataifa. Tutaendelea kuwekeza zaidi ili kuinua kiwango cha chuo na kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya Tanzania,” amesema.

Wataalamu wa afya wakishiriki mjadala kuhusu rasilimali watu katika sekta ya afya ulioandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa. 

Mtaalamu wa elimu, Dk Bonea Mathew, amesema kipimo cha uwezo wa wahitimu kupata ajira kimekuwa moja ya viashiria muhimu katika kutathmini ubora wa vyuo vikuu, kwa sababu kinaonesha kama taasisi zinatoa maarifa na ujuzi unaohitajika na waajiri.

“Chuo kinapopata alama nzuri katika eneo la ajira, kinatoa ujumbe kwa wanafunzi, wazazi na waajiri kuwa wahitimu wake wanatoka wakiwa na uwezo unaoendana na mahitaji ya soko la kazi. Hilo ndilo lengo kuu la elimu ya juu,” amesema.

Mafanikio hayo ya UDSM yanakuja wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza mageuzi katika sekta ya elimu ya juu kupitia uwekezaji katika utafiti, ubunifu, miundombinu ya kidijitali na maboresho ya mitaala chini ya mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET).

Kupitia mageuzi hayo, Serikali inalenga kujenga mfumo wa elimu ya juu unaozalisha wataalamu wenye ujuzi wa vitendo na uwezo wa kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mtaalamu wa elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, Dk Devotha Minquza, amesema mafanikio ya UDSM hayapaswi kuangaliwa kama ushindi wa chuo kimoja pekee, bali ni ishara ya mabadiliko katika taswira ya elimu ya juu Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), Dk Ntuli Kapologwe.

Amesema vyuo vinapofanya vizuri katika viwango vya kimataifa huongeza uaminifu wa mfumo mzima wa elimu wa nchi husika na kufungua milango ya ushirikiano wa utafiti, kubadilishana wataalamu na kuvutia wanafunzi wa kimataifa.

“Chuo kimoja kinapofanya vizuri kwenye viwango vya kimataifa, kinaongeza imani kwa mfumo wa elimu ya juu wa nchi nzima. Pia huleta fursa za ushirikiano wa kitaaluma na utafiti,” amesema.

Kwa muda mrefu, viwango vya vyuo vikuu duniani vimetawaliwa zaidi na taasisi kutoka Afrika Kusini na Afrika Kaskazini, huku nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiwa na uwakilishi mdogo.

Kutokana na hilo, mafanikio ya UDSM yanaonekana kuwa hatua muhimu kwa Tanzania katika kuonesha kuwa vyuo vyake vinaanza kushindana kimataifa, hususan katika eneo la kuzalisha wahitimu wanaoweza kuingia kwenye soko la ajira na kutoa mchango katika maendeleo ya kiuchumi.

Katika miaka ya karibuni, UDSM imeongeza ushirikiano wa kimataifa, kuimarisha tafiti, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuchochea ubunifu miongoni mwa wanafunzi na watafiti.

Hata hivyo, wataalamu wa elimu wanaonya kuwa kudumisha mafanikio hayo kutahitaji uwekezaji endelevu katika ubora wa ufundishaji, tafiti na ujuzi wa wahitimu ili kuhakikisha ushindani huo unaendelea.

Dk Minquza amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa vyuo vikuu Tanzania havilengi tena kuongeza idadi ya wanafunzi pekee, bali vinaanza kutambulika kwa uwezo wa kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la dunia.