Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kutotambua hali za watoto kunavyoathiri elimu jumuishi

Picha ikionesha wanafunzi wakiwa darasani. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kabla hata ya kufikia madarasa ya juu hasa ya mitihani, watoto wengi tayari huwa katika hatari ya kutengwa kielimu kwa sababu mahitaji yao maalumu ya kielimu hayakugunduliwa mapema.

Mbeya. Kwa maelfu ya watoto nchini Tanzania, darasa bado si mahali pa fursa sawa za kujifunza. Badala yake, ni eneo ambalo changamoto za ukuaji na  ujifunzaji huendelea kujificha bila kutambuliwa, hali inayowaathiri watoto wengi katika safari yao ya elimu.

Kabla hata ya kufikia madarasa ya juu hasa ya mitihani, watoto wengi tayari huwa katika hatari ya kutengwa kielimu kwa sababu mahitaji yao maalumu ya kielimu hayakugunduliwa mapema.

Kwa mfano, watoto wenye matatizo ya usikivu, changamoto za kujifunza, usonji, kuchelewa kuzungumza, wenye matatizo ya kuona au changamoto za kitabia,  mara nyingi hupitia hatua za awali za elimu darasani  bila kutambuliwa kama ni wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Kutokana na kutogunduliwa mapema kwa mahitaji yao, baadhi yao hupewa sifa wanafunzi wasioelewa haraka, huadhibiwa isivyo stahili au hatimaye huacha shule.

Wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza sera  ya elimu jumuishi, wataalamu wanaeleza kuwa changamoto kubwa kwa sasa si uwepo wa sera, bali uwezo wa kubaini mahitaji ya watoto mapema, yaani kile wanachokiita “hatua ya kwanza inayokosekana katika utekelezaji wa elimu jumuishi.”


Simulizi ya Amina

Kwa Amina Juma (34), mkazi wa Mkoa wa Mbeya, hali hiyo imekuwa sehemu ya maisha yake kwa miaka kadhaa.

Mwanawe mwenye umri wa miaka minane, ambaye anamuelezea kuwa ni “mwerevu lakini mtulivu darasani”, alianza kukwama kimasomo muda mfupi baada ya kuanza shule. Walimu walieleza kuwa alikuwa na ugumu wa kufuata maelekezo na kuwasiliana kwa ufasaha.

Lakini nyumbani, Amina aliona hali tofauti.

“Mwanangu alikuwa akielewa kwa urahisi nikimuonyesha kwa vitendo. Alikuwa na kumbukumbu nzuri sana ya vitu anavyoviona, lakini kila nilipompeleka shule niliambiwa huenda ni mkaidi au bado hajawa tayari kujifunza,” anasema kwa sauti ya huzuni.

Anasema kutokana na kukosa majibu ya uhakika, aliamua kumbakisha mtoto wake nyumbani kwa hofu ya kuendelea kumuweka katika mazingira yaliyomuumiza kihisia.

“Kama wazazi wengi, sikujua mahali pa kupata huduma za uchunguzi wa mapema. Niliendelea kujiuliza tatizo ni nini,” anasema.

Kisa chake kinaakisi hali ya watoto wengi nchini ambao changamoto zao za ukuaji au ujifunzaji,  huendelea kufichika hadi wanapofikia hatua ambayo msaada wa mapema unakuwa umechelewa.

Mfumo unaojengwa hatua kwa hatua

Mwaka 2022, Serikali ilitoa mwongozo wa kuanzisha Vituo vya Uchunguzi, Utambuzi, Tathmini na Malezi ya Awali (ESRAC) katika ngazi ya halmashauri, kwa lengo la kusogeza huduma za uchunguzi karibu na wananchi na kuwezesha watoto kupata msaada mapema kabla ya kuathirika zaidi kielimu.

Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa wa taratibu. Takwimu zilizowasilishwa wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji na Uimarishaji wa Vituo vya ESRAC uliofanyika Mkoa wa Mbeya,  zinaonyesha kuwa kati ya halmashauri 184 nchini, ni halmashauri 36 pekee zilizofanikiwa kuanzisha vituo vinavyofanya kazi.

Aidha, baadhi ya vituo hivyo vinakabiliwa na uhaba wa wataalamu, vifaa vya uchunguzi na miundombinu.

Wadau wa elimu wanaonya kuwa pengo hilo linaacha maelfu ya watoto bila msaada unaohitajika.

“Msingi wa elimu jumuishi ni utambuzi wa mapema. Bila hatua hiyo, elimu jumuishi hubaki kuwa dhana tu,” anasema mtafiti wa elimu maalumu wa Afrika Mashariki, Dk Ayub Timbe.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo,  kuchelewa kugundua changamoto za mtoto,  huongeza uwezekano wa kutengwa kielimu, kupunguza fursa za ajira baadaye na kuongeza unyanyapaa katika jamii.


Mfano wa Mbeya

Katika Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya, kituo cha ESRAC kinatoa taswira ya namna mfumo huo unavyoweza kufanya kazi kwa mafanikio.

Kituo hicho kinatoa huduma za uchunguzi, tathmini na rufaa kwa watoto wenye changamoto mbalimbali za ujifunzaji na maendeleo.

Kati ya Januari na Aprili mwaka huu pekee, watoto 190 walifanyiwa tathmini katika kituo hicho, jambo linaloonyesha ongezeko la mahitaji ya huduma hizo pamoja na kuongezeka kwa uelewa kwa wazazi na walimu.

Shule hiyo pia inahudumia wanafunzi 115 wenye mahitaji maalumu kupitia mbinu mbalimbali za usaidizi wa kujifunza, ikiwamo msaada wa usikivu, uoni na uwezo wa utambuzi.

Mkuu wa kituo hicho, Aida Mwakalukwa, anasema hatua ya mapema ndiyo silaha muhimu zaidi katika kuwasaidia watoto hao.

“Watoto wengi hukabiliwa na changamoto za ukuaji na ujifunzaji ambazo hazitambuliki mapema. Wanapogunduliwa huwa tayari wamechelewa katika maendeleo yao ya kielimu,” anasema.

Anaeleza kuwa vituo vya ESRAC vinawezesha watoto kutambuliwa mapema na kupata huduma stahiki, ikiwamo ushauri, rufaa na matunzo yanayohitajika.


Matumaini mapya

Kwa Amina, taarifa kuhusu uwepo wa huduma za ESRAC katika Shule ya Msingi Mwenge zimempa matumaini mapya.

Hivi karibuni amepata taarifa za huduma hizo na anafikiria kumpeleka mwanawe kwa ajili ya tathmini.

“Kama ningejua mapema, pengine mambo yangekuwa tofauti. Lakini sasa natamani tu apate msaada ili arejee shuleni kama watoto wengine,” anasema.

Kauli yake inaakisi kile ambacho wataalamu wengi wanakiona kuwa hitaji la haraka zaidi kwa sasa si kujenga vituo pekee, bali kuhakikisha jamii zinafahamu uwepo wake na namna ya kuvifikia.


Nguvu ya utekelezaji

Uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kuimarisha vituo vya ESRAC umewaleta pamoja watetezi wa elimu, viongozi wa Serikali na mashirika ya kiraia, yakiwamo HakiElimu na Child Support Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Mary Ndaro, anasema changamoto kubwa kwa sasa si uelewa wa umuhimu wa vituo hivyo, bali utekelezaji wake.

“Tunaongelea watoto ambao mahitaji yao ya kujifunza hayagunduliki kwa miaka mingi. Takribani miaka mitano tangu kuanza kwa miongozo hii, ni halmashauri 36 pekee zenye vituo vinavyofanya kazi. Hili ni suala la mfumo mzima na linahitaji hatua za pamoja,” anasema.

Anabainisha kuwa sera na miongozo ya elimu jumuishi tayari ipo chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo lililoboreshwa) pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lakini utekelezaji wake bado haujaenda kwa kasi inayohitajika.

“Ndiyo maana tumeamua kuelekeza nguvu zetu hapa. Tunaamini kupitia kampeni hii ya kitaifa tutaweza kuhamasisha uanzishwaji wa vituo zaidi vya ESRAC ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika kupata elimu bora,” anasisitiza.


Athari za muda mrefu

Wataalamu wa elimu na maendeleo ya watoto wanaonya kuwa kushindwa kupanua huduma za uchunguzi wa mapema kunaweza kuhatarisha malengo ya Tanzania ya kufanikisha elimu jumuishi.

Mtaalamu wa maendeleo ya mtoto kutoka Dar es Salaam, Maryline Kombe, anasema suala hilo si la elimu pekee bali pia la afya ya jamii na maendeleo ya uchumi.

“Watoto wasipopata tathmini mapema, hukosa fursa muhimu za matibabu au msaada wa kielimu unaoweza kuboresha hali zao kwa kiwango kikubwa. Bila msaada huo, mfumo wenyewe unawasukuma kuelekea kutengwa,” anasema.

Naye mtaalamu wa mifumo ya afya, Juma Tabu, anaeleza kuwa Tanzania inaweza kuendeleza pengo la usawa ikiwa huduma za uchunguzi zitaendelea kupatikana zaidi mijini kuliko vijijini.

“Halmashauri zisizo na vituo vya ESRAC zinafanya kazi bila taarifa sahihi kuhusu watoto wenye mahitaji maalumu. Hilo linazalisha pengo la kimfumo katika upatikanaji wa haki ya elimu,” anasema.


Njia kuelekea elimu jumuishi

Wadau wa elimu wanakubaliana kuwa uchunguzi wa mapema ndiyo lango la elimu jumuishi yenye matokeo.

Bila hatua hiyo, watoto wenye changamoto zisizoonekana wataendelea kupotea katika mfumo wa elimu, wakieleweka vibaya, kupewa taswira isiyo sahihi na kuachwa nyuma.

Lakini kwa kuimarisha mifumo ya uchunguzi na tathmini, Tanzania inaweza kubadili taswira ya madarasa yake na kuhakikisha kila mtoto, bila kujali uwezo wake, anapata nafasi sawa ya kujifunza na kufanikiwa.

Changamoto iliyobaki sasa, kwa mujibu wa wadau, si kutunga sera mpya bali kupanua mifumo inayofanya kazi, kuzifikia familia kama ya Amina na kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki bila kuonekana wala kusikika katika safari ya elimu.