Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yasisitiza masomo ya sayansi kukuza uchumi wa kidijitali

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea akitoa cheti kwa mwanafunzi aliyefanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Muktasari:

  • Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa tuzo kwa wanafunzi wa kidato cha nne na sita waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya sayansi pamoja na walimu wa masomo hayo.

Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika sekta za kimkakati, hususan elimu ya sayansi, ikieleza kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea uwepo wa wataalamu wa sayansi na teknolojia watakaoboresha huduma za jamii na kukuza uchumi.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyambea wakati wa hafla ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ya kuwatunuku wanafunzi 48 na walimu wanane waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya Taifa ya kidato cha nne ya mwaka 2024 na kidato cha sita ya mwaka 2025, iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Dk Nyambea alisema maboresho yanayofanywa na Serikali sekta ya afya yanategemea maendeleo ya sayansi na teknolojia, akieleza hata vifaa na mashine za kisasa zinazotumika hospitalini ni matokeo ya ubunifu wa kisayansi.

“Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayowezesha upatikanaji wa wataalamu wa sayansi ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yanachochewa na matumizi ya teknolojia,” alisema.

Aliwataka wazazi na walezi kuwahamasisha watoto wao kusoma masomo ya sayansi, akisema ndiyo msingi wa maendeleo ya teknolojia, uchumi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Masomo ya sayansi yana mchango mkubwa katika maisha ya watu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi. Pia, yanawafungulia vijana fursa nyingi za ajira na taaluma mbalimbali,” alisema.

Dk Nyembea alisema Serikali itaendelea kuunga mkono programu zinazotambua wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi ili kuongeza hamasa kwa vijana wengi zaidi kuchagua taaluma hizo.

Pia, aliipongeza GCLA kwa kuendeleza utoaji wa tuzo hizo, akisema zinaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha elimu ya sayansi na kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko alisema tangu Tanzania ipate uhuru, GCLA imeendelea kuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za maabara na uchunguzi wa vielelezo mbalimbali, ikiwemo vinavyohusiana na makosa ya jinai, ubora wa bidhaa na afya ya mazingira.

Alisema mamlaka hiyo, pia, inasimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali, zikiwemo za udhibiti wa kemikali na vinasaba vya binadamu huku shughuli zake zikiendeshwa kwa misingi ya sayansi.

“Hafla hii inayohusisha masomo ya fizikia, kemia, baiolojia na hisabati ni sehemu ya mchango wa GCLA katika kujenga kizazi kipya cha wataalamu wa sayansi kitakachochangia maendeleo ya Taifa,” alisema.

Dk Mafumiko alisema GCLA inaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya elimu, hususani ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi pamoja na kuwahamasisha vijana kuyapenda.

Alifafanua kuwa idadi ya wanafunzi wanaonufaika na tuzo hizo imeongezeka kutoka sita mwaka 2007 hadi 48 mwaka 2026, huku walimu wakiongezeka kutoka wawili hadi wanane.

Alisema tangu kuanzishwa kwa mpango huo, wanafunzi 480 na walimu 64 wametunukiwa kwa kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.

Katika hafla hiyo, wanafunzi 48 wa kidato cha nne na sita walioshika nafasi ya kwanza, pili na tatu kitaifa katika masomo ya fizikia, kemia, baiolojia na hisabati walitunukiwa pamoja na walimu wanane waliochangia mafanikio yao.

Kwa upande wake mmoja wa walimu waliopewa tuzo katika hafla hiyo, Emmanuel Urassa amesema wazazi wanapaswa kuwekeza zaidi kwa watoto wao ili wafanye vyema kwenye masomo ya sayansi.