Wadau wa elimu wahamasisha vijana kujiunga na mtalaa wa amali
Mratibu wa mtandao wa elimu Tanzania, Martha Makala akiwa kwenye trekta likiendeshwa na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Msangano, Rahabu Siame anayesoma fani ya kilimo. Picha na Denis Sinkonde
Muktasari:
- Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Martha Makala, amesema mtalaa wa amali ni muhimu kwa vijana kwani umelenga kuwajengea ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira la sasa.
Songwe. Wadau wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) wamewataka wazazi na walezi nchini kuwahamasisha watoto wao kujiunga na masomo ya mtalaa wa amali, ulioanzishwa kwa lengo la kuwawezesha vijana kujitegemea na kukabiliana na changamoto za ajira.
Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya wadau hao katika Shule ya Sekondari Msangano, iliyopo wilayani Momba mkoa wa Songwe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa.
Shule hiyo ni miongoni mwa zinazotekeleza mtalaa wa amali kwa majaribio tangu mwaka 2024, na wanafunzi hupatiwa mafunzo ya kilimo cha mbogamboga, mazao ya nafaka pamoja na afya ya mifugo.
Akizungumza katika ziara hiyo leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, Mratibu wa Kitaifa wa TEN/MET, Martha Makala, amesema mtalaa wa amali una umuhimu mkubwa kwa vijana kwa kuwa unalenga kuwajengea ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira la sasa.
Amesema si lazima kila mwanafunzi afuate masomo ya nadharia pekee, kwa sababu kuna fursa nyingi katika kada za ufundi na ubunifu zinazoweza kuwawezesha vijana kujiajiri na kujipatia kipato.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Msangano, Rahabu Siame akimpa maelekezo mratibu wa mtandao wa elimu Tanzania, Martha Makala namna wanavyojifunza kwa vitendo mtaala wa amali shuleni hapo. Picha na Denis Sinkonde
“Ni muhimu kubadili mtazamo wa jamii kuhusu elimu ya amali. Siyo elimu ya waliofeli, bali ni njia mbadala yenye tija kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Makala.
Aidha, Makala amesema mtalaa huo unaweza kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo na ufugaji, na ukiboreshwa ipasavyo unaweza kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za kiuchumi zinazowakabili vijana wengi nchini.
Amesema katika shule hiyo wamejionea uwepo wa mitambo ya kilimo pamoja na wanafunzi wakionesha ujuzi kwa vitendo, ikiwemo kuendesha trekta na kushiriki katika huduma za afya ya mifugo.
“Tunatamani kuona shule nyingi zaidi zikianzisha mtalaa wa amali ili kuongeza maarifa ya vitendo kwa vijana,” ameongeza.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Momba, Florence Haule, amesema mtalaa huo ulianza kutekelezwa katika shule hiyo mwaka 2024, ukiwahusisha wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha tatu katika mafunzo ya kilimo cha mbogamboga, mazao ya nafaka na afya ya mifugo.
Hata hivyo, amebainisha kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi, hususan katika fani ya afya ya mifugo, hali inayowalazimu kutumia mifugo ya wananchi kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.
“Kwa sasa hatuna vitendea kazi vya kutosha katika fani ya afya ya wanyama na uzalishaji. Walimu wanajitahidi kutumia mifugo ya jamii kuwapa wanafunzi ujuzi wa awali utakaowasaidia kujiajiri baada ya kumaliza masomo,” amesema Haule.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mtalaa huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Msangano, Frola Kawonga, amesema shule imepokea ruzuku ya Sh366.29 milioni kutoka serikalini kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika fani za kilimo.
Amesema kupitia mtalaa huo, shule imefanikiwa kulima jumla ya hekta 18 za mazao mbalimbali, zikiwemo hekta 10 za mahindi, hekta tatu za maharage, hekta nne za mtama na hekta moja ya alizeti.
Hata hivyo, Kawonga ameomba Serikali kuendelea kuisaidia shule hiyo kwa kuipatia fedha za kununua mifugo itakayosaidia katika ufundishaji wa fani ya afya ya wanyama na uzalishaji.
Naye Rahabu Siame, mwanafunzi wa kidato cha tatu shuleni hapo anayesomea fani ya kilimo, amesema mafunzo anayopata yamembadilishia mtazamo kuhusu ajira, akieleza kuwa sasa anaona uwezekano wa kujiajiri kupitia sekta ya kilimo.
“Awali nilidhani kilimo ni kazi ngumu isiyo na faida, lakini sasa nimejifunza mbinu za kisasa zinazoweza kunipatia kipato. Mtalaa huu unatoa ujuzi wa vitendo badala ya nadharia pekee,” amesema Siame.