FIESTA 2016: Ni Wizkid Vs Bongo Fleva na Singeli

Staa wa Nigeria, Ayodeji Ibrahim Balogun ‘Wizkid’

Muktasari:

Katika burudani inayotarajiwa kuangushwa leo katika viwanja vya CCM Kirumba, staa wa Nigeria, Ayodeji Ibrahim Balogun ‘Wizkid’ atatumbuiza.

Imoooo!…Ndiyo kauli mbiu ya Tamasha la Fiesta 2016. Baada ya kupata likizo mwaka mmoja, leo hii tamasha hili linakwenda kuzinduliwa rasmi Mwanza kwa kuangusha burudani kwa wakazi wote waishio mkoani humo na maeneo ya karibu.

Katika burudani inayotarajiwa kuangushwa leo katika viwanja vya CCM Kirumba, staa wa Nigeria, Ayodeji Ibrahim Balogun ‘Wizkid’ atatumbuiza.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2012 pale Lagos Nigeria, alipiga shoo mpaka Chriss Brown akamkubali, lakini safari hii mkali huyo wa wimbo Ojuelegba na Baba Nhla, anatamba kuwa lazima ahakikishe anafanya shoo ya kumbukumbu Mwanza. Hii itakuwa mara ya pili kwa Wizkid kuja Tanzania, baada ya mwaka jana kutumbuiza kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.

Tofauti na miaka mingine, mwaka huu kumefanyika usajili. Usajili huu umekuwa ukifanyika katika pande tofauti hasa zile ambazo wasanii wanatokea, wengi walifuatwa katika maskani zao hali iliyoonyesha heshima na kukua kwa sanaa nchini.

Katika orodha ya kwanza ya wasanii watakaotumbuiza ilitajwa pale B.O.B Kinondoni na jumla ya wasanii sita walitajwa na kusainishwa mikataba pia kukabidhiwa jezi zao maalumu za Fiesta 2016.

Wasanii waliotajwa ni pamoja na Ben Pol, Maua Sama, Bill Nas, Rubby, Mr Blue, Chegge, Msami na Christian Bella.

Wengine waliosajiliwa Mwenge jijini Dar es Salaam ni pamoja na Navy Kenzo, Fid Q, Weusi, Ommy Dimpoz, Baraka The Prince na Nandy.

Usajili uliendelea na wengine walisajiliwa Agosti 11 katika Maskani ya Tip Top Connection iliyopo Manzese jijini Dar es Salaam.

Wasanii Raymond wa WCB, Shilole aka “Shishi Baby”, Dogo Nigga, Dayna Nyange na Tip-Top Connection yaani Madee, Dogo Janja na Tundaman.

Licha ya burudani nyingine, Dansi la Fiesta na Super Nyota ni baadhi ya vipengele ambavyo havijaachwa nyuma katika kukamilisha tamasha hilo kwa mwaka huu.

Ni Fiesta ya tofauti

Ukilinganisha jinsi ilivyokuwa miaka iliyopita, Fiesta ya mwaka huu imekuja tofauti kuanzia namna ya kuwapata wasanii na hata katika upangwaji wa matukio.

Mwaka huu tiketi za Fiesta zimeanza kuuzwa kupitia mtandao wa simu jambo ambalo miaka ya nyuma halikuwapo.

Ushindani kwa wasanii wa kike kwa sasa umeongezeka kwani wengi wanafanya vizuri, hivyo mwaka huu Fiesta inatarajia kutakuwa na mwamko katika majukwaa hayo kulingana na namna wasanii hawa walivyojipanga.

Wasemavyo wasanii

Madee

Ikifika msimu kama huu wanamuziki tunaona ni msimu wa mavuno na unaonyesha thamani ya mwanamuziki, kila mmoja angetamani kujiunga lakini kwa sababu tupo wengi waandaaji hawawezi kutuchukua wote.

Sisi tuliobahatika hatuwezi kusema kwamba ndiyo wakali sana hapana, tunashkuru hii inaonyesha kabisa kwamba nafasi tunayopewa tumekuwa tukifanya vizuri, pindi Fiesta inapomalizika utaona wasanii wanajenga, wana magari mazuri, wanasoma na wengine wanasomesha ndugu zao… ni msimu ambao wanamuziki wanauheshimu sana.

Rayvan

Naona Fiesta ni shoo za taifa kwa kuwa ni kubwa sana nchini, kila mwaka ukijiona upo humu ujue wewe ni bora kwa hiyo kwa mimi ambaye nilikuwa napigana siku zote ifike siku na mimi nipate nafasi kwenye sanaa ya muziki, ninapoona naingia katika Fiesta kama msanii kwangu ni bahati.

Kwa sababu muziki wangu unakua na watu wananipokea, kuna sehemu nzuri naenda kwa hiyo nashukuru sana inanitia moyo kwa kidogo nilichonacho wananikubali.

Maua Sama

Kiukweli kuwa mmoja ya wasanii waliosaini kwangu nashukuru naona ni hatua kubwa kwangu, tangu nianze muziki 2016 umekuwa mwaka mzuri kwani mambo mengi yananitokea na ninajiona kana kwamba nimekua kimuziki na hata katika fani ya sanaa.

Ni msanii ambaye kazi zangu zinaanza kuonekana na ninaanza kula matunda yake kutokana na jitihada ninazozifanya lakini kutokana na muziki nimepata mbunifu ambaye anajulikana kila kona, ananifaa na amekuwa akinisaidia na kunipa sapoti katika mambo yangu mengi ambayo sasa yanakwenda vizuri kwa kweli ananivalisha na mengine mengi anaitwa Noel. Kama siyo muziki nisingefikia hatua hii.

Fiesta imenifanya itanifanya nipate mengine mengi zaidi. Naona ni kitu kikubwa kwangu nakithamini kwa sababu naona imekuja wakati mwafaka.

Man Fongo

Wana Mwanza wakae mkao wa kula kwa sababu nikisema Man Fongo ngaa Mwanza, namaanisha kwamba nakuja. Mwaka huu ni wa kipekee kwa sababu sijawahi kufanya shoo za Fiesta hivyo nimejiandaa kuvunja miiko.

Ninachowaambia wakae mkao wa kula, raia Singeli wameipokea na ni muziki wa Tanzania.

Dayna

Namshkuru sana Mungu unajua wasanii wa kike tupo wengi ila nimebahatika. Mashabiki wangu wana nguvu ya kufanya hayo yote yaliyotokeza. Niliahidi nimejipanga nitafanya kazi kwa wakati na haya ndiyo matunda yanayoonekana leo, Fiesta ni shoo kubwa ambayo wasanii wengi wanapenda kuwapo lakini ni vigumu kwa sababu walengwa ni wanaohitajika kutokana na kazi zao na mazingira waliyoyatengeneza. Nashukuru kwa kupata hii fursa.