Jeniffer Mgendi: Kutoka uimbaji hadi uigizaji

Jeniffer Mgendi

Muktasari:

Jeniffer aliyeanza uimbaji miaka 19 iliyopita, amesema katika filamu hiyo ambayo ipo katika mchakato wa kutengenezwa hivi sasa, imewashirikisha waigizaji wakubwa wa filamu ambao majina yao yatatajwa baadaye, huku ikiwachanganya na waimbaji wa muziki wa injili ambao wameshawahi kufanya kazi ya kuigiza akiwamo Bahati Bukuku, Cheristina Matai, Jeniffer Mgendi na wengineo.

Wakati akiendelea kutamba na video yake mpya ya “Hongera Yesu”, ambayo imewashirikisha waimbaji na wasanii mbalimbali kama Bahati Bukuku, Godliver Vedastus, Boniphace Mwaitege, Christine Matai na wengineo, Jeniffer Mgendi Juni anatarajia kuachia filamu ya “Shelina”.

Jeniffer aliyeanza uimbaji miaka 19 iliyopita, amesema katika filamu hiyo ambayo ipo katika mchakato wa kutengenezwa hivi sasa, imewashirikisha waigizaji wakubwa wa filamu ambao majina yao yatatajwa baadaye, huku ikiwachanganya na waimbaji wa muziki wa injili ambao wameshawahi kufanya kazi ya kuigiza akiwamo Bahati Bukuku, Cheristina Matai, Jeniffer Mgendi na wengineo.

Akizungumza na Starehe, Mgendi alisema filamu ya “Shelina” inahusu changamoto mbalimbali anazoweza kupitia mtoto wa kike na jinsi imani kwa Mungu inavyoweza kuwa ufumbuzi kwa changamoto hizo .

“Filamu hii kama zilivyo filamu zangu zingine itakuwa na nyimbo nne ambazo mbali na kuongeza nakshi, lakini pia zimebeba ujumbe wa maonyo na kufariji mbali na kuburudisha kwa hiyo nawaomba mashabiki wangu wote na wapenzi wote wa injili na wale wa sanaa wasikose kabisa filamu hii pindi itakapoingia sokoni,” anasema.

Mbali na filamu hiyo, Jeniffer ametoa filamu za Joto la roho, Teke la Mama na Chaimoto kwa nyakati tofauti. Pia aliwahi kutamba na albamu ya “Mchimba Mashimo” iliyotoka miaka ya 2006 na bado inaendelea kuwashika mashabiki hadi sasa.

Jeniffer amesema mwaka huu ni mwaka wa kazi kwake hivyo muda mwingi atakuwa bize studio na “location” (maeneo ya uchukuaji picha za video), kwa ajili ya kuandaa kazi zake mbalimbali.

“kwa kweli mwaka huu nataka nifanye kazi kama punda na kama Mungu atanipa uzima natarajia kumalizia viporo vya kazi nilizojipangia kufanya mwaka jana, mfano video ya Dhahabu ambayo ni ya nyimbo zangu za zamani,” alisema na kuongeza:

“Pia mbali na filamu ya Shelina ambayo itatoka sambamba na albamu ya kusikiliza ya nyimbo, zitakazotumika kwenye filamu hiyo, pia natarajia kutoa ‘collection’ ya nyimbo za vichekesho lakini zenye ujumbe mbali na kuburudisha”.

Mwimbaji huyo aliyezaliwa miaka 40 iliyopita jijini Dar es Salaam, katika familia ya watoto watatu akiwa ametanguliwa na kaka zake wawili, anaeleza kuwa alipata elimu yake katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga na kuanza uimbaji mwaka 1995 na huku akifanya kazi kadhaa zikiwamo ualimu na ukutubi, lakini tangu mwaka 2007 aliamua kuacha kazi za kuajiriwa na mpaka leo anafanya shughuli zake binafsi.

Anaeleza kuwa kuna waimbaji wengi walikuwa wakimvutia na kumhamasisha katika uimbaji lakini miaka hiyo alivutiwa zaidi na Jim Reeves na Yvonne Chakachaka ambao anasema kuwa alikuwa akisikia nyimbo zao, aliburudika zaidi na kutaka kuwa kama wao.

Jeniffer anaelezea waimbaji wa injili kuhusishwa na mambo ya kidunia na kusema “kuna watu wengine hata kupiga makofi tu wakati unaimba kwao ni kidunia la muhimu ni kwamba mradi mashairi na ujumbe unampa Mungu sifa na utukufu, binafsi sioni ubaya wowote wa nyimbo za dini kuwa na midundo na wala sijawahi kusoma kwenye biblia sehemu inayokataza kupiga midundo sanasana nimesoma Zaburi ikisema pigeni kwa ustadi,” anasema.

Jeniffer anaeleza tofauti ya muziki wa injili na bongo fleva kwa kusema kuwa “ujumbe wa muziki wa Injili unaelekea katika kuijenga roho ya mtu, wakati muziki wa Bongo fleva asilimia kubwa unalenga katika mambo yahusuyo mwili tena mara zingine unapotosha roho ya mtu (mfano) nyimbo za kuhamasisha ngono, kuutukuza mwili, kujisifia, kusifia wanawake na hata ukitazama hata video za Bongo fleva nyingi zina vitendo ambavyo havifai hasa kwa watoto tofauti na nyimbo za Injili,” anasema.

Anasema tofauti nyingine ni wanamuziki wa injili wanakuwa na mipaka kutokana na imani waliyonayo tofauti na wale wa Bongo fleva wengi wana ile hali ya “full kujiachia” kwa hiyo si ajabu kwao kuvaa jukwaani nguo zisizo na maadili, kupigana, kutumia vileo na mambo mengine jambo ambalo huwezi kuliona kwa wanamuziki wa Injili.

Akiwataja wanamuziki wanaomvutia anasema kuwa ni Rose Muhando kwa mashairi yake na anavyosukuma sauti yake na Upendo Kilahiro kwa jinsi anavyoweza kucheza na sauti yake kwa waimbaji wa nje anavutiwa na Yvonne Chakachaka na Rebecca Malope.

Jeniffer anasema tangu awe muimbaji amejifunza mambo mengi ikiwemo kuifahamu vizuri nchi yake, kwani amesafiri katika mikoa na wilaya nyingi ambazo asingefika huko kama siyo muziki.

Akizungumzia changamoto anazokutana nazo anasema ni nyingi, lakini baadhi ni wizi wa kazi zake jambo ambalo linamrudisha nyuma kimaendeleo kwa kumkosesha mapato.

Nyingine anasema kuwa ni umaarufu ambao mara zingine unamnyima uhuru binafsi pia anashindwa kufikia matarajio fulani ya wanajamii na wao hutafsiri wanavyopenda.