‘Wanawake wanapenda kupigiwa simu, wanaume hawapendi’
Muktasari:
Baada ya dakika kama 10 simu yake inaita tena, anaitizama anasonya, anapunguza sauti halafu anaiweka mezani, mazungumzo ya kawaida kati yangu na yake yanaendelea dakika nane baadae inapigwa tena anaitizama na kusimama anajipangusa kichwa huku amekunja uso.
Nimekaa pembeni ya mtu anapigiwa simu ya kwanza anapokea na kuzungumza kama mtu mwenye haraka ya kufanya jambo fulani, inaita tena na hali ni ilele na majibu ya mkato.
Baada ya dakika kama 10 simu yake inaita tena, anaitizama anasonya, anapunguza sauti halafu anaiweka mezani, mazungumzo ya kawaida kati yangu na yake yanaendelea dakika nane baadae inapigwa tena anaitizama na kusimama anajipangusa kichwa huku amekunja uso.
…”Unasemaje? …enhe enhe eeeh… hicho ndiyo kinachokufanya unipigie kila mara, nipo kazini na nina kikao hadi saa mbili usiku.”(anasonya kisha anaikata simu hiyo).
Napata shauku ya kufahamu hasira na hicho kikao kwa sababu kuna mahali tunakwenda pamoja muda siyo mrefu.
“Huyu mwanamke mpuuzi sana, tangu asubuhi ameshapiga simu zaidi ya 20 kitu cha maana hakuna zaidi ya kuuliza upo wapi, unafanya nini, utarudi saa ngapi, utaniletea nini.
“Ananichosha, muda wote anataka kufahamu kama nipo mahali salama au laa, sitaki kufuatwa fuatwa ndiyo maana nimejibu kwa hasira. Nisingefanya hivyo angeendelea lakini atatulia sasa baada ya kumfokea.”ananieleza mwanaume huyo wa makamo.
Mkazi wa Yombo Buza, jijini Dar es Salaam, Zuri Abdallah anachukulia mumewe kutopokea simu ni kwa sababu ana wanawake wengine na akipigiwa simu na mumewe moyo hulipuka na kuhisi kuna tatizo kwa sababu siyo kawaida yake kufanya hivyo.
Mtaalamu wa saikolojia Modester Kamongi anasema siyo kwamba wanaume hufanya makusudi kuikwepa simu bali kawaida hawataki kutawaliwa.
Anafafanua kuwa hiyo hali ipo tangu enzi na enzi na imejengeka hivyo, lakini kwa kawaida wanawake ni watu wanaotaka kukumbatia, kuenziwa, kuonyesha mapenzi kwa kufanya haya na yale ikiwamo kununua zawadi.
“Kuna nyumba nyingine hadi kisu kipo cha baba na marufuku mtu kukigusa au kukitumia na mlinzi mkuu ni mama, ”anasema Kamongi.
Kamongi anasema ni ngumu kumbadili mwanaume akafanya sawa na wanawake wanavyotaka kwa sababu uhalisia wa tabia zao ni tofauti.
“Halafu licha ya kuwa hawapokei simu, siyo kwamba hawawapendi wake zao bali wao mapenzi huwa na nafasi katika hatua za awali baada ya kukamilisha huamini mwanamke ni wao, ndiyo maana wakimfumania kwa bahati mbaya huwa wakali sana kwa sababu wanajiamini.
“Tofauti na wanawake ambao ili wajiamini uhitaji zaidi kuwa karibu na waume, wapenzi wao na hawajiamini sana ndiyo sababu ya kupiga simu kila mara, ” anasema.
Mwandishi na mtaalamu wa saikolojia wa nchini Marekani, Renee Wade anasema kuwa wanaume hutumia simu kama kitendea kazi ambacho huwasaidia kutoka hatua A kwenda B, kukusanya taarifa au kutoa taarifa.
Renee ambaye huchapisha makala zake katika mtandao wa Thefeminine Woman anasema vivyo hivyo hutumia simu kama kukusanya taarifa za kumpata mwanamke kwa ajili ya kuoa au mpenzi.
Anasema hakuna sababu ya moja kwa moja zaidi ya mmoja kati yao kutokubali kuwa kila upande watu wake wameumbwa kwa tabia na majukumu tofauti.
Anaeleza kwa mujibu wa wanaume kadhaa aliofanya nao mahojiano, wengi walisema wanafanya vitu muhimu kwa faida yao kwanza.
Anasema baadhi yao walisema hawapigi wala kupokea simu zilizokithiri siyo kwa sababu hawawapendi wenzi wao, bali kwa sababu wanajua watakachoulizwa na kinakuwa hakina nafasi kwa wakati huo.
“Mwanaume hajali maumivu ya mwanamke anayopata kwa kujibiwa kwa ukali, akipiga simu au ya kutopigiwa kwa sababu anaamini atakutana naye muda ukifika na hakitaharibika kitu.”
Renee anaitaja sababu nyingine inayowafanya wanaume wasipokee simu au kupiga ni kukwepa lawama na kusikiliza sauti za manung’uniko na maombolezo ya wenzi wao.
“Mara chache mwanamke anapopigiwa au kupiga simu akakosa malalamiko, anafurahia kupigiwa lakini akipigiwa anahoji, analalamika, ”anasema Renee.
Wataalamu wanazitaja sababu hizi kuwa ndiyo huwakimbiza wanaume kupiga, kupokea simu za wenza wao.
• Wanaume kipaumbele chao cha kwanza ni kile wanachoona kina umuhimu kwao na simu siyo sehemu ya vitu hivyo.
• Ni mara chache kutumia muda wao kwenye simu kama kifaa cha mawasiliano siyo kitu wanachotumia kufanya majadiliano, huitumia kufanya mambo ya msingi zaidi. Lakini ni hadithi tofauti linapokuja suala hilo kwa wanawake, wao hutumia muda mwingi kuzungumza kwenye simu, huku waitamani zaidi kuzungumza na wenza wao kupitia kifaa hicho mara kwa mara.
• Wanaume kwa kawaida hutumia simu kwa madhumuni fulani hususani masuala ya kazi ikiwa ni tofauti kabisa na wanavyoitumia wanawake. Wanaume pia hutumia simu kutafuta habari, taarifa au kuwasilisha ujumbe fulani wa kikazi.
• Wanawake hutumia simu kuwasiliana na rafiki zao kwenye mitandao ya kijamii, wakati wanaume hufanya hivyo wanapotaka kujenga uhusiano mpya na mwanamke.
• Katika hatua hii ya awali ya kujenga uhusiano wa kimapenzi , hutumia muda mwingi kuwasiliana na wanawake ikiwa ni jitihada mpya za kuwateka kimapenzi , kazi yao huwa rahisi kwa sababu baadhi ya wanawake hupenda maisha ya aina hiyo.
• Kama inavyofahamika wanaume hutumia muda, fedha wanapokuwa wanajenga uhusiano mpya, ikiwamo kukaa hadi usiku wote kuzungumza kwenye simu, na wakati mwingine kusahau kula, kulala na kutumia muda huo kuzungumza kwenye simu kwa dhamira maalumu.
• Kutopigiwa simu, kutopokelewa simu ni matokeo yanayotokana na mwanaume au wanaume kufanikiwa kuwapata wanawake waliokuwa kwenye mitego yao na kuamini hakuna anayeweza kuvuruga walichokiunda kwa gharama, huku wanawake wakiwa hawajiamini na kuamini kuwa yupo anayezungumza na mwenza wake kama ilivyokuwa kwao.