Anti Bettie: Ananiita nyumba ya wageni tukajadili kuhusu posa na ndoa yetu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mimi ni binti wa miaka 17, nimemaliza kidato cha nne sijabahatika kuendelea na elimu, kuna mwanamume amesema anataka akajitambulishe kwetu kwa ajili ya kunioa. Lakini siku mbili hizi ananilazimisha nikutane naye nyumba ya wageni ili tukazungumze vizuri kuhusu mipango ya ndoa. Kimwonekano ni mtu na heshima zake.

Anataka tukajadili posa na ndoa kwenye nyumba ya kulala wageni

Anti Bettie shikamoo.

Mimi ni binti wa miaka 17, nimemaliza kidato cha nne sijabahatika kuendelea na elimu, kuna mwanamume amesema anataka akajitambulishe kwetu kwa ajili ya kunioa. Lakini siku mbili hizi ananilazimisha nikutane naye nyumba ya wageni ili tukazungumze vizuri kuhusu mipango ya ndoa. Kimwonekano ni mtu na heshima zake.

Je, nikienda anaweza kunifanyia kitu kibaya?

Moyo wa mtu msitu, siwezi kusema moja kwa moja kuwa atakufanya kitu kibaya, lakini sifikirii kama ni busara kwenda kujadili suala muhimu kama hilo katika nyumba ya wageni.

Hujui ni kiasi gani unamvutia na hupata hisia gani unapokuwa karibu naye, mkikaa wawili eneo la faragha anaweza kupata kishawishi na kukutamani.

Ikifika hali hiyo na mpo wawili ni rahisi kukushawishi vinginevyo.

Kama ana nia ya kuleta posa kwenu amekuambia na umemkubalia huko faragha mnakwenda kuzungumza nini?

Atoe kwanza posa awe mchumba wako na anapotaka kuzungumza na wewe akuombe nyumbani wazazi wamkubalie au wamkatalie kwa sababu bado upo chini ya wazazi, walezi.

Kuwahusisha wazazi anapotaka kuzungumza na wewe ni muhimu, ukizingatia hata kukuoa inabidi akusubiri angalau utimize miaka 18, kwa kuwa husomi suala lako linajadilika lakini siyo faragha kama anavyotaka.

Nina mpenzi nampenda sana, lakini tukiwa nje kwenye watu anajifanya kama hanijui, hanitafuti hadi nifanye hivyo. Lakini ananilazimisha nimzalie kwa madai nikifanya hivyo kila kitu kitakuwa sawa.


Nifanyeje, ninampenda lakini simuelewi kama ananipenda au anapita njia

Huyu ananishangaza hata mimi ujue, haiwezekani mwanamke unayetaka kuzaa naye lakini hutaki watu wajue kama mna uhusiano. Simaanishi mtangaze kama mpo pamoja, hapana ila hapaswi kukuficha kiasi cha kujifanya kama hakujui.

Halafu huanza mapenzi, kuzaa huja baadaye, kwa nini kipimo chake kiwe kumzalia kwanza?

Angalia usije ukawa sehemu ya kuzalisha watoto wasiopata malezi ya baba, ilhali wapo wanakula bata mahali.

Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati hana visingizio.

Kama ana nia na wewe anatakiwa afanye utaratibu wa kisheria wa kuishi pamoja, tofauti na hapo msikilize kwanza...