Chanzo mauaji ya wanandoa hiki hapa

Taarifa za mauaji ya wanandoa zinazidi kuongezeka kiasi cha kukera na kutisha. Haupiti mwezi, na sasa wiki, bila kusikia taarifa za mume kumuua mkewe kwa sababu mbalimbali, kuu ikiwa wivu wa kimapenzi, kugombea mali na mambo mengine kama hayo.

Je, mauaji haya yanasababishwa na wivu wa kimapenzi au ujinga, tamaa, uvunjifu wa maadili na mengine mengi? Kama jamii na taifa tunachukua hatua gani kupambana na tatizo hili? Tumekubali kuwa mashahidi na wahanga kana kwamba hatuwezi kuingilia kati?

Tunaweza kusema kuwa ukatili katika ndoa unaweza kusababishwa na yafuatayo:

Mosi, kuingia katika ndoa bila maandalizi na utafiti wa kutosha. Haya yakifanyika, wahusika huwa tayari kusomana na kukubali mapungufu yao na kuyafanyia kazi, kujiboresha na kukjiongeza.

 Pili, kutojua au kukumbuka kuwa duniani tunaisha mara moja. Hivyo, sisi binafsi hupenda kutumia kila fursa na kuifaidi, hasa ikizingatiwa hatujui tutakufa lini. Kuhakikisha hatupotezi fursa hii adhimu, hukosoana bila kutishana, kudharauliana tukijua sisi si wakamilifu wasiojua kila kitu.

Tatu, kutojua umuhimu wa amani. Hivyo, tangu tulipokubaliana kufunga ndoa, tuliahidiana kujenga familia ya amani ili tuwarithishe watoto wetu bila kushawishi, bali kuwapa fursa waangalie wenyewe waige.

 Nne, kutojua na kukubali kuwa hakuna binadamu mkamilifu hata mmoja. Badala yake kuna watu wenye mapungufu ambao ni vizuri kukubali kuishi nao tukirekebishana tukiamini kuna siku tutafanikiwa kupunguza mapungufu yetu na kuyageuza fursa.

 Tuangalie vyanzo vya ukatili katika ndoa. Kwa uzoefu wetu, kama wanandoa na mmoja wetu mwanataaluma ya mahusiano na usuluhishi wa migogoro, tunaomba tujielekeze kwenye sababu kuu zifuatazo ambazo zaweza kuwa vyanzo vikuu vya mauaji na ukatili katika taasisi hii adhimu na muhimu ya ndoa.

 Mosi, wanandoa wengi hudhani wameoa au kuolewa na malaika, wasijue ni binadamu wenye mapungufu, kama vile:

A) Ujinga ambapo wahusika hufanya mambo bila kujipa nafasi ya kutafuta lau ushauri na ujuzi juu ya taasisi hii isiyoepukika katika maisha.

 B) Wapo wanaosukumwa na tamaa, iwe ya ngono au vitu vingine kama elimu, mali na mambo mengine, ukiachia mbali upofu na haraka kimaamuzi. Kuna makabila nchini ambapo wazazi huwaambia mabinti zao kutafuta wanaume wenye fedha au taaluma zinazoingiza fedha kama vile biashara, udaktari, uhasibu, uanasheria, au zenye kuvutia rushwa bila kuangalia watu wanaoolewa nao.

Unaweza kupata mume mwenye sifa hizo hapo juu, mfano mfanyabiashara wa mihadarati, jambazi au hata mnyanyasaji na muuaji. Mara nyingi, makabila haya ni ya watu wavivu kutafuta na wanyonyaji wanaowageuza mabinti zao vitegauchumi na ‘chuma ulete’ wasijue madhara yake yanaweza kuwa makubwa hata vifo.

Hawa ni wengi. Huwa hawajiamini na wanaamini katika waganga wa kienyeji na ujinga mwingine. Mara nyingi, wanaofuata ufanisi au utajiri kupitia ndoa hujikuta kwenye matatizo, kama vile kutothaminiwa na kupendwa kama walivyotegemea, hasa kwa wale wanaojua walichofuata.

Japo si wahanga wote wako kwenye kundi hili. Wanaweza kuvutiwa na vitu badala ya utu kwa vile walifuata vitu na hawakuwapenda wenzao kimapenzi bali kivitu. Wengine wanapozidiwa, ima huwaua waume au kuwageuka na kutaka waachane ili kugawana au kupewa mali kiasi cha kuwaacha watoto kwenye matatizo yasiyo na sababu zaidi ya tamaa.

Pili, wapo wanaoingia kwenye taasisi kifasheni au kutoa nuksi wasijue wanaingia kwenye taasisi ya kudumu ambapo mhusika hapaswi kuangalia vitu vya muda. Mfano, wale wanaopeana mimba au kuzidiana akili. Kuna wasichana wengi, hasa ambao wameshakata tamaa.

Wakipata mtu wa kufanya nao urafiki, watafanya kila mbinu lau ‘watoe nuksi.’ Mara nyingi, hawa huwapata wanaume wasio na uzoefu na kuwasukumiza kwenye ndoa ambazo, mara nyingi, huishia kuvunjika pale wenza wao wanapokomaa na kukengeuka kwa kujikuta wameingizwa mkenge.

 Tatu, sababu nyingine ni uvunjifu wa maadili. Mfano, kutegesheana mimba au kufungishana ndoa za mkeka bila kujua udhaifu na ubora wa wenzi wao kwa vile wahusika walivunja maadili na kuanza kufanya mambo yasiyokubalika kimaadili kijamii. Hili linawakumba sana wanaume wazinzi na wanaotaka kuchezea watoto wa wenzao.

Nne, ulimbukeni wa kuiga mambo nao unaweza kuwa sababu katika wakati huu wa mitandao ambapo wanandoa hukutana kwenye mitandao na kuamua kuoana bila kufanya utafiti na kujipa muda wa kutosha.

Juzijuzi nchini Marekani, binti mmoja wa Mkenya aliyekuwa akisomea unesi, alipotea baada ya kupata mwanaume wa kizungu kwenye mtandao ambaye anatuhumiwa kumuua na kutumia akaunti yake ya benki iliyokuwa na dola kama laki tatu hivi. Je, ni wauaji wangapi wamo kwenye dating sites?

Tumalizie kwa kushauri jamii ianze kurejea kwenye maadili na ijiulize wapi ilikosea. Kimsingi, ndoa ni taaluma. Inahitaji maandalizi na muda wa kupata ujuzi na kufikia uamuzi. Kikubwa zaidi ni upendo wa kweli na kuvumiliana kwa wanandoa.

Kwa wale wanaoona kuwaua wenzao ni jibu, si jibu. Unamuu kwani ulimuumba? Wewe utaishi milele? Kama una hasira, tafuta namna ya kuzituliza kuliko umuue mwenzako, umuache utafute akufaaye, ingawa unaweza kumkimbia mjusi ukamkumbatia mamba.

(Imeandikwa na: Nkwazi Mhango & Nessa Mhango)