Mke adaiwa kumbana ‘nyeti’, kumchoma kisu mumewe hadi kumuua

Waombolezaji wakiwa kwenye msiba wa Julius Rubambi 

Muktasari:

  • Kifo cha Ofisa Kilimo wa Kata ya Neruma Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Julius Rubambi  aliyefariki dunia juzi katika Hospitali ya Kibara kimedaiwa kusababishwa na ugomvi baina yake na mkewe, Elizabeth Steven (30), anayedaiwa kumjeruhi huku chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.

Bunda. Uchunguzi wa awali umebaini kifo cha Ofisa Kilimo wa Kata ya Neruma Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Julius Rubambi (39) kimesababishwa na kuvuja damu nyingi kwenye majeraha yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Pia uchunguzi huo umebaini mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha yaliyotokana na kuminywa na kung’atwa maeneo mbalimbali ikiwemo sehemu za siri, sikioni na puani jambo lililochangia kuvuja zaidi ya lita 3.5 za damu.

Ofisa kilimo huyo alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Kibara wilayani Bunda mkoani humo baada ya kuibuka ugomvi baina yake na mkewe, Elizabeth Steven (30), huku chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 3, 2024 katika Hospitali ya Kibara ulipohifadhiwa mwili wa marehemu, daktari wa hospitali hiyo, Justine Zacharia amesema baada ya uchunguzi huo imebainika kulikuwa na damu iliyovilia upande wa kulia wa mapafu ya marehemu.

Mke anavyodaiwa kumbana nyeti, kumchoma kisu mmewe hadi kumuua

Dk Zacharia amesema ofisa huyo alifikishwa hospitalini hapo Machi 2, 2024, Saa 3:24 asubuhi akiwa mahututi kutokana na majeraha aliyokuwa nayo na alifariki dunia Saa 6 mchana alipokuwa akiendelea kupatiwa matibabu.

"Tulijitajidi kumpatia huduma ya dharura ikiwa ni pamoja na kufanyiwa upasuaji na kuzuia damu hali ikawa nzuri kiasi tukaanza kufanya utaratibu wa kumpa rufaa ghafla hali ilibadilika na akafariki kabla ya kuanza safari ya kwenda hospitali ya rufaa.”

"Alifika hapa (hospitalini) akiwa amejaa damu mwili mzima yaani nguo zote zilioana na kujaa damu akawa analalamika kuwa na maumivu ya kifuani jitihada zilifanyika kuokoa maisha yake kakini ilipofika Saa 6 alifariki dunia," amesema Dk Zacharia.

Akizungumzia majeraha aliyokuwa nayo Dk George Mathew amesema walibaini alikuwa na majeraha makubwa mawili kifuani ambayo yalisababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

"Alikuwa na jeraha lingine kwenye paja ambalo pia alikuwa amechomwa na kitu chenye ncha kali, lakini pia nyeti zake zilikuwa zimevilia damu na nyingine kuvuja," amesema Dk Mathew.

Kwa mujibu wa daktari huyo, kucha ya kidole cha pili cha mkono wa kulia wa marehemu haikuwepo huku sehemu ya kulia ya pua ikiwa imenyofolewa jambo lililosababisha mifupa ya ndani ya pua kuonekana.

“Hata sehemu ya mdomo wa chini wa marehemu ilinyofolewa na kuondolewa kabisa na inaonekana majeraha hayo yalisababishwa na kung’atwa,” amesema.

Kuhusu mke wa marehemu, Dk Mathew amesema mwanamke huyo pia alifikishwa hospitalini hapo akiwa na jeraha kidevuni.

"Huyu mwanamke naye alikuwa ameloa damu mwili mzima lakini mbali na jeraha hilo dogo hakuwa na shida yoyote hivyo tulikaa naye hapa hospitalini hadi jioni alipochukuliwa na polisi kwaajili ya taratibu zingine," amesema Dk Mathew.

Tukio lilivyotokea

Hata hivyo mtoto wa kike wa marehemu (13) alidai ugomvi baina ya wazazi wake uliibuka baada ya baba yake mzazi kudaiwa kuzaa mtoto na mwanamke mwingine wan je.

"Usiku wa juzi ugomvi ukawa mkubwa baada ya kumaliza kula chakula cha usiku wakati huo mama alikataa kula sisi tukaangalia TV na baba kisha tukaenda kulala lakini baadaye wakaanza kugombana hadi baba akaniamsha akaniambia nimtoe mama alikuwa amemkalia miguuni," anadai mtoto huyo.

Mtoto huyo alidai alipoamka asubuhi aliondoka kwenda shuleni kuhudhuria masomo ya ziada wakati huu wa likizo, ndipo alipofuatwa na mdogo wake (mtoto wa mtuhumiwa) ambaye alimtaka warudi nyumbani haraka, walipofika wakakuta sebule imetapakaa damu.

Anadai baada kupita dakika kadhaa mama yake, alimtaka kufanya eneo lote lililotapakaa damu sebuleni.

Hata hivyo, mtoto huyo anadai alipoanza kufanya usafi huo, alibaini kuwepo kwa vipande vya sehemu za mwili.

“Kulikuwa na vitu kama sehemu za nyama ya pua, mdomo na kidole,” anadai mtoto huyo.

Awali, mtoto wa mtuhumiwa (9) jina linahifadhiwa, alidai kuwa asubuhi ya tukio alikuwa akiangalia runinga, alimuona mama yake akitoka chumbani huku akimtaka mtoto huyo atoke nje huku akiendelea kuzozana na baba yake na kisha mama huyo akafunga mlango kwa ndani.

Hata hivyo, mtoto huyo anadai kuwa kelele za baba yake zilikuwa ni za kuomba msaada. “Tulizunguka na kuanza kufungua mlango, lakini hatukuweza kwa sababu ulikuwa umefungwa kwa ndani tukakimbilia kwa mama China na kumwambia mama anamuua baba na yeye akaja akaanza kusukuma mlango na kuubomoa," anadai mtoto huyo.


Majirani wafunguka

Jirani wa familia hiyo, Jesca Kasora amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa watoto hao walifika eneo la tukio na kumkuta ofisa kilimo huyo akiwa ametapakaa damu mwilini huku mkewe akiwa amemlalia juu akiendelea kumshambulia.

"Watoto walipokuja wakaniambia baba yao anaomba msaada nilikimbia hadi mlangoni kweli nikakuta anaomba msaada nikajaribu kugonga mlango ili wafungue lakini hawakuweza kufanya hivyo badala yake mwanaume aliendela kuomba msaada," amedai Jesica.

Jesca anadai hata walipofika na kujaribu kumuondoa, mwanamke huyo aligoma huku akiwa amembana mumewe sehemu zake za siri, na kisha alitoa kisu alichokuwa amekishikilia mkono mwingine akitaka kuendelea kumshambulia ndipo

“Pale tukatumia nguvu kumdhibiti kisha tukampeleka kituo kidogo cha Polisi Kibara,” alidai jirani huyo.

Cypran Deus akisimulia mkasa huo, alidai ugomvi wa wanandoa hao ulianza baada ya kusambaa kwa taarifa kuwa kazaa na mtoto nje ndoa.

Alidai mwanamke huyo alikuwa akimtuhumu mumewe kwamba alifikia uamuzi huo kutokana na yeye (mtuhumiwa) kutoshika ujauzito kipindi chote cha ndoa yao.

"Huyu mama alikuwa na mtoto mmoja ambaye alimzaa kabla hajaolewa na huyu bwana, na huyu bwana pia alikuwa na watoto wawili ambao aliwazaa na mke wake wa kwanza ambaye inasemakana alifariki kabla hajumuoa huyu na tangu wameishi ni muda mrefu ila hawakuwahi kupata mtoto," amedai Deus.


Mama afunguka

Kwa upande wake, mama wa marehemu, Agnes Julius alikiri kuwa na taarifa ya uwepo wa mgogoro wa wanandoa hao huku akisema kulikuwa na taarifa za ugomvi wa mara kwa mara baina ya wanandoa ambao hata hivyo ulikuwa haudumu.

"Mimi naishi Mwanza kwa hiyo sijui kwa undani zaidi ila nilikuwa nikipata taarifa za mara kwa mara za ugomvi ambao hata hivyo ulikuwa haudumu kwa muda mrefu na hawa watoto wameishi kwa miaka mingi kabla ya kuamua kufunga ndoa Julai 2023," amesema mama huyo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mara, Salim Morcase amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na jeshi hilo linamshikilia mwanamke huyo (Elizabeth Steven) kwa uchunguzi akidaiwa kuhusika katika mauaji hayo.

Wakati Kamanda Morcase akithibitisha polisi kumshikilia mwanamke huyo, Mwananchi ilipewa taarifa kuwa mwili wa ofisa kilimo huyo umesafirishwa leo kuelekea nyumbani kwao eneo la Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa ajili ya maziko.