Mke adaiwa kumuua mumewe kwa kumchoma kisu

Ofisa Kilimo Kata ya Neruma wilayani Bunda,  Julius Rubambi aliyeuawa akiwa na mke wake Elizabeth Steven siku ya harusi yao.

Muktasari:

 Ofisa kilimo Kata ya Neruma wilayani Bunda anadaiwa kufariki dunia baada ya kuchomwa kisu na mkewe katika ugomvi

Bunda. Ofisa Kilimo wa Kata ya Neruma wilayani Bunda Mkoa wa Mara, Julius Rubambi (38) amefariki dunia kwa madai ya kuchomwa na kisu na mke kisa wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amesema tukio hilo limetokea leo Jumanne Aprili 2, 2024 eneo la Kibara wilayani Bunda saa nne asubuhi.

Amemtaja mtuhukiwa wa mauaji hayo kuwa ni Elizabeth Steven (30) ambaye tayari anashikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.

"Ni kweli tukio lipo, mke wa marehemu naye amejeruhiwa na tunavyoongea amelazwa Hospitali ya Kibara huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi kwa ajili ya taratibu zingine," amesema Kamanda Morcase.

Amesema taarifa za awali, zinadai kuwa, wanandoa hao walikuwa na ugomvi, mume akimtuhumu mkewe kuwa na uhusiano nje ya ndoa hali iliyosababisha ugomvi.

Kamanda Morcase  amedai kuwa kufuatia ugomvi huo,  Elizabeth alimchoma kisu kifuani mumewe, ndipo mwanamume alipompiga na kusababisha mke  kupoteza fahamu kabla ya wote kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda  Dk Vicent Naano amesema marehemu pamoja na kuchomwa visu amekutwa na majeraha ya kung'atwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kibara.

"Amejeruhiwa sehemu mbalimbali hadi sehemu za siri na taarifa zinasema ugomvi wao ulianza tangu usiku wa kuamkia leo, ila hadi sasa bado sijajua chanzo cha ugomvi ni nini ila amefariki akiwa anaendelea kupatiwa matibabu," Dk Naano

Amesema baada ya kufikishwa hospitalini hapo hali ya ofisa kilimo huyo ilionekana kuwa mbaya, hivyo uongozi wa hospitali ukiwa unafanya maandalizi ya rufaa kwa ajili ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa  matibabu ofisa kilimo huyo alifariki dunia.

Dk Naano amesema mbali na kuwa ofisa kilimo, marehemu pia alikuwa mchungaji wa kanisa moja la kilokole huko Bunda.