Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fahamu aina za watu na migogoro kwenye uhusiano

Muktasari:

  • Kinachotofautisha uhusiano unaodumu na unaovunjika si kutokuwepo kwa migogoro, bali namna ambavyo wahusika wanavyoikabili na kuitatua.



Dar es Salaam. Migogoro ni sehemu ya kawaida ya uhusiano wa kimapenzi. Hakuna uhusiano usio na tofauti za kimtazamo, hisia au matarajio.

Kinachotofautisha uhusiano unaodumu na unaovunjika si kutokuwepo kwa migogoro, bali namna ambavyo wahusika wanavyoikabili na kuitatua.

Kila wanandoa au wapenzi huwa na mtindo wao wa kushughulikia migogoro. Wengine hupaza sauti, wengine hunyamaza, wengine hutafuta suluhu kwa mazungumzo, huku wengine wakijitoa ili kulinda amani.

Mara nyingi mitindo hiyo haifundishwi shuleni wala nyumbani; hujengeka kutokana na malezi, uzoefu wa maisha na tabia binafsi.

Wataalamu wa sayansi ya jamii wameainisha mitindo hiyo katika makundi matano makuu.


Washindani

Hawa ni watu wanaoamini kuwa katika mgogoro lazima kuwe na mshindi na mshindwa. Wanapokosana na wenza wao, mara nyingi hupandisha sauti, hulazimisha maoni yao na hutaka upande wao ushinde kwa gharama yoyote.

Kwao, mahitaji yao ndiyo hupewa kipaumbele kuliko ya mwenza. Kauli kama, "Toka nyumbani kwangu," "Nimekufanyia kila kitu," au "Tutakutana mahakamani haki ijulikane" hujitokeza mara kwa mara.

Mtindo huu unaweza kuongeza majeraha ya kihisia na kuifanya migogoro kuwa mikubwa kuliko ilivyokuwa awali.


Waepukaji

Kundi hili huchagua kukwepa migogoro badala ya kuikabili. Wanapoulizwa kuhusu tatizo, hujibu, "Sitaki kulizungumzia," "Yamekwisha hayo," au "Usinikumbushe tena."

Kimya chao kinaweza kuonekana kama njia ya kuzuia ugomvi, lakini mara nyingi humwacha mwenza akiwa hajui tatizo ni nini au namna ya kulitatua. Hali hiyo inaweza kupunguza ukaribu wa kihisia na kujenga ukuta wa mawasiliano ndani ya uhusiano.


Walazimisha mwafaka

Hawa huamini kuwa kila mmoja lazima akubali kupunguza baadhi ya matakwa yake ili kufikia mwafaka. Kauli zao hujengwa katika misingi ya kubadilishana, kama vile, "Nitafanya hivi kama na wewe utafanya vile."

Ingawa kila upande hujikuta umetoa sadaka fulani, mtindo huu mara nyingi husaidia kupunguza mvutano na kuwezesha maisha kuendelea.

Mfano ni wanandoa wanaoweza kugawana majukumu ya kumlea mtoto baada ya kazi. Baba anaweza kuchukua jukumu la kumhudumia mtoto hadi muda wa kulala, huku mama akisimamia huduma za usiku. Hakuna anayepata kila anachotaka, lakini wote hupata suluhisho linalowafaa kwa kiasi.


Washiriki

Hili ndilo kundi ambalo wataalamu wengi huliona kuwa lenye afya zaidi katika uhusiano. Washiriki huamini kuwa mgogoro ni fursa ya kutafuta suluhisho linalomnufaisha kila mmoja.

Badala ya kushindana au kukimbia tatizo, hukaa pamoja, husikilizana na kutafuta njia itakayokidhi mahitaji ya pande zote mbili. Kwao, ushindi si kumshinda mwenza, bali kuhakikisha hakuna anayehisi amepoteza.


Wasaka amani

Hawa huweka amani mbele ya kila kitu. Wapo tayari kuachia baadhi ya matakwa yao ili kulinda uhusiano.

Kauli kama, "Chukua unachotaka alimradi tuishi kwa amani," au "Mimi niko tayari kukupisha ili mambo yaende vizuri," ni za kawaida kwao.

Ingawa mtindo huu unaweza kupunguza migogoro ya haraka, wataalamu wanaonya kuwa kujinyima kila mara bila kueleza hisia zako kunaweza kujenga maumivu ya ndani ambayo baadaye huibuka kwa nguvu zaidi.


Ni mtindo gani unaofaa?

Hakuna mtu anayebaki katika kundi moja maisha yote. Kutegemeana na mazingira, watu wanaweza kubadilika kutoka mtindo mmoja kwenda mwingine. Hata hivyo, tafiti nyingi zinaonyesha kuwa uhusiano unaodumu kwa muda mrefu huwa na mchanganyiko wa ushirikiano, utayari wa kufikia mwafaka na moyo wa kusamehe.

Washiriki, walazimisha mwafaka na wasaka amani kwa kiwango kinachofaa hujenga mazingira bora ya kuaminiana na kuheshimiana kuliko washindani na waepukaji.

Mwisho wa yote, ukomavu katika uhusiano hauonekani kwa kutokuwepo kwa migogoro, bali kwa uwezo wa kuitatua kwa busara. Si kila jambo linapaswa kuwa vita ya kushinda au kushindwa. Chagua kupigania yale yenye msingi na ujifunze kuachilia mambo madogo yasiyoongeza thamani katika uhusiano.

Hekima, mawasiliano mazuri na kuheshimiana ndiyo silaha bora za kulinda upendo. Nishati tunayowekeza katika kugombana, inaweza kutumika kujenga ukaribu, kuimarisha uaminifu na kuifanya safari ya maisha ya pamoja kuwa yenye furaha na mafanikio.