Hakikisha unapendeza hivi siku ya Valentine

Picha na mtandao

Kiuhalisia watu hupendana kila siku japo kuna mikwaruzano ya hapa na pale na hauwezi kusema siku ya wapendao ndio ninayompenda mpenzi wangu ila Februari 14 hupewa upekee kwa watu kusherehekea upendo na uhusiano wao.

Wapo ambao huitumia siku hii kwa mitoko mbalimbali ikiwemo sehemu za chakula, kuogelea au kubarizi ufukweni lengo likiwa ni kusherehekea na kufurahi pamoja na wenzi wao.

Unapozungumzia mtoko suala la mavazi lazima lizingatiwe ili kupata mwonekano unaoweza kukamilisha furaha ya siku hii, katika makala yetu ya mitindo wiki hii tumeangalia kwa kina kuhusu hilo.

Picha na mtandao

Mwanamitindo Chris Momo anasema ni kawaida watu wengi kuhisi mavazi rasmi katika siku ya wapendanao ni yale yenye rangi nyekundu wakiamini inaashiria upendo.

Anasema rangi nyekundu ni alama ya upendo baina ya mtu na mtu au mtu na jamii hivyo watu kuvaa mavazi yenye rangi hio ni sahihi.

“Mavazi ya rangi hio huweza kuwa sehemu ya nguo na isiwe nguo nzima kuwa na rangi nyekundu. Namna gani unavyoweza kuvaa na kupata mwonekano wa kipekee katika mtoko wako siku hii ya wapendanao hivyo ni muhimu watu kuvaa katika mwonekano wa sherehe.

“Kwa mwanamke unaweza kuvaa gauni lako la usiku lililo la rangi nyekundu au maua yaliyo na mchanganyiko wa rangi nyekundu chini ukapigilia na viatu vyenye kisigino kifupi au virefu kama umezoea kutembelea. Usisahau hereni, cheni, bangili, mkoba na lipstiki mdomoni itakayokupatia mng’ao na kufanya kuwa na mvuto zaidi,” anasema Momo na kuongeza.

‘Unaweza pia kuvaa mavazi yako ya kila siku kama gauni au blauzi ya nyeusi yenye mtindo wa ‘Off shoulder’ shingoni ukavaa skafu au cheni yenye rangi nyekundu. Pia hayohayo mavazi yako unaweza kuyavaa katika mpangilio tofauti na ulivyozoeleka ukanakshia na kiatu, cheni, hereni, bangili au mkoba wenye rangi nyekundu kuzivaa njia hii itakupa mwonekano wa kipekee na kupendeza,”.

Kwa upande wa wanaume wanaweza ukavaa suti, jeans na tisheti kulingana na matakwa yako lakini zingatia viatu utakavyovaa kwa chini viendane na nguo ulizovaa kuepusha kutovutia ukiwa katika matembezi.

Mbunifu wa mavazi Tydo Master anasema imezoeleka watu kuvaa nguo zenye rangi nyekundu siku ya valentine lakini anashuri kuwa upo uwezekano wa kuchanganya rangi nyekundu na nyeusi au hata kijani na ukapata mwonekano mzuri.

“Watu wengi wamekariri kuvaa nguo zenye rangi nyekundu siku ya Valentine lakini unaweza ukachanganya rangi hio na nyeusi au dark green na kupata mwonekano wa kipekee kwa mfano unaweza ukavaa gauni, sketi topu ya dark green kwa mwanamke na koti au suruali ya rangi nyeusi kwa mwanaume ukachanganya na viatu, tai, au mapambo ya kike yenye rangi nyekundu ukapata mwonekano mzuri na wa kuvutia” anasema Tydo

Tydo anaongeza kwa baadhi ya watu ambao hawana sehemu za kwenda kutembea na wanatamani kutoka kivalentine wanaweza kuvaa simple lakini wakabamba mavazi kama jeans na topu yenye rangi nyekundu au nyeusi chini akapigilia na sendo au kaptula na tisheti kwa wanaume.

Andrew Budah yeye anashauri watu wasikurupukie siku hiyo wajitahidi kufanya vitu vilivyo ndani ya uwezo wao hasa katika suala zima la mavazi na sehemu za kwenda kutembea na wenza wao.

Hii ni kutokana na baadhi ya watu hutumia gharama kutafuta nguo ili wapate mwonekano wa kipekee ambapo baada ya siku hio kupita huanza kujutia na kubaki hawana kitu.