Hawa hapa mahausigeli wenye digrii, waeleza walivyozipata

Tumekuwa tukisikia namna baadhi ya Watanzania wanaokwenda nchi zilizoendelea wanavyosoma huku wanafanya kazi za majumbani kwa watu katika muda wao wa ziada na hii sio kwa wanaosoma vyuo vya kati tu, bali hata chuo kikuu na wale wanaochukua masomo yao ngazi ya uzamifu na baadaye kuwa madaktari katika taaluma fulani.

Hii huwasaidia kujikimu kimaisha wanapokuwa huko na kwa mujibu wa waliowahi kufanya kazi hizo, hulipwa hela nzuri tu na wakati mwingine kushinda walio maofisini hapa kwetu.

Debora Mwageni na Farida Daniel ambao ni wafanyakazi wa majumbani, wamedhihirisha kuwa iwapo utasimamia ndoto zako kikamilifu, unaweza kuzitimiza licha ya changamoto mbalimbali utakazokumbana nazo.

Wasichana hawa wanasema wamefanikiwa kujiendeleza kielimu wakiwa wanafanya kazi hizo hadi kufika kiwango cha elimu ya chuo kikuu.

Wakati Debora amemaliza mwaka jana shahada ya masuala ya sayansi ya jamii katika Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, Farida amemaliza elimu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini, kampasi ya Dar es Salaam.


Debora Mwageni

Safari ya Debora kuwa mfanyakazi wa ndani ilianza mwaka 2013, baada ya kutoka nyumbani kwao Mbalizi mkoani Mbeya na kufanya kazi hiyo wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Debora (26), anasema akiwa kidato cha kwanza mwaka 2011 katika Shule ya Mshikamano, baada ya kufaulu wazazi wake walitofautiana hadi kufikia hatua ya kutengana, licha ya kuwa huko nyuma ilikuwa ni familia iliyoishi kwa raha na kupata mahitaji yote.

Wakati huo anasema alikuwa ana miaka 13 na kujikuta akishuhudia ugomvi wa wazazi wake ambao ulifikia hatua ya kutengana.

“Katika kutengana kwao huko, kila mmoja akawa anagombania kukaa na mimi, lakini mwisho wa siku baba alishinda.

“Hata hivyo, kwa bahati mbaya nikiwa nakaa na baba hakuonekana mtu wa kunijali, kwani alikuwa akitoka asubuhi na kurudi usiku tukiwa tumelala, hajui naendaje shule wala hanunui vifaa vyovyote vya shule,” anasema na kuongeza;

“Jambo hili lilinifanya kutokuwa na utulivu wa kusoma, na hata nilipokuwa nikitoka nyumbani nikawa siendi shule, naenda mtaani kuzurura na kwa kuwa baba hakuwa mfuatiliaji wala hakulijua hilo.”


Kufanya kazi za ndani

Debora anasema mwaka 2013, alikwenda kwa rafiki wa mama yake nyumbani kwao na kumweleza anatafuta mfanyakazi wa ndani wa kwenda Bagamoyo na kumuomba amsaidie kutafuta.

Ilipopita wiki moja yule mama alirudi kumuuliza kama amempata, ndipo alipomjibu ameamua atakwenda yeye na hii ni kutokana na kuishi maisha magumu, aliyoyaona hayana tofauti na kuishi mbali na wazazi wake.

Anasema licha ya yule mama kuwaogopa wazazi wake kuwa huenda wakagombana naye kwa kitendo hicho au kuja kumpeleka Polisi, Debora alimwambia wafanye siri na wakati huo ilikuwa kipindi cha likizo ya Desemba.

“Nilimwambia kwa maisha ya wazazi wangu wanayoishi niliona sitaweza kuendelea kuishi pale wala kuwa na utulivu wa kusoma, hivyo bora nikafanye kazi mbali ambapo hawataniona, nashukuru alinielewa.

“Hivyo nauli ikatumwa nikaenda kukutana naye stendi, akaniandikia namba ya bosi ninayeenda kufanya kazi Bagamoyo kwenye karatasi na nilipofika alikuja kunipokea stendi na kuanza kazi ambapo ndipo naishi hapo hadi leo na paliponiwezesha kusoma hadi kufika chuo kikuu,” anasema mfanyakazi huyo.


Alivyojiendeleza kielimu

Akizungumza jinsi alivyojiendeleza kielimu, Dobora anasema alipofika Bagamoyo alikaa miezi mitatu bila kuwasiliana na baba yake kwa kuhofia atamgombeza kwa alichokifanya.

Anasema hata alipompigia simu kuzungumza naye alimkatia, hivyo kukaa miezi mingine mitatu tena kisha kumtumia ujumbe mrefu kumuomba msamaha na kumueleza kwa nini aliamua kwenda kufanya kazi mkoani.

“Nashukuru ujumbe huo baba aliusoma na kutaka azungumze na bosi wangu, huku akimhoji ingekuwa ni mtoto wake angekubali amfanyie kazi hizo za kufua na kumpikia tu, bila kwenda shule na kumuamuru anirudishe Mbeya nikaendelee na shule, lakini mimi nilikataa,” anasema Debora.

Baada ya kupita miezi saba ikiwa mwaka 2014, alimwambia bosi wake wa kiume kuwa anatamani kurudi shule, naye alimuuliza iwapo anapenda hoteli au kitu gani, lakini akawa na wasiwasi na kozi hiyo kwa kuwa hakuwa amemaliza kidato cha nne.

“Mwisho wa siku aliniamulia niende masomo ya QT ambayo nilitakiwa nisome jioni, ili asubuhi nifanye kazi za nyumbani. Nilisoma kwa miaka minne,” anasema.


Alijigawaje

Safari ya kusoma haikuwa rahisi, kwani alipitia mengi, kwani kabla ya kuanza masomo kulikuwa na mtoto wa miaka mitatu, lakini alipoanza shule akaletwa wa mwaka mmoja na jukumu la kuwalea lilikuwa lake.

Wakati huo pia alikuwa akifanya kazi nyingine za ndani pamoja na kumsaidia bosi wake ambaye ni mwalimu, kusahihisha madaftari ya watoto waliokuwa wakisoma masomo ya ziada hapo kwake.

“Nilikuwa nachoka hadi nakosa muda wa kujisomea nyumbani, hivyo nilichokuwa nafanya wakati nikiwa darasani natumia muda mwingi kumsikiliza mwalimu ili nielewe na nilikuwa msumbufu kwao ilimradi nikitoka pale niwe nimeelewa, kwa kujua sitapata muda mwingine wa kusoma nikirudi nyumbani,” anasema Debora.

Anashukuri mabosi wake walimlipia ada, kumpa hela ya matumizi na nauli na alipofanya mitihani yake ya kidato cha nne alifaulu kwa kupata daraja la tatu.

Hata hivyo, anasema wakati akiendelea na masomo yake, siku moja mwaka 2016 alikwenda kumsaidia bosi wake kuhudumia chakula kwenye semina ya Shirika la Jumuiya ya watu wanaojitolea Ulimwenguni (CVM)Tanzania, ambalo linajishughulisha na utoaji elimu kwa wafanyakazi wa ndani.

Akiwa kwenye semina hiyo alieleza mambo mazito wanayopitia wafanyakazi wa majumbani na shirika hilo walimpenda na hata kuahirisha kutomlipa posho na kumlipa kwa kuwa aliingia kupitia bosi wake huyo, ingawa hakuwa kwenye bajeti ya waliopaswa kupewa elimu siku hiyo.

Anasema tangu wakati huo, shirika hilo likawa linamfuatilia kujua maendeleo yake, kwani kikubwa walichovutiwa ni kuona akisoma huku akifanya kazi. Mwaka 2017 alipomaliza kidato cha nne alikurudi nyumbani kwao Mbeya.

Akiwa anasubiri majibu, anasema bosi wake alimpigia simu kwenda kumsaidia mtoto wake aliyekuwa amejifungua, hivyo kukaa naye miezi mitatu mkoani Iringa na hakuwa analipwa chochote mpaka matokeo yalipotoka akawa amepata daraja la tatu.

Alirudi nyumbani kwa bosi wake Bagamoyo, akawa anamlipa mshahara wa Sh60,000 kwa kufanya kazi mbalimbali, ikiwemo kusahihisha madaftari na kwenda kuhudumia chakula.

Mwaka 2018 matokeo yalipotoka katika awamu ya kwanza hakuwa amepangiwa shule, lakini awamu ya pili alipangiwa kwenda Shule ya Sekondari Kikaro iliyopo Chalinze, mkoani Pwani ambako alikaa bweni.

Bosi wake aliendelea kumsaidia akishirikiana na nyumbani kwao kidogo kupitia mama na dada zake, na moja ya shirika lililokuwa likiwasaidia wasichana, japo fedha nyingi anasema zilikuwa zinatoka kwa mwajiri wake.

Mwaka 2020 alimaliza kidato cha sita, wabosi wake walimpeleka mafunzo ya jeshi ambako alikaa huko miezi mitatu. Alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Mwalimu Nyerere.

Akiwa chuoni, mabosi wake waliendelea kumuunga mkono kwa kumlipia ada na kuhakikisha anapata mahali pa kukaa, akawa anafanya kazi na CVM na wakati mwingine Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Hifadhi, Mahotelini, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu) na Novemba mwaka jana CVM walimuajiri kabisa.

Japokuwa mpaka sasa bado anaishi kwa bosi wake, anafanya shughuli zote kama mtoto wa nyumbani, siku za karibuni ana mpango wa kwenda kuanzisha maisha yake.

Anasema kozi ya sayansi ya jamii aliyoisomea anaamini itasaidia jamii kwa ukaribu, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, kwani sasa amefungua asasi inayoitwa Initiative for Domestic Workers, harakati zake alizianza kama kikundi cha wafanyakazi wa majumbani na hii ni baada ya kutoka kwenye semina ya CVM ambako alikuwa mwenyekiti wake.

Ingawa wengine waliishia njiani, yeye aliendelea na mwaka 2021 ilisajiliwa rasmi na kuanza kufanya kazi, hivyo Debora pia ni Mkurugenzi wa taasisi hiyo.

Anasema malengo yake ni kuhakikisha kazi ya wafanyakazi wa majumbani inaheshimiwa, huku akitoa wito kuridhiwa kwa mkataba namba 189 unaohusu kazi zenye staha kwa wafanyakazi hao, kwani pamoja na mambo mengine unasisitiza uwepo wa mikataba, kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa wafanyakazi hao kama zilivyo kazi nyingine.


Farida Daniel

Farida (26), anasema alianza kufanya kazi za ndani baada ya kumaliza kidato cha nne wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Kipindi hicho anasema alikuwa tu nyumbani, pia wazazi wake walikuwa ametengana na kwa bahati nzuri akiwa katika maisha hayo alikutana na Debora.

“Debora alinikuta katika wimbi la mawazo kutokana na kutengana kwa wazazi wangu, alinipa moyo na ndiye aliyenishauri nikafanye kazi kuliko kukaa tu mpaka matokeo yatakapotoka, ili nipate hela ya kujikidhi,” anasema.

Anasema alifanikiwa kupata kazi kwa mama moja aliyekuwa akimlipa ujira wa Sh100,000 kwa mwezi, wakati huo baba hakujua, kwani alimshirikisha mama pekee.

Anasema baadaye alikwenda kusoma kidato cha tano katika shule ya Jitegemee, Dar es Salaam na akawa anaishi kwa kaka yake waliyechangia baba.

“Kipindi chote hiki nilikuwa napitia changamoto za kufanya kazi zote nyumbani, lakini nilichukua kawaida kwa kuwa tayari nilishawahi kufanya kazi kwa mtu.

“Nilipomaliza shule, nikarudi tena kwa bosi wangu nikaendelea kufanya kazi. Nilikusanya hela kwa ajili ya chuo na mpaka majibu yanatoka nikapata Chuo cha Tumaini, kusoma sheria. Nilikuwa nimeshakusanya Sh1 milioni, huku kaka yangu akinilipia hela ya ada, lakini nauli, bweni na matumizi mengine nikawa najitegemea. Nyingine mama na baba walikuwa wakinisaidia kidogo,” anasema.

Anasema kipindi cha likizo alikuwa akiendelea kufanya kazi kwa mama yule na fedha alizopata zilimsaidia kwa matumizi chuoni kwa kuwa hakuwa amepata mkopo wa Serikali.

Julai mwaka huu amemaliza chuo, ameamua kufanya kazi katika asasi yao Initiative For Domestic Workers ili kusaidiana na Debora kuwafikia wafanyakazi wengi wa majumbani ambao huwapa elimu ya kujitambua kwa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Serikali ya mitaa na waajiri.

Lengo lao, Debora anasema ni kuja kumfanya mfanyakazi wa majumbani kujiona mwenye thamani na anaweza kufanya vitu vingine, ikiwemo kujiendeleza kielimu kama walivyofanya wao.


Imeandaliwa na kushirikiana na Bill & Melinda Gates.