Prime
Mwandiko wamrudisha hausigeli darasani
Licha ya kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2020, hakufanikiwa kuendelea na masomo.
Aliyekuwa akiishi naye, hakuona haja ya kumwendeleza kimasomo, ili aje kuifikia ndoto yake maishani. Ni ndoto ya kuwa muuguzi.
Hakuwa na namna zaidi ya kukubali kuanza maisha mapya ya kuwa mtumishi wa kazi za nyumbani. Hakujua kumbe majaliwa yake yako huko.
Akaanza kazi nyumba ya kwanza jijini Dar es Salaam alikoletwa kwa lengo la kuendelezwa kimasomo, lakini akageuzwa dada wa kazi.
Akabadili nyumba, huko ndiko alikokutana na mwajiri mpya ambaye ni mwalimu, aliyeshangazwa na aina ya mwandiko wake.
Ni mwandiko uliomvutia mwajiri wake kila alipokuwa akiandika mahitaji ya nyumbani; huu ukawa mwanzo mpya wa maisha ya binti Safina Ramadhani (20) kutoka kazi za ndani hadi kuwa mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Mbezi Inn ya jijini Dar es Salaam.
Simulizi yake
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Safina anasema akiwa kijijini mkoani Singida mwaka 2020 baada ya kumaliza darasa la saba, baba yake mkubwa hakuweza kumuendeleza kielimu.
Anasema alikuwa akiishi na baba yake baada ya wazazi wake kutengana, huku mama yake akiolewa na mwanamume mwingine jijini Dar es Salaam.
“Mama yangu aliondoka nikiwa sijaanza shule ya msingi na alichokuwa akifanya ni kunitumia tu sare za shule na madaftari,” anasema Safina.
Safina anasema siku moja akiwa nyumbani kwao Singida alifika mama mmoja na kumwambia anamchukua kwenda naye Dar es Salaam ili akamsomeshe.
“Hata hivyo, nilipofika hali haikuwa hivyo, alinifanyisha kazi ya kumuuzia vitu mbalimbali katika shule aliyokuwa anafundisha, ikiwamo ice cream, kufanya kazi za ndani na mambo mengine,” anasema mwanafunzi huyo.
Safina anasema alikaa na mama huyo kwa miezi sita na kuamua kumuuliza mbona alichomwambia kuhusu kumsaidia kumsomesha ni tofauti na anachokifanya.
“Majibu yake yalikuwa, mimi nimekuleta hapa sio kwa ajili ya kukupeleka shule, bali kwa ajili ya kufanya kazi,” anasimulia Safina.
Pia, anasema baada ya majibu hayo, alikaa kwa miezi miwili kisha akamtoroka bosi wake na kwenda kumtafuta mama yake baada ya kuomba namba yake, kwa kuwa aliishaambiwa anaishi Dar es Salaam.
Hata hivyo, Safina anasema maisha kwa mama yake ambaye ni mgonjwa hayakuwa mazuri, kwa kuwa hakuwa na kipato cha kuweza kumhudumia, akaona kukaa kwake itakuwa mzigo.
“Ndipo hapo nilipoamua kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine na ndio hapo ninapoishi kwa huyu mama hadi sasa,” anasema Safina.
“Tayari nimekaa naye mwaka mmoja na baada ya kunielewa, alinihoji nimeishia darasa la ngapi na nilipomjibu la saba, akaniuliza endapo kuna mtu atajitokeza kukusomesha je, nitakuwa tayari kurudi shule, nikamjibu ndiyo.
“Akanitafutia shule na leo nipo hapa Shule ya Sekondari Mbezi Inn nikiendelea kusoma,” anasema Safina.
Anamzungumziaje bosi wake
Safina anasema kitendo mama huyo alichomfanyia, hana cha kumlipa kwa kuwa ni mabosi wachache wenye mioyo hiyo, huku akiahidi kuwa hatamuangusha.
Safina anasema mama huyo mbali ya kuendelea kumlipa mshahara, pia humpa nauli ya kwenda shule na hela ya kula.
Kuhusu ndoto zake, anasema anapenda kuwa nesi na hata mwili wake mdogo anaona anatosha kufanya kazi hiyo.
Anajigawaje na kazi za nyumbani
Licha ya kusoma, Safina bado anatambuliwa na bosi wake kuwa ni mfanyakazi wake, hivyo kabla ya kwenda shule saa sita, huwa anaamka saa 12 asubuhi na kuhakikisha amefanya kazi zote anazostahili kuzifanya na inapofika saa tano anaanza safari ya kuelekea shule.
Vilevile anaporejea nyumbani majira ya saa 12 jioni, huendelea na shughuli nyingine na akimaliza huwa na muda wa kupitia kile alichofundishwa shuleni kabla ya kwenda kulala.
“Nashukuru watoto wa bosi wote ni wakubwa na wako shule, hivyo nyumbani tupo mimi na yeye na ninapomaliza kazi zangu huwa napata muda wa kujisomea,” anasema Safina.
Alichosema bosi wake
Bosi wa Safina, aliyejitambulisha kwa jina la Anita Kagirwa anasema alikutana na binti huyo baada ya kumtumia dalali ambaye hupeleka wasichana wa kazi kwa watu.
“Huyu dalali hajaanza kuniletea Safina tu, alishawahi kuniletea na wengine na anajua namna gani ambavyo huwa naishi nao vizuri,” anasema Anita.
“Hivyo nilipotaka msichana safari hii, ndipo aliniambia kuna msichana yupo hapa Dar es Salaam na tukazungumza naye pamoja na hela yake ya udalali akaniletea.
“Baada ya Safina kufika, nikamuona ni binti mdogo sana na kujiuliza hivi kweli ataweza kufanya kazi, lakini kwa bahati nzuri kadiri siku zilivyozidi kwenda nikaona anaweza,” anasema Anita.
“Kitu kilichonifanya nione Safina anahitaji kuendelezwa kielimu, ni pale nilipokuwa nikimwagiza vitu vya kwenda dukani na sokoni akawa anaandika kwenye karatasi huku mwandiko wake ukiwa mzuri, ambao sijawahi kuuona kwa mfanyakazi yeyote wa kazi za ndani niliyewahi kuishi naye.
“Pia, kwa kuwa mimi kazi yangu ni mwalimu, moja ya kumjua mtoto ana akili ni mwandiko wake na hapo ndipo nilipomuuliza kama aliwahi kusoma na kunipa simulizi yake kuwa aliishia darasa la saba na kufaulu, lakini hakuweza kuendelea kutokana na changamoto za maisha ya kifamilia,” anasema bosi wa Safina.
Anasema kwa namna anavyomuelezea mama yake, inaonekana naye anafanya kazi nyumbani kwa mtu.
Alivyomtafutia shule
Anita anasema wakati Safina alipokuwa tayari kwenda shule, ilikuwa ni Machi mwaka jana na aliuliza namna ya kupata shule kwenye moja ya makundi aliyopo kwenye mtandao wa kijamii na kumwelekeza wapi pa kumpeleka.
Mmoja wa wanakikundi alimwambia kuna programu ya Mama Samia ya kuwasomesha watoto wa kike bure na kumpatia mawasiliano ya mtu mmoja wa kuweza kumpa mwongozo.
Hata hivyo, katika kuulizia kwa huyo aliyeelekezwa, aliambiwa amechelewa mpaka Oktoba, 2022 na wakamkumbusha siku ilipofika.
Anasema wasiwasi wa Safina ilikuwa hataweza kujilipia vifaa, lakini alimuahidi vyote atagharamia yeye na mwisho wa siku akaanza shule.
“Pamoja na kuanza shule nilimwambia nitaendelea kumlipa mshahara wake, kwa kuwa pia ana ndugu yake anayesoma huwa akimtumia hela kwa ajili ya matumizi, hivyo ni mtoto ambaye naye ana majukumu,” anasema Anita.
Safina ni binti wa aina gani?
Bosi huyo anasema Safina ni binti ambaye huwezi kushindwa kukaa naye, anaweza kuishi na kila mtu, japo ana mambo madogo madogo ya utoto.
Jingine ni binti ambaye akikosea huwa anaumia sana mpaka unaona, jambo linalomfanya aogope wakati mwingine kumgombeza anapokosea.
“Nashukuru Safina ni binti muelewa sana, huwa anafanya kazi zake bila kutumwa, hufanya kazi zake zote kabla hajaenda shule na akirudi anafanya kazi atakazozikuta na akishamaliza anakaa mezani kuandika notes zake, lakini pia huamka usiku kujisomea,” anasema Anita.
“Pia, kwa zile notes nyingine zinazohitaji kudurufiwa huwa namsaidia kufanya hivyo kila anaponiambia na moja ya mambo ninayomkazania ni kupambana kusoma kwa kuwa najua QT ni ngumu sana.”
Hata hivyo, anasema yupo tayari kumsaidia mpaka hapo atakapotimiza ndoto zake, pia kuna mpango wa kuwekwa shule ya bweni watakapofika kufanya mitihani ya kidato cha nne.
“Nitakuwa tayari kuvumilia mwaka mmoja huyu binti akasome ili kutimiza ndoto zake, labda awe anarudi tu (nyumbani kwa bosi wake) mwisho wa juma, na nitajitahidi kuendelea kumpa mshahara wake na kumgharimia mahitaji yote ya shule hata akiwa bweni,” anasema bosi wa Safina.
Pia, kifamilia anasema Safina aliwahi kusema ana mdogo wake wa kike anayefanya kazi za ndani pia, lakini wa kiume ndio huyo anasoma na kumtumia hela.
Manispaa, mwalimu wamzungumzia Safina
Ofisa Elimu ya Watu Wazima kutoka Idara ya Elimu Sekondari Manispaa ya Ubungo, Christa Ndunguru anasema Safina ni mmoja wa wanafunzi wanaofanya vizuri shuleni hapo, jambo linaloonyesha kuwa atafanya vizuri katika mtihani wake.
"Safina na wenzake mwaka huu wanatarajia kufanya mtihani wa Taifa kidato cha pili na kwa namna anavyojitahidi kujisomea tunamuona atafanya vizuri," anasema Ndunguru.
Hata hivyo, anatoa wito kwa jamii kuwasaidia watoto wa namna hiyo ili watimize ndoto zao na isionekane kwa waliyoyapitia ni wakosaji, huku akimpongeza bosi wa Safina kwa kumpa ruhusa hiyo ya kwenda shule.
"Hapa tuna wanafunzi ambao ni mama wa watoto, lakini wengine pamoja na kuwa hivyo hawana vipato na wakati mwingine kushindwa kupata hata nauli ya kuja shule,” anasema Ndunguru.
"Lakini wapo wanaofanya kazi za house girl kwa watu na za kuuza maduka, hivyo mabosi, wazazi na walezi wawape nafasi ya kujisomea, "anasema ofisa huyo.
Pia, anashauri wazazi kuwa karibu na watoto wao, ikiwamo masuala ya afya ya uzazi, kwa kuwa kuwaacha wenyewe watakwenda kujifunza kwa watu wengine na kufundishwa mambo yasiyo sahihi, hivyo kupata ujauzito.
Kuhusu manispaa, anasema kila shule ina walimu wa walezi ambao wamekuwa wakikaa nao kuzungumza masuala mbalimbali ili kuyaepuka katika umri wao wa kupevuka, kubwa kujitambua wao ni nani.
Mwalimu wa Safina, Hidaya Mohammed anasema Safina amekuwa mwanafunzi msikivu darasani na anayependa kuuliza mahali asipoelewa.
Hidaya ambaye pia ni mratibu wa wanafunzi waliorejea shule ya Mbezi Inn, anasema hata kwenye masomo ya sayansi anayosoma Safina anaona dalili za kutimiza ndoto yake ya kuja kuwa nesi, huku akiahidi shule itafanya liwezalo kusaidia katika hilo.
Safina ni miongoni mwa wanafunzi wa programu ya kuwarudisha shule wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.
Kwa mujibu wa Ndunguru, Manispaa ya Ubungo ina jumla ya wanafunzi 60 wanaosoma kwenye programu ya mama Samia.
Uamuzi wa kurejeshwa shule kwa wanafunzi hao, ulitangazwa na Serikali Novemba 24, 2021, na tangu programu hiyo ianze hadi kufika Januari mwaka huu, wanafunzi 1,907 walikuwa wamerejea shuleni.