Jinsi wazazi wanavyoua, kukuza vipaji vya watoto

“Katika kipindi hiki cha changamoto ya ajira, pengine wazazi wangu wangeruhusu kipaji changu cha uchezaji mpira kuendelezwa kingenisaidia kuajirika.”

Hiyo ni kauli ya Sadiki Saidi, ambaye ni mhitimu wa shahada ya awali ya sanaa katika Uchumi mwaka 2019 na hadi sasa hajaingia kwenye ajira.

Anasimulia kuwa alipokuwa mdogo katika eneo alilokuwa akiishi na wazazi wake huko Kinondoni jijini Dar es Salaam alipewa jina la “Mkono wa Sumaku” kutokana na uhodari wake wa kudaka mipira wavuni kama golikipa alipokuwa akicheza mpira na watoto wenzake.

“Niliendelea kuwa maarufu hadi kufikia timu za maeneo ya jirani kama vile Mwananyamala na Magomeni, walikuwa wakinikodi kuwa golikipa katika timu zao na kunilipa fedha.”

Hata hivyo, anaeleza kuwa jambo hilo halikuwapendeza wazazi wake, hivyo walimtaka asitishe mara moja kucheza mpira na kujikita katika masomo pekee.

“Waliniadhibu sana hadi wakahakikisha naachana kabisa na masuala ya mpira na kujikita zaidi katika masomo, nilipoona adhabu zimekuwa nyingi ikanilazimu kufanya kile walichokitaka na nashukuru nimehitimu masomo yangu ya elimu ya juu lakini hadi sasa sijapata ajira.

“Pengine wazazi wangu wangenisaidia kukuza kipaji changu huku nikiendelea kuweka bidii katika masomo yangu ningekuwa golikipa msomi na pengine kupitia kipaji changu ningepata ajira,” anasimulia kijana huyo.

Alichokipitia Sadiki, pia wanapitia baadhi ya vijana wenye vipaji na kusababisha hata vipaji vyao kufa, ambavyo pengine vingeendelezwa vingewasaidia kuajiriwa na hata kujiajiri wenyewe, hivyo kujikwamua kimaisha.

Kipaji ni uwezo wa kuzaliwa nao wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu bila kufundishwa au baada ya kufundishwa kidogo tu na si kila mtu anaweza kufanya jambo hilo. Kinaweza kuwa cha kimwili au cha kiakili lakini pia kinaweza kuendelezwa au kudumazwa.

Inaelezwa kuwa pamoja na mambo mbalimbali yanayosaidia kukuza vipaji vya watoto, ikiwemo mfumo wa elimu, wazazi wana nafasi kubwa katika kukiendeleza au kukidumaza kipaji cha mtoto wake kwa kuwa mara nyingi yeye ndiyo huwa wa kwanza kutambua uwezo ama kipaji cha mtoto wake.


Nafasi ya wazazi kwenye hili

Petro Peter ambaye ni baba wa watoto wawili, anasema ni kweli baadhi ya wazazi wamekuwa nyuma katika kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto wao kwa kuwa wamekuwa na dhana ya kuwa ufaulu wa masomo ya darasani ndiyo unaoamua mafanikio ya mtoto hapo baadaye.

“Baadhi ya wazazi bado wamekuwa wakiamini kuwa ufaulu pekee ndio utakaofanya mtoto aje kuwa na maisha mazuri hapo baadaye, hivyo msisitizo mkubwa wamekuwa wakiuweka huko na kuweka kando juhudi za kukuza na kuendeleza vipaji vyao kwa kuona wakifanya hivyo kutawafanya watoto wao kushindwa kuzingatia zaidi masomo yao,” anasema.

Anaeleza kuwa inawezekana kwa mtoto kuendelea na masomo yake huku akitumia muda wake wa ziada kufanya shughuli zitakazomwezesha kukuza kipaji chake.

“Mfano, kama ana kipaji cha kuimba, kucheza, kuchora na vingine katika muda wake wa ziada, mzazi anaweza kumtafutia mkufunzi kulingana na kipaji husika ambaye atamsaidia kumuongoza, kwa namna gani anaweza kutumia kipaji alichonacho kuwa fursa.

Kwa upande wake, Mwanaisha Salum ambaye ni mama wa mtoto mmoja, anaeleza kuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwazuia watoto wao kufanya shughuli mbalimbali zitakazowawezesha kukuza vipaji vyao, mfano kuimba au kucheza mziki kwa kuona ni upotevu wa maadili.

“Japokuwa hili kwangu naona kama ni upotofu, vipaji kwa sasa vimetumika na kuwa sehemu ya ajira kwa vijana na hata kuzalisha ajira kwa vijana wenzao,” anaongeza.

Akizungumza na Mwananchi, Mratibu wa Miradi Kitaifa kutoka Shirika la Great Hope ambalo moja ya majukumu yake ni kuinua na kuendeleza vipaji vya watoto, Noelle Mahuvi anasema familia, haswa wazazi wana mchango mkubwa katika kuhakikisha ndoto za mtoto kupitia kipaji chake zinatimizwa.

Anasema moja ya sababu inayopelekea vipaji vya baadhi ya watoto kushindwa kuviendeleza ni pamoja na wazazi wenyewe kushindwa kubaini vipaji vya watoto wao mapema.

“Kwa hiyo ni jambo muhimu katika familia au jamii kuwa na utaratibu wa kuvibaini na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu,” anasema.

Hata hivyo, anaongeza kuwa kuna baadhi ya familia hata baada ya kubaini vipaji vya watoto wao huwa hawafanyi jitihada yoyote kuviendeleza.

Anasema kama mtoto ana kipaji cha kufanya jambo fulani mfano kuimba, kucheza, kuchora na vinginevyo na familia haitoi ‘sapoti’ ya hali na mali katika kukiendeleza, kwanza humvunja moyo na pengine kumpelekea kutokuona umuhimu na thamani ya kipaji alichobarikiwa.

“Mara nyingi tunapofanya mambo yenye manufaa tunatarajia familia zetu kuwa bega kwa bega na sisi, hii huwa inaamsha moyo na ari ya kufanya jitihada zaidi na hatimaye kulifikia lengo.

“Mfano mimi nimekuwa nikiendesha shirika hili kwa muda wa takribani miaka 10, haikuwa rahisi, kwani kuna milima na mabonde, lakini kutokana na umoja na ushirikiano ninaopatiwa na familia yangu umenifanya kufikia hapa,” anaeleza.

Anasema baadhi ya watoto wenye vipaji wamekuwa wakikumbana na vikwazo kutoka kwa wazazi, jambo ambalo linachangia watoto kushindwa kufikia ndoto za vipaji walivyonavyo.

“Baadhi ya wazazi wamekuwa na mwitikio mdogo wa ushirikiano kwa watoto wao katika kuonyesha vipaji vyao, jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linachangia kuwakatisha tamaa na kusababisha kudidimia kwa vipaji vya vijana wengi waliopo kwenye jamii.

“Kusoma ni muhimu, lakini lazima tuendeleze uwezo na kipaji ulichonacho nje ya masomo, kwani kupitia kipaji alichonacho mtoto kinaweza kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii,” anasema.

Mahuvi anatoa wito kwa wazazi wajitahidi kuelewa watoto wao na kuwafuatilia maendeleo yao toka wanapoanza kujitambua ili wabaini talanta zao na kuziendeleza na watambue kuwa zama zimeshabadilika kwa sasa, vipaji vimezalisha sehemu kubwa ya ajira kwa vijana wengi wa kitanzania.


Kutengeneza fursa

Anasema kutokana nakubaini baadhi ya watoto kukosa ‘sapoti’ zitakazowasaidia kukuza na kuendeleza vipaji, wao kama wadau wa elimu nchini kwa kushirikiana na mashirika mengine ikiwemo Karimjee Foundation na Segal Foundation, tangu mwaka 2016 kupitia miradi yao ya Uwezo Award na Uwezo Bonanza, wamekuwa wakiwasaidia wanafunzi kukuza vipaji, ujuzi na maarifa waliyonayo ili waweze kuajirika na kujiajiri, hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya ajira nchini.

Akitolea mfano mradi wa uwezo wa bonanza, anasema wamekuwa wakiwafikia wanafunzi wenye vipaji katika shule mbalimbali za sekondari na kuwasaidia kuwapa mbinu pamoja na maarifa ya namna gani wanaweza kugeuza vipaji walivyonavyo kuwa fursa.

“Hadi sasa tumeweza kufikia shule zaidi ya 50 katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na tunaendelea kuwanoa na kuwashika mkono wanafunzi wenye vipaji mbalimbali kama vile kuimba, kuigiza, kuchora, kuruka sarakasi pamoja na wabuni wa mavazi,” anasema.

Vilevile, kuwaelekeza ni kwa namna gani wanaweza kutumia vipaji walivyonavyo kuzalisha fursa ya ajira kwao na vijana wengine.

Kwa upande wa Uwezo Award, Noelle anasema inawapa wanafunzi maarifa ambayo wanaweza kuyatumia kupitia rasilimali zilizopo katika mazingira yao kufanya shughuli za ujasiriamali.

Pia, kuwafundisha maarifa yanayohitajika katika karne ya 21 ambayo yatamsaidia mwanafunzi kutumia uwezo alionao na rasilimali zilizopo kutatua changamoto zinazoikabili jamii inayowazunguka.

“Tangu mwaka 2016, tulikuwa na lengo la kuwapa wanafunzi jukwaa la kujifunza ujasiriamali kwa vitendo wakiwa bado wako shuleni, ambapo wanafunzi wa shule za sekondari hupaswa kubuni na kutekeleza miradi ya kijasiriamali na fedha wanazopata hutumia kufanya miradi ya kijamii kwenye maeneo wanayochagua,” anasema.

Anasema kupitia jukwaa hilo, wanafunzi wanapata maarifa yatakayowawezesha kujitambua na kupata ujuzi katika maeneo ambayo wao wanaona wanayapenda na kuyamudu kuwajenga kujiamini na kuwa wabunifu ambapo, ubunifu wanaoutumia katika kufanikisha miradi yao utawasaidia kuwapa ujasiri wa kuanzisha miradi mbalimbali wanapotoka nje ya shule.

Akizungumza na Mwananchi, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule ya sekondari Kibiti, Rodgers Shipela anasema kupitia miradi hiyo ya Uwezo Award shuleni hapo, amefundishwa ni kwa namna gani anaweza kutumia vitu vilivyopo katika mazingira yake na kuwa fursa ambazo zitamwezesha kujiajiri na hata kutengeneza ajira kwa wengine.

Pia, anasema ameweza kupata maarifa mbalimbali ya kutengeneza bidhaa kama vile sabuni za maji, mishumaa na namna gani ya kufanya biashara.