Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KIUME: Komaa kiume, acha kutafuta wachawi vijiweni

Picha na AI

Muktasari:

  • Mwanamume unapaswa kukomaa, kupambana chini ya jua, na kukabili changamoto zako kiume badala ya kuhusisha kila anguko la kiuchumi na mambo ya giza.

Dar es Salaam. Kuna mtindo wa ovyo sana ulioshamiri kwenye jamii yetu siku hizi, hasa miongoni mwa baadhi ya wanaume ambao kila jambo likiwaendea mrama, kimbilio lao la kwanza ni kunyoosha kidole kwa ndugu zao au majirani vijijini.

Ukweli uliowazi lakini unaouma ni huu: hujarogwa, hujajipanga tu! Unakuta mwanamume mzima, mwenye nguvu zake na akili timamu, anashinda kijiweni tangu asubuhi hadi jioni akicheza dhumna au karata, halafu jioni mifuko ikikausha anaanza kulalamika.

"Ona mambo yangu hayanyooki kabisa, bila shaka mjomba wangu wa kambo kule kijijini amenifungia nyota yangu." Huu ni ujinga uliopitiliza, uvivu wa kufikiri, na kukwepa majukumu kulikoishiwa mipaka.

​Maisha hayajawahi kuwa mchezo wa mteremko, na hayaji kwa miujiza ya kukaa kitako na kusubiri mbele ya runinga au kijiweni. Imani hizi za ushirikina zimekuwa kama kichaka na blanketi la kujifunika kwa wanaume wengi wavivu, wanaotumia visingizio hivyo ili kuficha uzembe wao wa kutochukua hatua madhubuti za kubadili maisha yao.

Mwanamume unapaswa kukomaa, kupambana chini ya jua, na kukabili changamoto zako kiume badala ya kuhusisha kila anguko la kiuchumi na mambo ya giza.

Inashangaza kuona mwanamume anavyoweza kupata fedha leo, akazitumia bila bajeti yoyote, akanywa pombe na marafiki, akafanya starehe zisizo na tija, na kununua vitu vya kifahari vinavyozidi uwezo wake wa kipato, halafu kesho yake akifilisika anaanza kwenda kwa waganga wa kienyeji au kutafuta mafuta ya upako akidai amerogwa.

Hivi kweli hapo umerogwa na mtu mwingine au umerogwa na akili yako mwenyewe? Matumizi mabaya ya fedha, kukosa nidhamu ya akiba  na kuishi maisha ya kuigiza ili kuwaridhisha watu wa mtaani, ndiko kulikokufanya ufulie, wala si mchawi yeyote kutoka mkoani.

​Kama huna mpango kazi unaoeleweka wa miaka miwili au mitatu ijayo, kama huna vyanzo vingi vya mapato na bado unategemea mshahara mmoja mdogo usio na marupurupu, na kama huamki asubuhi na mapema kwenda kutafuta fursa mpya, maisha lazima yakupige ngumi ya uso.

Unaposhindwa kulipa kodi ya nyumba au unaposhindwa kusomesha watoto wako, usianze kutazama picha za ndugu zako kwenye simu ukiwatuhumu kwa uchawi.

Angalia ratiba yako ya siku nzima; unaamka saa ngapi? Unatumia muda wako kufanya nini? Je, unajishughulisha na kazi gani ya maana mbali na kupiga soga? Hapo ndipo utakapopata majibu ya umaskini wako, na si kwenye ramli chonganishi.

Heshima na hadhi ya mwanamume thabiti haipo kwenye kulalamika na kulia-lia kama mtoto aliyenyimwa pipi. Maisha ya uanaume yanahitaji kifua cha chuma na ngozi ngumu inayostahimili mapigo. Ukifanya biashara ikafa, usiseme washindani wako wamekuroga; kaa chini, fanya tathmini,  gundua wapi ulikosea, jifunze mbinu mpya za masoko, na uanze upya ukiwa na akili zaidi.

 Ukifukuzwa kazi, usidai kuwa bosi wako ana majini yanayomfanya akuchukie; jinoe, ongeza ujuzi wako, na utafute fursa nyingine kwa bidii na nidhamu kubwa zaidi.

​Acheni imani hizi potofu za kishirikina zinazozorotesha maendeleo na kuleta mifarakano isiyo na msingi ndani ya familia zetu. Hakuna mchawi mwenye nguvu ya kuzuia baraka za mwanamume anayeamka saa kumi na moja alfajiri, anayejitoa kwa jasho na damu mtaani, na anayeheshimu kila senti anayoipata kwa mikono yake.

Badala ya kupoteza muda na fedha zako chache zilizobaki kwenda kununua maji ya baraka au kulipa waganga ili wakupe "dawa ya mvuto wa biashara," tumia fedha hizo kama mtaji, badili mtazamo wako, weka mikakati inayotekelezeka na komaa kiume. Ndoto zako hazitafufuka kwa miujiza, bali zitafufuka kwa nguvu ya uamuzi wako na kujituma kwako bila kuchoka.