Kuficha ‘makucha’ kwenye uchumba kunavyotesa ndoa nyingi
Juma Manyama alianza kusali kwenye moja ya makanisa kwa lengo la kuonekana kwa Happiness naye ni mcha Mungu, ili iwe rahisi kwake kuanzisha uhusiano naye.
Anasema alivutiwa na Hapiness, lakini ili awe naye karibu, ilikuwa ni lazima naye aanze kusali kwenye kanisa alilokuwa akisali mwanamke huyo.
"Nilifanya hivyo kwa miezi mitatu, Hapiness alinielewa, akakubali nimchumbie tukafunga ndoa ambayo ilidumu kwa mwaka mmoja ikavunjika," anasema kwa hisia za maumivu Juma.
Anasema, baada ya ndoa hakuweza tena kuendelea kwenda kwenye kanisa la mkewe, ilikuwa ni ugomvi baina yao kila siku kutokana na yeye Juma kuonyesha tabia yake halisi.
Huo ni moja kati ya mifano mingi ya wapenzi kuonyeshana tabia bandia, ambazo si tabia zao halisi wakati wa uchumba na wanapoingia kwenye ndoa wanakuwa watumwa na wengine kushindwa kuendelea kuishi kwa kuigiza.
Mariam Mustapha, yeye anasema, katika miaka sita ya uhusiano wake na Rajabu hakuwahi kufahamu kama mumewe ni mlevi, siku zote wakiwa wote alikunywa soda.
"Alikuwa anaswali swala tano, nikajua ni ustadhi, kumbe hakuwa kama nilivyodhani, hata wazazi wangu leo hii nikiwaambia Rajabu anakunywa pombe watanikatalia, kwani katika miaka sita ya mahusiano yetu nilijua hanywi pombe, kumbe mwenzangu kwa miaka sita ya urafiki hadi mahusiano alikuwa anakunywa kwa siri.
"Siku ya ndoa ndipo nilijua anakunywa, nilishangaa kumuona anakunywa mvinyo, nikastuka, nikamkataza lakini ilishindikana, alipogundua nimejua hivi sasa anakunywa bila kificho," anasema.
Ndoa ya Shamira Jamal ilivunjika licha ya kuwa anapendana na mumewe kutokana na tabia yake bandia.
Anasema alianzisha uhusiano na mwanamume aliyemdanganya ana watoto wawili waliopo kwa baba yao Uganda.
"Yule mwanaume alinioa akijua nina watoto wawili, lakini nilikuwa na watoto wengine watano ambao hakuwajua, tuliishi vizuri jijini Mwanza kwa upendo, huku wale watoto sitaki kujua habari zao.
"Siku moja watoto wangu watatu waliamua kunitafuta, walikuja Mwanza, walielekezwa wakafika nyumbani na kutukuta na mume wangu ambaye aliposikia habari zao alishangaa, hakuwahi kujua kama niliacha watoto Dar es Salaam.
Anasema mumewe alikwenda kushtaki kwa bibi yake jambo hilo ambalo alimficha katika miaka saba ya ndoa yao.
"Bibi ili kusuluhisha akiamini anataka kuniweka huru akamwambia mume wangu, kwa kuwa amefahamu, basi hana budi kujua nina watoto saba, mume wangu alishangaa na akaniona sikuwa mkweli na palepale alinipa talaka," anasema.
Jemima Baraka, yeye anasema katika miaka mitano ya mahusiano na mumewe hakuwahi kufahamu kama anavuta sigara.
"Tumekuwa kwenye uchumba miaka mitatu bila kufahamu, nilijua miaka miwili baada ya ndoa, nilipomuuliza akanijibu kwa ujasiri, ndio navuta muda mrefu.
"Alipojua nimejua akataka kujihalalishia kuvuta muda na mahali popote akijisikia, nikawa mkali, hivi sasa hata nikikuta kipisi kimezagaa mazingira ya nyumbani, bila kujali ni yeye au si yeye nitamwambia akakitoe," anasema.
Anasema amejaribu kumuelimisha kuhusu athari za moshi wa sigara, lakini ni tabia ambayo mumewe anayo na hawezi kubadilika, hivyo ambacho anakizingatia ni kuhakikisha havutii ndani.
Daniel Dunia anasema alipomuoa mkewe, hakujua kama ni shabiki kindakindaki wa mpira wa miguu.
"Mimi naipenda Simba, yeye kumbe ni Yanga, lakini ili nisimjue tukiwa kwenye mahusiano alikuwa ananiambia hapendi mpira na hayo si mambo yake, alikuwa akifanya hivyo akijua mimi ni Simba, hivyo yeye kuwa yanga angenikera.
"Nilipomvalisha pete tu, akaanza kuvaa jezi ya Yanga, ndipo nyumbani kwao wakaniambia kama hakuwahi kukwambia pole, huyo ni Yanga lialia, ambacho hakunificha ni jinsi asivyopenda marafiki," anasema.
Daniel Mzena anasema chanzo cha tabia bandia inatokana na namna mlivyoanza mahusiano yenu, akitolea mfano yeye na mkewe wana mwaka wa 16, lakini ni kama wamefahamiana jana. "Hatukuanza kwa uongo, ndio sababu tumedumu hadi sasa," anasema.
Athari za tabia bandia
Mchambuzi wa masuala ya malezi na mahusiano, Christian Bwaya anasema athari ya kwanza kwa mtu anayeonyesha tabia bandia kwa mwenzake ni kuishi kama mtumwa kwenye mahusiano.
"Hali hii sasa itasababisha mahusiano yao kukosa utoshelevu na pale atakapoanza kuonyesha tabia zake halisi kule kumuamini kwa mwenzake kunapungua.
"Katika mahusiano mnapoanza inatakiwa mtu awe yeye, hivyo ulivyo kuna mtu atakupenda tu, shida ni kwamba watu wanataka vitu ambavyo sio vyao.
Akitolea mfano kwa mwanamke aliyepata mtoto kabla ya ndoa, ukipata mchumba hakuna haja ya kuficha, kwani kama ni kaka ambaye ishu ya mtoto haimsumbui atakupenda na mtoto wako na kukuoa.
"Tabia bandia huwa haina maisha marefu kwenye uhusiano, athari zake ni nyingi, ikiwamo migogoro mikubwa kwenye uhusiano na huwa haiishi.
"Hii inakuwa mtu anajijua ana tabia fulani fulani anazificha ili apate kizuri anachokitaka, ikifahamika baadaye inaondoa kufahamiana ambayo italeta shida kwa kuwa kuaminiana ndiyo msingi wa mahusiano".
Anasema kuigiza katika mahusiano kunatumia nguvu nyingi na mahusiano yanakosa ladha kwa kuwa mtu anapata raha anapoonyesha tabia yake, hivyo akiigiza anakuwa mtumwa na hapo raha ya ndoa inapotea.
"Mfano ndoa ya Kikristo huwa haina talaka, mtu anaingia na kukutana na matabia tofauti ambayo hakuwahi kuyafahamu kabla mlipokuwa wachumba, lazima mtagombana.
"Kisaikolojia mahusiano yanahusisha watu wawili waliojikubali, jitambua na kuyafahamu mapungufu yao vizuri, hivyo wanaunganisha utambulisho wao na kuwa utambulisho mmoja, lazima kila mmoja aonyeshe rangi yake ili iwe rahisi kwa mwingine kuikubali na kumkubali mwenzake na si kuonyesha tabia bandia."
Kisaikolojia ipo hivi
Mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya malezi, Mchungaji Daniel Sendoro anasema hadi mtu kuishi kwa kudanganya ili apate kitu fulani, ikiwamo kuanzisha mahusiano huo ni ukosefu wa maadili.
"Wapo ambao wanadanganya kwa kuwa wana nia ya kumuoa mtu, hivyo wanachagua kuigiza maisha, lakini baada ya muda atarudi kuishi maisha yake halisi.
"Akishafanikiwa dili lake anaanza kuonyesha tabia yake halisi, kama mnywaji pombe au mtu wa kuchelewa kurudi nyumbani, ataanza tu kuonekana.
Anasema athari inaanza pale mwenza wake anapomuona ni mtu mwingine tofauti na yule aliyemfahamu na hapo ndipo migogoro inaanza.
"Kinachofuata ni ndoa kuvunjika au mmojawapo kuanza usaliti, zikianza vurugumechi hizo, basi hiyo ndoa itakosa amani.
Sendoro, ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, anasema kinachotakiwa, mnapoanza mahusiano, mwanzoni kila mmoja anapaswa kuonyesha rangi yake halisi.
"Hii itasaidia mwenzako kukujua vema, hata huko mbele ya safari haitasumbua, pia kila mmoja ajiongeze kumfahamu mtu kabla ya kuingia kwenye ndoa, pamoja na maneno yake, chukua muda kumfahamu.
"Kwa mwanamke, usimpende tu mwanamume sababu anakupa pesa au kulipa bili, anaweza kufanya hivyo huku akikuona mjinga, maisha ni zaidi ya mali," anasema.
"Utakuta huyo mwanaume anakwenda kuangalia mpira nje ya nyumba yake hadi saa 7 usiku na kumuacha mkewe ndani, yeye anaona ni kawaida, hivyo zile harakati za mtoto wa kike zingekuwa sawa na upande wa pili," anasema mchungaji Sendoro.