Kwanini wajawazito wanakula vitu hivi?

Sunday December 27 2020
Wajawazito pic

Kwa mujibu wa umoja wa madaktari wa magonjwa ya akili duniani, ulaji wa vitu ambavyo si vyakula ni mojawapo ya matatizo ya ulaji yanahusishwa na matatizo ya kiakili.

Tatizo hili hujulikana kitabibu kama ‘pica’ na huweza kugundulika na kubainishwa endapo itaonekana kwa mtu kuwa na tabia hii kwa zaidi ya mwezi mmoja. Tatizo hili linaonekana zaidi kwa wajawazito, watoto na wenye magonjwa ya akili.

Vitu hivyo ambavyo si lishe vinavyopendelewa kutafunwa na hata kumezwa ni pamoja na udongo, chaki, mkaa, raba, plastiki, mawe, barafu, mbao na makaratasi. Pia wapo wanaopendelea kula vyakula visivyopikwa ikiwamo utafunaji wa mchele.

Ulaji wa vitu hivi unaweza kumweka muathirika katika hatari ya kula vitu vyenye sumu, uambukizi na vya kusababisha majeraha katika mfumo wa chakula, kupata mzio (allergy), maumivu ya tumbo, ukosefu wa haja kubwa na kupata upungufu wa vitamini na madini mwilini.

Moja ya maswali ninayokutana nayo mara kwa mara ni kwanini wajawazito wanapata sana tatizo la pica.

Jibu ni hili, tatizo la pica linawapata zaidi wajawazito kutokana na mabadiliko yanayotokea kipindi cha ujauzito yanayosababisha ongezeko la uhitaji mkubwa wa virutubisho.

Advertisement

Hali hii kwa wajawazito huweza kuonekana zaidi katika muhula wa kwanza wa ujauzito yaani miezi mitatu ya kwanza. Ingawa hali hiyo inaweza kuwepo katika muhula wowote wa ujauzito.

Vile vile hali hii kwa wajawazito inahusishwa na upungufu wa madini ya chuma ambayo huwa ni kawaida kutokea wakati wa ujauzito.

Ikumbukwe kuwa hali ya ujauzito huweza kuleta mabadiliko kadhaa katika mfumo wa chakula ikiwamo kupata kichefuchefu, kutapika na kukosa hamu ya kula. Hali kama hii inaweza kuleta upungufu wa madini na vitamin mwilini.

Hali ya ujauzito ina uhitaji mkubwa wa virutubisho ikiwamo kwa mjamzito mwenyewe na mtoto aliye katika nyumba ya uzazi ambaye huitaji kwa ajili ya maendeleo ya ukuaji.

Tatizo hili halina madhara makubwa lakini matokeo yake yanaweza kuwa na madhara mfano inapotokea upungufu wa damu. Ingawa tatizo la picha linaweza kupotea lenyewe kadiri ujauzito unavyopiga hatua ila ni muhimu kulishtakia mapema katika huduma za Afya.

Inasisitizwa mjamzito kuhudhuria kliniki kama ilivyopangwa, huko anaweza kubainika na tatizo hili akapewa vidonge vya vitamin na madini pamoja na ushauri nasaha ili kukabiliana na pica.

Hali hiyo ikidumu kwa muda mrefu inaweza kuleta athari kwa mjamzito na mtoto aliye katika nyumba ya uzazi. Mjamzito anaweza kupata upungufu wa damu na ukuaji wa mtoto ukawa chini.

Hali ya kutapika na kichefuchefu inaweza kuhitajika kudhibitiwa ili kupunguza hatari ya kupoteza virutubisho kwa kutapika au kukosa hamu ya kula.

Hakuna kipimo maalumu cha kubaini tatizo hili, zaidi ni daktari kuchukua historia, kufanya uchunguzi wa kimwili na vipimo vya damu.

Ili kukabiliana na pica mjamzito ashikamane na ushauri na matibabu anaopewa kliniki, vilevile ajitahidi kula mlo uliosheheni makundi yote ya vyakula.

________________________________________________________________

Na Dk Shitta Samweli


Advertisement