Prime
Mbinu kuhimili misukosuko ya ujane na ugane
Picha na Akili Unde.
Muktasari:
- Ndani ya jamii zetu, mara nyingi maumivu ya ujane na ugane hufichwa chini ya maneno ya “vumilia” au “endelea na maisha”, bila nafasi ya kutosha ya kuelewa kina cha majonzi anayopitia mhusika.
Mwanza. Ujane na ugane ni hali zinazobeba uzito mkubwa wa kihisia, kijamii na kiroho. Kupoteza mwenza wa maisha au kuvunjika kwa ndoa si tukio dogo; ni mtikisiko unaogusa moyo, akili na mwelekeo mzima wa maisha.
Ndani ya jamii zetu, mara nyingi maumivu ya ujane na ugane hufichwa chini ya maneno ya “vumilia” au “endelea na maisha”, bila nafasi ya kutosha ya kuelewa kina cha majonzi anayopitia mhusika.
Mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya huzuni, Elisabeth Kübler-Ross anaeleza kuwa huzuni ni mchakato wa kujifunza kuishi bila kile kilichopotea. Anasema kuwa maumivu haya hayaishi haraka, bali hubadilika polepole kadri mtu anavyojifunza kukubali hali mpya. Anaandika: “Ukweli ni kwamba huwezi kuondokana kabisa na huzuni; unajifunza tu kuishi nayo.”
Kauli hii inaelezea kwa kina hali ya mjane au mgane anayelazimika kujenga maisha mapya akiwa na kumbukumbu nzito ya yaliyopita.
Dini zetu zinatambua uzito wa maumivu haya na zinatoa faraja ya kiroho. Quran Tukufu inasema: “Na hakika tutakujaribuni kwa khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na matunda; na wabashirie wanaosubiri.” (Suratul Baqarah: 155).
Aya hii inakiri kuwa misukosuko ni sehemu ya maisha, lakini pia inaweka msingi wa matumaini kwa anayevumilia.
Nayo Biblia Biblia inawatia moyo wajane na wagane kuwa na subira, uvumilivu, na tumaini kwa Mungu wanapopitia maombolezo na changamoto za maisha. Zaburi 68:5 inasema: "Mungu katika maskani yake takatifu ni baba wa yatima, na mwamuzi wa wajane." Pia Zaburi 146:9 inaeleza: "Bwana huwalinda wageni; huwategemeza yatima na mjane; bali njia ya wasio haki huipotosha."
Katika maisha ya ujane na ugane, mtu hujikuta akipambana na maswali mazito: nitaanzaje upya, nitakabiliana vipi na upweke, na jamii itanichukuliaje?
Haya yote ni maswali halali yanayohitaji majibu ya polepole, si ya haraka. Kukubali maumivu ni hatua ya kwanza ya kuhimili misukosuko hii.
Simulizi waathirika
Asha Mwinjuma anasema alipoteza mume wake ghafla baada ya kuugua kwa muda mfupi, na kuwa siku ya mazishi ilikuwa mwanzo wa safari ngumu, ambayo hakuwahi kuifikiria baadhi ya ndugu wanaume kila mmoja akitolea macho mali za marehemu.
"Familia ya marehemu ilianza kuingilia maisha yangu... wasimamizi wa urithi walijitokeza wakidai kusimamia mali zote alizoacha mume wangu nyumba, shamba, hata biashara ndogo niliyokuwa naitegemea walitaka ziwe chini yao,"anasema.
Anasema bahati nzuri ilipigwa kura nani awe msimamaizi aliyepigiwa kura ni mtu aliyekuwa anamjali hivyo alianza kupata afueni.
"Changamoto iliyotokea ni baadhi ya ndugu kutaka kuanzisha uhusiano na mimi wakisema kama nitakataa nitakuwa na hali ngumu mimi na watoto wangu...lakini nashukuru Mungu nilisimamia msimamo wangu na watoto wangu niliyoachiwa watatu walisomeshwa na mjomba wao ambaye ndiye aliteuliwa kuwa msimamizi,"anasema.
Awali nilikuwa na msongo mkubwa wa mawazo nikijiuliza kama na huyu anayesimamia mali za marehemu mume wangu akinitaka kimapenzi na ndiye anayenisaidia kulipa ada itakuwaje?
Ina maana nikikataa ndiyo atasitisha huduma kwa watoto wangu? wanaachwa bila ada ya shule, chakula, au mahitaji ya msingi hofu iliyonipa wakati mgumu hadi sasa navyoongea na wewe maana mume wangu ana miaka miwili tangu afariki,"anaeleza.
Kwa uande wake, Haruna Juma anasema alipoteza mke wake baada ya kujifungua mtoto wao wa tatu kifo kilichomuacha katika hali ya kuchanganyikiwa, kwakuwa hakuwa tayari kuwa mzazi wa watoto watatu peke yake.
"Awali nilidhani maisha yataendelea kawaida lakini niligundua watoto walihitaji uangalizi wa karibu, chakula, usafi, shule na hasa upendo wa mama ambao sikuweza kuutoa kwa kiwango kilekile," anaeleza.
Anasema kazi yake ilianza kuathirika, alipochelewa kazini au kuomba ruhusa ili kumtunza mtoto mgonjwa, alionekana mwajriwa asiye wajibika.
Anasema alikumbwa na upweke pamoja na msongo wa mawazo kwakuwa hakukuwa na mtu wa kushirikiana naye kimawazo, wala wa kumsaidia kupanga maisha ya familia.
"Watu walinipa pole, lakini wengi waliniambia nioe tena lakini suala la changamoto za mama wa kambo lilizidi kunipa stress (msongo wa mawazo), mwishowe niliamua kuoa ili nifanye kazi bila shida na watoto wangu wapate malezi bora,"anasema.
Kujijenga upya
Mwandishi na mshauri wa masuala ya majonzi C.S. Lewis, aliyepitia uchungu wa kumpoteza mke wake, anaeleza kwa undani safari ya huzuni.
Anaeleza kuwa huzuni humvua mtu kinga zote za ndani na kumwacha akiwa mnyonge.
“Huzuni bado inahisi kama woga, isipokuwa huna pa kukimbilia," anasema.
Kauli yake inaakisi hali ya mjane au mgane anayehisi kutokuwa na usalama baada ya kupoteza nguzo ya maisha yake.
Hadithi ya Mtume Muhammad (Rehema na amani ziwe juu yake) pia inatoa mwelekeo muhimu. Mtume amesema: “Ajabu ilivyo hali ya muumini; mambo yake yote ni kheri. Akipata neema hushukuru, nayo huwa kheri kwake; na akipata msiba husubiri, nayo huwa kheri kwake.”
Hadithi hii inaweka msingi wa mtazamo chanya hata katika hali ngumu kama ujane na ugane.
Mwanasaikolojia, Viktor Frankl, aliyenusurika mateso makubwa ya kambi za mateso, anaeleza kuwa binadamu anaweza kustahimili karibu hali yoyote ikiwa ataona maana ndani yake.
Anaamini kuwa mateso yasiyo na maana humvunja mtu, lakini mateso yenye maana humjenga.
“Yule aliye na sababu ya kuishi anaweza kustahimili karibu ‘vipi’ lolote," anaandika.
Kauli yake ni somo muhimu kwa mjane au mgane anayejifunza kuona maisha yake mapya kama fursa ya maana mpya.
Katika hatua hii, mbinu muhimu si kukimbia upweke, bali kujifunza kuishi nao kwa hekima.
Kujenga mazoea mapya, kuimarisha uhusiano na Mungu, na kuruhusu muda ufanye kazi yake ni sehemu ya safari ya uponyaji.
Hatua za kuendelea na maisha
Mwandishi wa kiroho, Henri Nouwen anaeleza kuwa majeraha ya maisha yanaweza kuwa vyanzo vya huruma na hekima.
Anasema kuwa mtu aliyejeruhiwa ana uwezo mkubwa wa kuwafariji wengine. Nouwen anaandika: “Majeraha yetu, yakikubaliwa, yanaweza kuwa vyanzo vya uponyaji.”
Kauli hii inafungua mlango wa kuona ujane na ugane si mwisho wa maisha, bali mwanzo wa jukumu jipya ndani ya jamii.
Changamoto kubwa kwa wajane na wagane si maumivu pekee, bali pia mitazamo ya jamii. Wengine hutazamwa kwa huruma kupita kiasi, wengine kwa mashaka, na wengine kwa dharau.
Hali hii huongeza mzigo wa kisaikolojia. Ndiyo maana mojawapo ya mbinu muhimu za kuhimili misukosuko hii ni kuchagua sauti za kuwasikiliza na kujenga mtandao wa watu wanaoelewa na kuheshimu safari yako.
C.S. Lewis anaongeza kwa kusema: “Huzuni inashirikishwa vyema kuliko kufichwa.” Tafsiri hii inakumbusha kuwa kujitenga kupita kiasi kunaweza kuzidisha maumivu. Kushirikiana na watu sahihi, iwe ni familia, marafiki au jumuiya ya kiimani, husaidia kupunguza mzigo wa ndani.
Ni muhimu kukumbuka maisha ya ujane na ugane ni mojawapo ya safari ngumu zaidi katika maisha ya binadamu. Hata hivyo, kwa kutumia mbinu za kiroho, kihisia na kijamii, misukosuko hii inaweza kuhimilika.
Kukubali maumivu, kumtegemea Mwenyezi Mungu, kutafuta maana mpya ya maisha na kuruhusu watu sahihi kusaidia, ni nguzo muhimu za safari hii.