Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MWALIMU WA MAISHA: Mapenzi pekee yatosha kudumisha ndoa yenu?

Picha na Mtandao.

Katika ulimwengu wa sasa, wengi huingia kwenye ndoa au uhusiano, wakiamini kuwa mapenzi ya dhati pekee yanatosha kudumisha uhusiano wa kudumu.

Hili ni swali ambalo wataalamu wa uhusiano wamekuwa wakiulizwa mara kwa mara: Je, upendo pekee unatosha?

Wataalamu wa saikolojia ya familia wanatufundisha kuwa mapenzi ni msingi muhimu, lakini si wa kutegemewa peke yake. Dk Miriam Lukumeta mshauri wa ndoa na familia, anasema:

“Mapenzi ni kama mbegu. Inapandwa, lakini ili imee na kustawi, inahitaji maji (mawasiliano), mwanga wa jua (kuaminiana), na mbolea (muda pamoja, msaada wa kihisia na kihisia).”


Nini kingine kinahitajika?

Ukweli ni kuwa, ndoa au uhusiano wa muda mrefu unahitaji zaidi ya hisia kali. Unahitaji mawasiliano ya wazi: Kukaa na kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia, matarajio, na changamoto.

Heshima na uaminifu: Kuaminiana hujengwa kwa muda, na huhitaji heshima ya kila mmoja kwa mwenzake.

Kujitolea: Kuna nyakati mapenzi hupungua kwa muda, lakini kujitolea huendelea kuwa daraja la kuyavuka mawimbi magumu.

Kukubaliana kutokubaliana: Hakuna uhusiano usio na migongano. Siri ni namna mnavyokabiliana nayo kwa hekima. Janeth na George, wanandoa waliokuwa karibu kuachana baada ya miaka mitano ya ndoa, wanasema:

“Tulianza kwa kupendana sana, lakini baadaye hatukuweza kuelewana hata kuhusu vitu vidogo. Tulipoenda kutafuta ushauri wa ndoa, tuligundua kwamba tulikuwa hatuna muda wa kuzungumza wala kusikilizana. Tuliishi kama wapangaji. Tulijifunza upya namna ya kuwa marafiki,” anasema Janeth.

Kama unajikuta katika uhusiano ambao una changamoto, usikate tamaa. Tambua kuwa hisia za mapenzi zinaweza kufifia lakini huweza kurudishwa kwa kujitahidi pamoja. Tafuteni msaada, ongeeni kwa uwazi, na kumbukeni sababu iliyowaleta pamoja.


Kumbuka na haya

Ili ndoa idumu zaidi kwa miaka mingi, nakushauri pia kuzingatia haya;

Mosi, wanandoa wanapaswa kujifunza kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia zao, changamoto, na matarajio yao.

Ukimya au kuficha mambo huweza kuleta umbali mkubwa kati ya wawili. Kusikilizana kwa makini ni sehemu ya mawasiliano bora.

Pili, heshima ni msingi wa kila ndoa yenye afya. Hata kama kuna kutokubaliana, ni muhimu kuheshimu mawazo na utu wa mwenza wako. Maneno mabaya au dharau huumiza na kuharibu uhusiano taratibu

Tatu, uvumilivu na msamaha ni muhimu sana. Hakuna mtu mkamilifu, na makosa hayaepukiki.

Kujifunza kusamehe na kuendelea mbele huimarisha uhusiano badala ya kuuvunja. Kushikilia makosa ya zamani kunaweza kuleta chuki na maumivu yasiyoisha.

Nne, ushirikiano katika majukumu ya kila siku huleta usawa. Ndoa si jukumu la mtu mmoja; ni juhudi za pamoja. Kugawana majukumu ya familia na kusaidiana hujenga mshikamano na kuondoa mzigo kwa mmoja.

Mwisho, jitihada za makusudi kudumisha urafiki ndani ya ndoa ni muhimu. Wanandoa wanapaswa kutumia muda pamoja, kucheka, na kufurahia uwepo wa kila mmoja.

Urafiki huu huimarisha uhusiano hata pale hisia za kimapenzi zinapopungua.

Kwa kifupi, mapenzi ni mwanzo mzuri, lakini nidhamu, heshima, mawasiliano, na uvumilivu ndiyo hulinda ndoa kwa muda mrefu.