Tokelezea kimtindo katika msimu huu wa mvua
Kipindi cha mvua, watu wengi wanatafuta njia ya kujikinga na baridi, hivyo kuvaa baadhi ya mavazi yatakayokuwa rafiki kuendana na hali ya hewa.
Mavazi unayoweza kuvaa katika msimu huu wa mvua
Damini koti - ni aina ya koti lenye kitambaa cha jeans nzito inayoweza kukinga baridi. Siku za hivi karibuni koti hizi zimekuwa zikivaliwa sana na kuwa mtindo unaotrendi, si kwa wanaume wala wanawake.
Damini koti zipo za aina mbalimbali, mfano kuna ambazo zinakuwa fupi usawa wa tumboni, mara nyingi hupendelewa kuvaliwa na wanawake, nyingine ndefu usawa wa kiuno huvaliwa na wanawake kwa wanaume.
Mtindo huu unabamba sana ambao utakusaidia kujikinga na baridi, pia kupata mwonekano wa kipekee. Damini koti inaweza kuvaliwa na tisheti kwa ndani au shati ya mikono mirefu kwa wanaume. Kwa wanawake, inaweza kuvaliwa na gauni ndefu au fupi wakati mwingine sketi.
Pia damini koti inaweza kuvaliwa na suruali ya jeans iwe mwanamke au mwanaume, kwa chini pigilia raba au viatu vya kufunika miguu kama mizunguko yako ya kawaida na kama unaelekea ofisini vaa damini koti na mavazi casual ya kiofisi.
Trakisuti- seti ya nguo isiyobana na yenye joto inayojumuisha fulana na suruali yenye kiuno kilichotengenezwa kuachia mwili au kuvutika, huvaliwa wakati wa kufanya mazoezi au kama vazi la kawaida.
Hizi sio nguo za kukosa katika msimu huu wa mvua kutokana na kitambaa kilichotumika kutengenezea kuwa na pamba laini inayoleta joto.
Unaweza kuvaa trakisuti yenye mpangilio mzuri wa rangi zinazoleta mvuto, chini ukavalia na sendo za ngozi, sendo aina ya plastiki zilizofunikwa juu ili kuzuia baridi bila kusahau soksi.
Wakati mwingine trakisuti unaweza kuivalia na raba zilizopanda juu kukinga na matope na haishauriwi sana kuvaa za rangi nyeupe kwa sababu zinaweza kuchafuka haraka na matope endapo unatumia usafiri wa umma au maeneo ambayo miundombinu yake siyo rafiki.
Prova - hizi ni aina ya sweta nzito ambazo zina kola ya duara, siku za hivi karibuni zimekuwa zikivaliwa sana na kuwa mtindo pendwa ambao hauchagui jinsi na mazingira ya kuvaa. Katika msimu huu wa mvua, linaweza kuwa vazi rafiki linalovutia, hasa likivaliwa katika mpangilio mzuri na kwa unadhifu ili kuleta mwonekano wa kipekee. Prova inaweza kuvaliwa na suruali, gauni pamoja na sketi.
Tisheti na suruali kubwa, hiki ndicho kipindi chake kwa sababu ya muonekano wake, ‘boyfriend jeans’, hizi ni aina ya suruali ambazo hazishiki mwili kutokana na kuwa pana, zina kitambaa kizito kiasi hivyo kuukinga mwili na baridi.
Pia tisheti pana hizi zinasaidia kujikinga na baridi, hasa zikiwa za mikono mirefu.
Jaketi zito - ni koti zenye kitambaa cha ngozi ‘leather’, hizi ni nzuri kutokana na kuzuia kulowana, pia zina joto, hivyo kukukinga na baridi. Koti hizi zinaweza kuvaliwa na nguo yoyote na mahali popote.
Mitandio mizito- ni fasheni inayopendwa tangu kipindi cha zamani na wengi huivaa kwa kujitanda juu hasa kipindi cha baridi.
Siku hizi mitandio hiyo imeboreshwa kwa kushonwa ambapo inavaliwa kama nguo kwa juu. Pia unaweza kuvaa mtandio shingoni kukinga baridi na kupata mwonekano wa kipekee.
Mabaibui na maabaya mazito, hasa kwa wale wasioweza kuvaa nguo za kawaida. Katika jamii haya yamekuwa mavazi yaliyozoeleka kuvaliwa bila kujali kipindi au hali ya hewa, lakini katika kipindi hiki cha mvua unaweza kutokelezea na baibui lako zito linalokupa mwonekano mzuri, pia kukukinga na baridi.