TUONGEE KIUME: Dalili ndoa yake ilishakufa

Kuna ndoa zimekufa lakini bado wanandoa hawajatengana au kutalikiana. Wanaendelea kuishi chini ya paa moja la nyumba, kulala chumba kimoja, wengine hata kitanda na shuka bado wanachangia.

Wapo wanaofanya hivyo kwa makusudi, kwamba wanajua ndoa zao hazina uhai tena lakini wanajitoa ufahamu kwa kuamua kutofanya chochote kuhusiana na ndoa yao. Na wapo ambao wenyewe hawana habari kabisa kwamba kati yao hakuna ndoa tena, kuna watu waliowahi kuoana na sasa wanaishi kama familia. Hawa wenyewe wanaweza kuona mambo yanavyokwenda vibaya lakini wasijue kwamba ndiyo angamio linaendelea hivyo wanahitajika kufanya kitu ili kuokoa ndoa au maisha ya wanandoa.

Kwa kukumbushana tu — hizi ni baadhi ya dalili ndoa yako imeshakufa.

Unaishi kama hujaoa

Wakati unaoa ulibadilisha mtindo wa maisha, kuna baadhi ya tabia uliachana nazo. Lakini sasa ghafla tu unajikuta umezirudia bila kujituma. Unaweza ukachelewa kurudi nyumbani bila taarifa, wengine hadi hawarudi kabisa. Unazungumza na wanawake wengine hovyo hovyo kwa ajili ya kuonana nao kimapenzi, marafiki wako wa ajabu ajabu umewarudia na makorokoro mengine yote ambayo hayapendezi kufanywa na mtu aliyeoa.

Na hii inatokea tu, unaweza kusema bila kukusudia kwa sababu roho ya ndani tayari inafahamu kwamba wewe haupo kwenye ndoa tena, ni kapera. Ukiona dalili hii kubwa, angalia namna ya kutafuta suluhisho kwa namna ya kuwafaa nyote wawili.

Kutomuamini mpenzi wako hakukuumizi tena

Kipindi ndoa yenu iko hai ilikuwa ukihisi kutomuamini mke wako unakumbwa na wivu na wasiwasi. Mfano, alikuaga akitoka kazini, kabla ya kurudi nyumbani atapita sehemu lakini atawahi kurudi. Lakini mara anapitisha muda. Unaamua kumpigia simu, mara ya kwanza inaita hapokei, mara ya pili hapokei, ya tatu hivyo hivyo na ya nne ndiyo hapatikani kabisa. Unaingiwa na wasiwasi, sio wasiwasi kwamba inawezekana kapata ajali au tatizo, bali kwamba labda yuko sehemu anavunja uaminifu.

Lakini ndoa yenu ikiwa mfu-hai. Apokee simu au asipokee wewe unaona sawa tu, arudi nyumbani au asirudi yote heri kwako, zaidi unaweza kuitumia kama chachu ya kuzusha ugomvi nyumbani lakini ndani yako ukielewa kabisa kwamba sio kwa sababu ulitaka awahi kurudi bali unataka tu ugomvi.

Mipango yako haimuhusishi

Mwanzo mlikuwa na mpango wa kupanga fremu mbili, kisha kuzitoboa katikati na kutengenezea duka kubwa, na mipango mingine mingi ya kimaendeleo. Lakini ghafla unajihisi kama humuhitaji tena kwenye mipango ya namna hiyo. Unahisi unaweza kufanya mwenyewe, bila msaada wake.

Kimsingi ni kweli unaweza kufanya mwenyewe na hata mara ya kwanza wakati unamshirikisha ilikuwa unaweza kufanya mwenyewe pia. Ila kilichokufanya ugundue hilo kwa sasa ni kwa sababu nafsi yako ndani haimchukulii tena kama mwenza wako. Bali mtu tu.