Ulaji wa pamoja siri ya afya bora kwa familia
Muktasari:
- Wataalamu wa afya na ustawi wa jamii wanaeleza kuwa kula pamoja kama familia kuna mchango mkubwa katika kujenga afya bora ya mwili, akili na uhusiano wa kifamilia.
Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa iliyojaa pilikapilika za maisha, familia nyingi zimejikuta zikikosa muda wa kukaa pamoja hata wakati wa kula.
Wengine hula kila mmoja kwa wakati wake kutokana na kazi, shule au matumizi makubwa ya simu na televisheni.
Hata hivyo, wataalamu wa afya na ustawi wa jamii wanaeleza kuwa kula pamoja kama familia kuna mchango mkubwa katika kujenga afya bora ya mwili, akili na uhusiano wa kifamilia.
Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, familia zinazokaa pamoja mezani mara kwa mara, huwa na nafasi kubwa ya kujenga mawasiliano mazuri baina ya wazazi na watoto. Wakati wa kula huwapa wanafamilia nafasi ya kuzungumza, kusikilizana na kujadili mambo mbalimbali ya maisha yao ya kila siku.
Mwanasaikolojia, Rachel Julius anaeleza kuwa watoto wanaokula pamoja na wazazi wao hupata hisia za usalama, upendo na kuthaminiwa ndani ya familia.
Hali hiyo huwasaidia kuwa karibu zaidi na wazazi wao na kuwa tayari kueleza changamoto wanazokutana nazo shuleni au katika maisha yao ya kawaida.
“Kula pamoja si suala la chakula pekee, ni muda muhimu wa kuimarisha ukaribu wa familia. Mazungumzo yanayotokea mezani yanaweza kusaidia kujenga kujiamini kwa watoto na kuondoa upweke,” anaeleza mwanasaikolojia huyo.
Mbali na kuimarisha uhusiano, wataalamu wa afya wanasema kula pamoja kunaweza kusaidia familia kuwa na mtindo bora wa lishe.
Mara nyingi familia inapokaa pamoja kula, huwa rahisi kwa wazazi kufuatilia aina ya chakula kinacholiwa na watoto wao na kuhakikisha wanapata lishe yenye virutubisho muhimu.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa watoto wanaokula pamoja na familia mara kwa mara huwa na uwezekano mdogo wa kula vyakula visivyo na afya kwa wingi, kama vile vyakula vya haraka, vinywaji vyenye sukari nyingi na vitafunwa visivyo na virutubisho.
Aidha, watoto hao hujifunza tabia nzuri za kula na kuwa na nidhamu mezani.
Wataalamu wa lishe wanaeleza kuwa kula pamoja kunaweza kusaidia pia kupunguza tatizo la unene uliopitiliza. Familia inapopika na kula nyumbani mara nyingi huwa rahisi kudhibiti kiwango cha mafuta, sukari na chumvi katika chakula ikilinganishwa na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vya mitaani au vilivyosindikwa.
Faida zaidi
Faida nyingine inayotajwa ni afya ya akili. Katika kipindi hiki ambapo watoto na vijana wengi hukumbwa na msongo wa mawazo, kula pamoja huwapa nafasi ya kuzungumza hisia zao na kupata msaada kutoka kwa familia.
Wazazi wanaweza kugundua mapema mabadiliko ya tabia au changamoto zinazowakabili watoto wao kupitia mazungumzo ya kawaida wakati wa kula.
Aidha, kula pamoja huweza kusaidia kupunguza matumizi makubwa ya simu na televisheni ndani ya familia.
Wataalamu wanashauri familia kutenga muda maalumu wa kula bila kushughulika na vifaa vya kielektroniki ili kuongeza umakini na mawasiliano.
Katika baadhi ya familia, tofauti za ratiba zimekuwa zikifanya iwe vigumu kwa wanafamilia wote kukutana kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, wataalamu wanasema si lazima iwe kila siku au kila mlo. Hata kula pamoja mara chache kwa wiki kunaweza kuleta faida kubwa kiafya na kijamii.
Wazazi wanashauriwa kutumia muda wa kula kujenga mazingira ya furaha badala ya lawama au ugomvi. Mazungumzo mepesi, utani na kusikilizana vinaweza kuwafanya watoto waone muda wa kula kuwa sehemu salama na yenye upendo.
Pia watoto wanapohusishwa katika maandalizi ya chakula, kama kuandaa meza au kusaidia jikoni, hujifunza uwajibikaji na umuhimu wa kushirikiana kama familia. Hali hiyo inaweza kuimarisha mshikamano na kuwafanya wajione kuwa sehemu muhimu ya familia.
Aidha, familia yenye mawasiliano mazuri huwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha. Kula pamoja mara kwa mara ni moja ya njia rahisi zinazoweza kusaidia kujenga mshikamano huo bila gharama kubwa.
Katika jamii nyingi za Kiafrika, kula pamoja ilikuwa sehemu ya utamaduni uliowakutanisha wanafamilia na hata majirani.
Hata hivyo, mabadiliko ya maisha na maendeleo ya teknolojia yamefanya baadhi ya familia kupoteza desturi hiyo.
Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kurejesha utamaduni wa kula pamoja ili kuimarisha afya na uhusiano ndani ya familia.
Kula pamoja si tu suala la kushiba, bali ni njia muhimu ya kujenga upendo, mawasiliano na afya bora kwa familia nzima. Kupitia muda huo wa pamoja, familia inaweza kujenga ukaribu, kusaidiana na kuimarisha ustawi wa kila mwanachama wake.