USHAURI WA DAKTARI: Unazuia U.T.I kwa kufanya hivi

U.T.I ni kifupisho cha Urinary Truck Infections, kwa Kiswahili ni maambukizi kwa njia ya mkojo. Ni tatizo linalowapata wanawake wengi na kujirudia mara kwa mara.

Zipo njia rahisi ambazo zikifanyika zinaweza kusaidia kupunguza au kuzuia mwanamke kupata U.T.I mara kwa mara.

Moja ya njia hizo ni kunywa maji kwa wingi kila siku, angalau mtu mzima wa kilo 72 anywe lita 1.5 kwa siku.

Hii itamfanya mhusika huyo kupata haja ndogo mara kwa mara na kukojoa, hivyo kutotoa nafasi kwa bakteria kujenga makazi kwenye njia ya mkojo.

Epuka tabia ya kubana mkojo kwa muda mrefu, hakikisha unakwenda haja ndogo mara tu baada ya kupata hisia za kwenda haja.

Wanawake wanapaswa kubadili pedi mara kwa mara wakati wanapokuwa katika hedhi, angalau wabadili pedi mara 2-3 kwa siku.

Epuka kujisafisha ukeni kwa sabuni zenye kemikali, pia kupulizia marashi yoyote au kutumia pedi zenye kemikali za kukata harufu. Mambo haya yanaharibu kinga ya maeneo hayo.

Pale unapojisafisha baada ya kujisaidia anzia mbele kwenda nyuma kuepusha bakteria walio eneo la haja kubwa kuingia kwenye njia ya mkojo.

Boresha usafi wa vyooni, mwaga maji kabla ya kwenda haja ndogo na tumia maji safi na salama kujisafisha sehemu za siri. Weka mazingira ya mwili wako safi ili kuepuka maambukizi haya.

Epuka kujamiiana kinyume na maumbile kwani chanzo cha U.T.I ni bakteria wapatikanao njia ya haja kubwa.

Safisha uke kabla ya kushiriki tendo la ndoa na nenda haja ndogo baada ya kumaliza kujamiiana. Tumia mipira ya kujikinga yenye vilainishi au mafuta ili kupunguza kutokea kwa michubuko ukeni ambayo uwepo wake ni mazalia ya vimelea.

Vifaa vya kupanga uzazi kama vile diaphram, kondomu kavu na mafuta mazito ya kuangamiza mbegu za kiume huambatana na michubuko. Hakikisha unatumia vifaa hivi katika viwango sahihi.

Kausha maeneo ya ukeni kwa kitambaa safi na kikavu, vaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba ili zisaidie kunyonya majimaji kirahisi.

Vaa nguo za ndani zisizobana mwili, epuka kuvaa nguo ngumu zinazobana mwili na nguo za ndani zilizotengenezwa kwa nailoni au silk kwani hazinyonyi maji hivyo kutengeneza mazingira ya mazalia ya vimelea wanaosababisha U.T.I.

Oga kwa maji ambayo yanatiririka kama vile maji ya bomba la mvua, kwani kutiririka kwa kasi kwa maji mwilini huondosha uchafu na vimelea kirahisi.

Wajawazito ndio wako katika hatari ya kupata U.T.I, ni vizuri wao na wengineo kula lishe bora na kuzingatia kanuni za afya ikiwamo mlo uliosheheni protini, mboga za majani na matunda ili kujenga kinga imara ya mwili.

Wajawazito na wengineo wanatakiwa kutokurupuka kutumia dawa kwa ajili ya kutibu U.T.I kwani si dawa zote ni salama kwa wajawazito, mjulishe daktari anayekutibu kuwa una ujauzito ili akupe dawa ambayo itaendana na kipindi cha ujauzito.

Pale unapopata dalili au viashiria vya awali fika mapema katika huduma za afya zinazotambulika na serikali kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri.

Epuka matibabu yanayotolewa kienyeji mtaani na watu wasio na sifa stahiki za kutoa matibabu ya binadamu. Zingatia matibabu ya wataalam wa afya na usikatishe dozi.