Uzembe unavyochangia ubakaji, ulawiti kwa watoto

Iringa. Limekuwa kama jambo la kawaida kusikia watoto wakibakwa au kulawitiwa.

Hata pale zinapotolewa habari za watoto kufanyiwa ukatili huo, kwa kuwa jamii imezoea kusikia hayo mara kwa mara, huchukulia poa jambo hilo.

Wakati jamii ikizoea taarifa hizo, hali inazidi kuwa mbaya kwa watoto.

Matukio ya ubakaji na ulawiti yanaendelea kuripotiwa kila uchwao, huku wa kike na kiume, wote wakiwa wahanga.

Mkoa wa Iringa ni kati ya mikoa yenye matukio mengi ya ukatili kwa watoto, hasa ubakaji na ulawiti.

Mathlani, Desemba mwaka jana, dereva bajaj mmoja alishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kubaka na kulawiti watoto 15 katika matukio mbalimbali katika Manispaa ya Iringa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Bukumbi matukio hayo yalikuwa yakifanyika muda watoto walipokuwa wanarudi kutoka shuleni.

Hilo siyo tukio la kwanza kwa mtu mmoja kupatikana na tuhuma za kulawiti watoto zaidi ya mmoja.

Katika Mtaa wa Semtema, mwalimu mmoja naye aliwekwa mbaroni akituhumiwa kulawiti watoto 14 katika mitaa ya Semtema, Manispaa ya Iringa.

Lakini pia, mwaka 2021, mtoto wa miaka 14 aliwekwa mbaroni akituhumiwa kulawiti watoto wenzake 19.

Mtaalamu wa Saikolojia, John Paul anasema watoto hufanyiwa matukio hayo kwa nyakati tofauti na wazazi au walezi huja kustuka wakati hali imeshakuwa mbaya.

"Mzazi au mlezi hana habari, yupo bize na kazi zake kumbe mtoto anaharibiwa kila siku na kutishiwa asiseme. Unakuja kustuka katika watoto 19 walio lawitiwa wako yupo," anasema.

Kutoka na hali hiyo, Pendo Mwashota na Dk Philpo John, Wahadhiri na Watafiti kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wameamua kuja na majibu, nini chanzo cha matukio hayo?

"Tumegundua tatizo linaanzia kwenye familia zenyewe, huko ndiko chanzo kikuu cha awali kabisa cha ukatili huu kwa watoto," anasema Dk Philpo.

Anasema wamebaini sababu kumi ambazo ni mzizi wa matukio hayo, huku sababu hizo zote zikianzia ngazi ya familia.


Utafiti wenyewe

Dk Philpo anasema awali walianza kubainisha matukio ya ukatili kujua ikiwa familia zinahusika.

"Tukachagua shule tano ambazo tulikaa na watoto tukazungimza nao, walimu, wazazi, walezi na jamii yao. Tukaenda kituo kimoja cha yatima na tunafuatilia matukio yenyewe," anasema.

Anasema, baada ya kazi hiyo walipata sababu kumi zinazofanya watoto waendelee kufanyiwa ukatili huo bila huruma, huku chanzo cha zote kikiwa ni familia.


Sababu 10 za ongezeko la ubakaji, ulawiti

Mwashota anasema sababu ya kwanza ilikuwa ni uwepo wa familia tegemezi.

Anasema familia tegemezi ni zile zinazokusanya ndugu wengi kwa pamoja na kuishi nao huku kukiwa hakuna usimamizi mzuri wa wazazi au walezi.

"Unakuta baba, mama, mjomba, binamu, mtoto wa babu yake binamu wote wapo nyumbani na kuna watoto. Hakuna anayejali kuhusu wao na mwisho, ukatili unatokea," anasema.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swali anakiri kuwa kweli matukio mengi ya ubakaji na ulawiti, yanahusisha ndugu wa karibu.

"Hao ndugu, wanaume wanalala na watoto chumba kimoja. Unaamini ni mjomba wao kumbe mwisho anawafanyia ukatili," anasema.

Kulingana na watafiti hao, sababu ya pili waliyobaini ni malezi mabaya ndani ya familia.

Dk Philpo anasema wapo baadhi ya wazazi na walezi hawajali kuhusu maisha, mienendo na tabia za watoto wao.

"Unakuta mtoto yupo kibandaumiza anaangalia TV usiku, pengine mzazi ndiye amempa pesa au anajua kabisa mtoto hayupo nyumbani lakini hana habari," anasema Dk Philpo.

Anasema sababu nyingine waliyobaini ni imani za kishirikina.

Anasema wapo baadhi ya wazazi au walezi wanaamua kwenda kwa waganga wa jadi kutafuta utajiri na matokeo yake wanaambiwa wakabake au kulawiti watoto.

"Mtu akitoka huko na mganga amemwambia akibaka atatajirika, anaenda kufanya huo ukatili kwa mwanaye," anasema.

Aidha, Mwashota anasema kwenye utafiti wao walibaini matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yameendelea kuathiri watoto.

Anasema mzazi au mlezi anaweza kuwa anatumia mtandao kwa ajili yake bila kujali mwanaye anafuatilia na mwisho mtoto anatumbukia kwenye ukatili.

Mbali na sababu hizo, Dk Philpo anasema umaskini kwenye familia umechangia kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na ulawiti.

Anasema baadhi ya watoto waliowahi kufanyiwa ukatili huo wanatoka kwenye familia maskini.

"Umaskini ndani ya familia imekuwa chanzo kwa watoto kufanyiwa ukatili, umaskini huu umefanya watoto wakubali kuhongwa pipi, pesa ndogo na kufanyiwa ukatili huku wazazi wakiwa bize kutafuta maisha," anasema Dk Philpo.

Kwenye maeneo ya shule, Dk Philpo anasema wakati mwingine walimu imekuwa vigumu kufuatilia mienendo ya watoto kuhusu tabia zao.

Kuna tukio ambalo mtoto wa miaka 24, alikuwa akiwalawiti wenzake shuleni na mtoto huyo alijifunza kwenye jamii anayoishi.

"Uongozi wa shule unaofuatilia tabia na mienendo ya watoto rahisi kubaini matukio kama haya na kuyafuatilia," anasema Dk Philpo.

Ipo tabia ya familia kuiga maisha ya kisasa, jambo ambalo watafiti wanasema, pia linachangia kuwepo kwa kasi ya matukio ya ukatili.

Mbali na sababu hizo, Dk Philpo anasema afya ya akili imekuwa tatizo kubwa kwenye familia.

Anasema, matatizo ya afya ya akili yamekuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kuwepo kwa kasi ya ubakaji na ulawiti.


Maoni ya wazazi, walezi

Baadhi ya wazazi na walezi wanakiri kweli kuwa familia zimekuwa eneo lisilo salama kwa watoto.

"Wazazi tumekuwa bize kutafuta maisha na tunasahau kuwa watoto ndio maisha yetu. Unatafuta hela mchana na usiku, mtoto analawitiwa, matokeo yake itakuwa nini? Pesa zitamsaidia nani kama sio mtoto?" Anasema Jonas Mhelwa, mkazi wa Semtema.

Mkazi wa Mtwivila, Manispaa ya Iringa anasimulia kuwa siku moja alishangaa kuona mtu amelala chumba cha wanaye usiku, akiwa bila nguo.

"Tuna kibandaumiza cha mpira nje ya nyumba, mimi na mama yao tukiendelea kutazama mpira, kijana mlevi aliingia chumba cha watoto akalala," anasimulia na kuongeza;

"Inaonekana pombe zilifanya ashindwe kutimiza azma yake, mwisho akapigwa usingizi hadi tunamkuta. Nikagundua, uzembe wetu ndio chanzo. Kwanza kibandaumiza nyumbani, pili mpaka saa sita watoto huwa peke yao."

Anasema walichoamua kufanya ni mkewe kuwa na watoto, huku yeye akikaa kwenye kibanda ambacho yupo mbioni kuondoa nyumbani awake.

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile anasema lazima familia zirejee kwa Mungu ili pengo baina yao na malezi ya watoto lizibike.

"Familia zimrudie Mungu, ziwe na hofu ya Mungu, ziachane na dunia inayojaribu watoto, hakika zikifanya hivyo zitakuwa salama," anasema Gavile.

Mwenyekiti wa UWT Iringa Vijijini, Lena Hongoli anasema inawezekana kuokoa watoto kutoka kwenye wimbi la ubakaji na ulawiti ikiwa familia zitagundua kosa lilipoanzia.

"Mimi pia ni Mwenyekiti wa malezi na familia KKKT hapa Iringa, naona namna hali ilivyo mbaya. Kina mama turejee kwenye majukumu yetu kwenye malezi. Tumeacha ndiyo maana hali ni mbaya," anasema Hongoli.


Nini kifanyike?

Kulingana na watafiti hao, bado wanaendelea kufanya tafiti ili waje na matokeo yatakayosaidia kumalizika kwa tatizo.

"Tunakusanya mapendekezo na kufanya tathmini ili tukija kushauri kuwe na matokeo chanya moja kwa moja," anasema.

Hata hivyo, anasema ipo hatari ya matukio hayo kuendelea kushamiri ikiwa hakutakuwa na hatua za haraka za kutibu.

"Serikali ije na sera zitakazojikita kustawisha watoto, sera hizi ziingie moja kwa moja kwenye familia ili kuwalinda watoto," anasema Dk Philpo.