Vita ya beki tatu na mama mwenye nyumba inavyogeuka fursa mtandaoni

Vita ya beki tatu na mama mwenye nyumba inavyogeuka fursa mtandaoni

Muktasari:

  • Biashara nyingi zimehamia mitandaoni siku hizi, sasa majuzi nilikumbana na tangazo moja la kampuni ya ma-house girl huko mtandaoni ndiyo nikagundua kumbe ile vita tuliyoianzisha ya madada wa kazi dhidi ya wake zetu bado haijakwisha, mbichi kabisa.

Biashara nyingi zimehamia mitandaoni siku hizi, sasa majuzi nilikumbana na tangazo moja la kampuni ya ma-house girl huko mtandaoni ndiyo nikagundua kumbe ile vita tuliyoianzisha ya madada wa kazi dhidi ya wake zetu bado haijakwisha, mbichi kabisa.

Kila nikitazama sioni dalili ya vita hiyo kwisha zaidi ya kupamba moto kwa sababu kuna mambo hayajakaa sawa.

Tangazo nililoliona lilikuwa linasema; “Je, una shida ya dada wa kazi? Karibu tukupatie dada wa kazi mwenye ubora, weledi, uaminifu, mchapakazi na upendo. Pia tunahakikisha hatukuletei mke mweziyo, bali dada wa kazi na ndoa yako itabaki kuwa na amani. Tupigie kwa namba …”

Kwa wataalamu wa biashara wanaelewa. Ili biashara yako ifuatiliwe kwa umakini na wateja ni lazima iwe inajihusisha na kutatua tatizo fulani. Yaani kama kuna sehemu wana shida ya maji, ukienda kuchimba kisima au kuweka bomba, hapo utawakamata ile mbaya.

Kwa maantiki hiyo, ndiyo maana wanaotengeneza matangazo ya biashara huwa hawaimbi kuhusu biashara wanayouza, isipokuwa wanatengeneza matangazo yanayolielezea vizuri tatizo lako kisha namna ambavyo litatatuliwa ukitumia bidhaa yao.

Lakini wanaotengeneza matangazo mazuri wanajua hiyo pekee haitoshi. Wanajua kuna biashara nyingi huko nje zinazotatua tatizo wanalolitatua wao, kwa hiyo inahitaji utaje vitu vya ziada kuhusu biashara yako ili iwapiku wengine na ionekane dili kubwa zaidi.

Ndio hapo tunaporudi kwenye tangazo la ma-house girl wanajua kuna watu wanahitaji madada wa kazi na wanaweza kuwapata sehemu yoyote. Hata hivyo sio madada wa kazi wengi wana ubora, weledi, waaminifu, wachapakazi na wana upendo…kwa hiyo wakahakikisha unaona hilo kwenye tangazo lao.

Zaidi ni kwamba, wanajua kwa kiasi kikubwa hata madada wa kazi wachache wenye ubora, weledi, uaminifu, uchapakazi, upendo walishindwa kitu kimoja, kuhakikisha hawawi wake wenza.

Kuna stori nyingi mtaani zinaeleza jinsi nyumba zilivyovunjwa na madada wa kazi. Inaweza kuwa kwa makosa ya dada wa kazi au ya baba, lakini mwisho wa siku nyumba zinavunjika.

Dada wa kazi anakuja nyumbani kama mlugaluga, mama mwenye nyumba hana wasiwasi naye, anahisi anamjua sana mume wake. Kwamba mume wake anapenda vitu vizuri, wanawake wa mjini wanaojua kupaka make up na kujitwisha mawigi kama jogoo kichwani, wanawake wanaojua kupendeza.

Lakini mwisho wa mchezo uhakika wa mama kwa mumewe unamuingiza chaka, vitu ambavyo anadhani haviwezi kumuangusha mwenyewe vinamuangusha sio tu mumewe, bali nyumba nzima. Anakuja kustuka ameshachelewa, dada wa kazi ameshakuwa mke mwenzake.

Unaweza kusema wanaume tumerogwa na kwa sababu hiyo… wenye kampuni za ma-house girl wameamua kucheza na udhaifu wetu kuwahakikishia wateja kwamba wao wanakuletea dada wa kazi, sio mke mwenzako.