Yafahamu mambo kumi yanayodumisha furaha katika ndoa – 2

Muktasari:

Maelezo yako yametugusa sana mimi na mke wangu. Ndoa yetu imepitia katika vipindi vya kubadilikabadilika. Mara inakuwa nzuri mara inakuwa mbaya. Kuna wakati ilifikia katika kilele cha misukosuko hadi ikaonekana kama hakuna suluhisho bali kuachana tu ingawa tayari tulikuwa na watoto watatu.

Wiki iliyopita nilianza kuandika makala kuhusu mambo kumi ambayo hufanya furaha kudumu katika ndoa. Mmoja wa wasomaji ameniandikia maneno haya. “Makala yako imetoa maoni na vidokezo muhimu kwa wanandoa.

Maelezo yako yametugusa sana mimi na mke wangu. Ndoa yetu imepitia katika vipindi vya kubadilikabadilika. Mara inakuwa nzuri mara inakuwa mbaya. Kuna wakati ilifikia katika kilele cha misukosuko hadi ikaonekana kama hakuna suluhisho bali kuachana tu ingawa tayari tulikuwa na watoto watatu.

Mungu bariki, tuliweza kukumbuka yale yote tuliyowahi kuyapitia kutokana na uhusiano wetu na hata tukajiuliza kilichotupelekea hadi tukamua kuoana. Kutokana na ustahimilivu na juhudi zetu za pamoja tulizoamua kuchukua tukafanikiwa kuinusuru ndoa yetu. Tukavuka mitihani na changamoto na kuibuka kama wanandoa wenye ujasiri na busara uliotuwezesha kudumisha furaha na mapenzi katika ndoa.”

Wiki iliyopita tulitaja mambo manne, leo tunaendelea na la tano hadi kumi kama ifuatavyo.

Kutumia vyema fursa za ajira

Katika ulimwengu wa siku hizi ni jambo la kawaida kwa mume na mke wote kufanya kazi. Mume na mke hawana budi kuitumia vyema fursa hii wanayopata ili kukabiliana na ukali wa maisha. Wanandoa wanaofanya kazi waweke uwiano mzuri kati ya majukumu ya kazini na ya nyumbani. Kila moja amuunge mkono mwenzake kwa mawazo na ushauri kuhusiana na kazi yake. Vile vile kila mmoja amsaidie mwenzake kwa kumuhamasisha na kumpatia ushauri utakaomsaidia kutumia vyema zaidi vipaji, uwezo na stadi katika kazi yake. Muhimu zaidi ni mwanamume kumsaidia mkewe kutambua ndoto na shabaha zake katika kazi na namna ya kuzifikia.

Ushirikiano katika masuala ya fedha

Kuna wanandoa ambao hutumia mtindo wa umiliki na utumiaji wa fedha ambao husababisha migogoro katika ndoa yao . Hawa ni wale ambao aidha, mume hufanya mambo yote yanayohusiana na fedha na kumfanya mwanamke asijue lolote kuhusu fedha ndani ya kaya au mume kumkabidhi mkewe fedha zote za matumizi na kukwepa uwajibikaji na kubaki akimlaumu kila anapoona hazitoshelezi mahitaji.

Njia sahihi ni kuhakikisha kuwa kila mwanandoa ana fursa ya usimamizi wa matumizi bora ya kipato cha familia. Hususan, ni vyema zaidi mwanamke asifichwe ila aelewe hali halisi ya kipato, matumizi, bajeti, akiba na malengo yanayotarajiwa kufikiwa au kutekelezwa. Hali hi humfanya aweze kujiamini na kutokuwa na mashaka au wasiwasi kuhusu uwezo wa kifedha na familia. Vile vile itamwezesha kuepusha matumizi yasiyo ya lazima au yasiyoendana na kiwango cha mapato yao. Ni vema zaidi wanandoa wote wawili kujadiliana na kuamua pamoja masuala yote muhimu ya mipango ya maendeleo ya familia yao.

Kushiriki pamoja katika burudani

Aghlabu sana wanandoa wawili kuwa na upenzi wa mvuto unaofanana katika mambo ya burudani. Mmoja anaweza kuwa anapendelea ngoma na dansi na mwingine anapendelea shughuli za riadha na michezo. Vilevile moja anaweza kuwa anapendelea kutoka na kujumuika na watu wengine na mwingine akawa mkinya sana anayependelea kuwa mpweke badala ya kuchanganyika na watu.

Wanapokuwa na tofauti za namna hii isiwe sababu ya mwanamke kuachwa nyumbani wakati wote, inabidi kila wanapotaka kutoka waafikiane ili wawe na ridhaa na shughuli ya burudani wanayotaka kuiendea. Kutoka nyumbani na kwenda kwenye burudani mara kwa mara huongeza furaha katika ndoa.

Kufuata madili yenye ridhaa

Mume na mke wanapooana huwa wameamua kila moja kuiacha familia yake ili waishi pamoja na kuanzisha familia yao. Kila moja huingia katika ndoa akiwa na imani na itikadi alizozizoea katika familia yake. Baadhi ya itikadi nyeti zaidi huwa zile za jadi.

Wanandoa kama watu waliamua kuishi pamoja maisha yao yote wanatakiwa kuwa na maadili wanayoyaridhia wao wote lazima wawe makini katika kufahamishana, kujadiliana na kuamua madili ambayo kila mmoja wao atayamini na kuyakubali kwa dhati bila shuruti au kero. Licha ya kukidhi matakwa na matarajio yao, itabidi wahakikishe wana mwenendo na tabia zinazokubalika katika jamii. Iwapo mwanandoa mmoja ataona mwenzake anayumba, itambidi aitambue sababu na kufanya ushawishi utakaomhamasisha ajirekebishe.

Kuepuka jazba

Jazba ni hisia ya mawazo ambayo huweza kumshika mtu ghafla na kumfanya ajisahau nafsi yake na kufanya jambo ambalo badaaye hulijutia. Kiwango kikubwa cha wanawake hushikwa na jazba kuliko wanaume. Mara nyingi ugomvi hutokea katika ndoa kutokana na jazba. Mume anapaswa kuepuka jazba zaidi kuliko mwanamke. Jambo muhimu kwa kila mwanandoa ni kuwa mvumilivu na kuishinda jazba. Kwa kufanya hivyo, kila wakati mwenziwe atakapopatwa na jazba ataweza kumtendea kwa wema na hivyo kuimarisha mapenzi yao.

Kujenga mazingira yasiyo na unyanyasaji

Mahali fulani niliwahi kuandika kuwa katika ndoa za siku hizi haifai kuwa na mfumo wa muamrishaji na mtekelezaji. Yani mume kazi yake ni kutoa amri na mke kazi yake ni kupokea amri na kuzitekeleza. Mume wa leo akitaka kupata mwitikio wa upendo wa dhati kutoka kwa mkewe hanabudi kuepuka mawazo yaliyopitwa na wakati kuwa manamke hana hadhi sawa na mwanamume.