Zawadi hewa janga kwa maharusi, jamii

Muktasari:
- Sadick Manemba alikumbana na changamoto kubwa siku ya harusi yake baada ya kupokea hundi batili na kumfanya akabiliwe na madeni makubwa kutoka kwa watu waliomkopesha fedha kugharimia sherehe, na hali hii ilimfanya asifurahie kipindi chake cha fungate.
Dar es Salaam. Kamwe siwezi kusahau kilichotokea siku ya harusi yangu, kamati yangu ilitangaza kunipatia kiasi cha fedha kama zawadi kwa kunikabidhi hundi ambayo baadaye nilikuja kugundua si halali. Hundi ile ilifanya maisha ya siku za mwanzo za ndoa yangu kuwa shubiri.
Hiyo ni kauli ya Sadick Manemba, akiwa ni miongoni mwa maharusi waliokutana na zawadi ya magumashi iliyofanya maisha ya siku za mwanzo ya ndoa yake yageuke shubiri badala ya furaha.
Hali hiyo ilitokana na sehemu kubwa ya waliokuwa wanamdai fedha alizokopa kugharimia harusi kushinikiza walipwe kwa kuwa wameona amepokea hundi inayoonesha kuwa na kiwango kikubwa cha fedha.
Kwa mujibu wa Manemba, hundi hiyo ilifuta sehemu kubwa ya mawazo, kwani wakati anaipokea tayari alishaanza kupanga mgawanyo wa fedha hizo kumalizia madeni.
“Unajua sisi watu wa kipato cha chini mara nyingi tunapofanya hizi sherehe unajikuta unaingia kwenye madeni kuhakikisha mambo yanaenda sawa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu, hadi sherehe inafanyika nilikuwa na madeni kadhaa, sasa ilipofika wakati wa zawadi wanakamati wakaja na zawadi iliyonipa matumaini mapya.
“Walikuja na mfano wa hundi iliyoandikwa zaidi ya milioni tatu, kwa kuwa sikuwa na taarifa ya zawadi hiyo nilifurahi, nikiamini labda kamati yangu imeamua kunisuprise, kumbe haikuwa hivyo. Tatizo likaanza sasa kila aliyekuwa ananidai aliona deni lake linaenda kulipwa, hata mke wangu alifurahia akidhani tumetunzwa fedha hivyo maisha yetu ya fungate yatakuwa mazuri,” anasema Manemba na kuongeza:
“Siku nagundua si halali niliishiwa nguvu, kwa sababu changamoto ilikuwa kuukubali ukweli katikati ya presha. Sitasahau, niliwaza nawajibu nini wanaonidai, kila kitu kilikuwa vurugu,” anasema.
Huo ukawa mwanzo wa maisha ya kudaiwa kwa karaha kiasi kwamba hakufurahia muda wake wa fungate, kila kukicha akipata simu za wanaomdai na hakuna aliyemwelewa hata alipowaambia hana fedha, wengi walimkumbusha hundi aliyopokea siku ya harusi.
“Ilikuwa mshikemshike kumwaminisha mtu kwamba ile hundi ilikuwa feki, ilikuwa ngumu sana, mmoja kati ya waliokuwa wananidai aliamua kufunga safari hadi nyumbani kuthibitisha na bado hakuamini, kiukweli kile kitendo kiliniletea shida mno,” Sadick Manemba.
Hali ngumu nyingine iliyomtokea Manemba kutokana na hundi hiyo, ni pale ndugu zake walipotaka sehemu ya fedha kulipa usafiri uliowapeleka ukumbini siku tatu baada ya sherehe.
“Niliwaambia sina fedha, hakuna aliyeamini, kila mmoja anakumbushia hundi niliyopokea nina hicho kiasi cha fedha kilichoandikwa kwenye hundi, ninachotakiwa kufanya ni kwenda benki kuwatolea. Wengine ililazimika tupishane kauli maana nilivurugwa pia,” anasema Mnemba.
Mwingine mwenye ushuhuda wa hilo ni Ayubu Motika (si jina halisi) ambaye siku ya harusi yake aliahidiwa zawadi ya ng’ombe wanne, shamba la ekari nne, kiwanja na samani za nyumbani, vitu ambavyo hajavipata hadi sasa ndoa yake ikiwa na mwaka mmoja.
“Nilipatwa na furaha ya aina yake kusikia ndugu zangu wameamua kunizawadia zawadi za muhimu kiasi hicho, kichwani mwangu nikawa nafikiri jinsi ya kuanza maisha mapya ya ufugaji huku nikijipanga kujenga kwenye kiwanja nilichopewa.”
Hata hivyo mambo hayakuwa kama alivyotarajia, siku kadhaa baada ya sherehe kupita alianza kufuatilia zawadi alizoahidiwa, kote alikoulizia hakupata majibu ya kueleweka.
Ayubu anasema kitendo kinachofanyika kudanganya maharusi ukumbini wakati mwingine husababisha migororo baada ya shughuli kuisha kwa mwenza kumuona si mwaminifu, akidhani huenda kazipokea ahadi zile na kunufaika nazo peke yake.
"Mfano mke wangu ndugu zake walimuahidi samani mbalimbali za ndani wakieleza kwamba vipo kwa fundi, lakini shughuli ilipoisha hata yeye nilipomuuliza hakuwa na majibu zaidi ya kuniambia vitakuja, ni zaidi ya mwaka sasa hakuna kitu,"anasema Ayubu.
Simulizi za wawili hawa zinakuja kufuatia kuwepo kwa matukio ya kamati za harusi kutoa zawadi mbalimbali, ikiwemo hundi ambazo zinaelezwa kutokuwa na uhalisia.
Kupitia mitandao ya kijamii zimekuwepo video zinazowaonesha maharusi wakipokea zawadi mbalimbali kutoka wanakamati, wazazi na wageni waalikwa ambazo zimezua mjadala.
Zawadi hizo ni pamoja na hundi za kiasi kikubwa cha fedha, funguo za magari, ahadi za nyumba, viwanja, mashamba na vifaa vingine vya thamani.
Video hizi, hasa zile zinazohusisha hela zimekuwa zikiibua mijadala, kukiwepo watu wanaoeleza kuwa siku hizi upo uwezekano wa kutengeneza hundi zisizo halisi na ndizo mara nyingi huwa zinatumika kutolewa kwenye sherehe.
Mwananchi limezungumza na mmoja wa washereshaji mahiri ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliyekiri kuwepo kwa wimbi la watoa zawadi hewa kwenye harusi na mara nyingi linaonekana zinapotolewa hundi.
Anasema mara nyingi hilo linafanywa na watu wanaotaka kuonesha ufahari kwamba wamewakabidhi maharusi kiasi kikubwa cha fedha, wakati uhalisia hauko hivyo.
“Hili suala lipo tena kwa kiasi kikubwa tu, sisi washereheshaji huwa tunafahamu kwa kuangalia thamani ya sherehe. Kuna sherehe unafika unaona bajeti yake ni ndogo halafu zawadi ya kamati inakuwa kubwa, hapo unajua kuna usanii umefanyika.
“Mara nyingi hizi hundi zinakuwaga siyo halisi, hasa zinazotaja kiasi kikubwa cha fedha, haiwezekani sherehe yenye bajeti ya milioni 15 hadi 20 halafu zawadi ikatolewa milioni 30. Ingawa zipo hundi nyingine zinakuja zenyewe kabisa za benki ile karatasi ndogo, ambazo hizi kwa kiasi kikubwa fedha zinaendana na uhalisia,” anasema.
Licha ya kuwa hulazimika kuchagiza zawadi zinapotolewa, hili si suala linalomvutia mshereheshaji huyu, kwa kile alichoeleza kuwa ni chanzo cha migogoro na inaweza kuwaweka maharusi katika wakati mgumu.
“Binafsi huwa sivutiwi na huu utaratibu kwa sababu unaweza kusababisha migogoro na hata kuwapa msongo wa mawazo maharusi. Ikitokea dharura yoyote siku chache baada ya harusi, ni rahisi kwa ndugu kurudi kwa maharusi wakiamini kuna fedha imeingia, lakini kumbe ilikuwa hewa.
“Na ingekuwa uwezo wangu, haya mambo yanayohusu fedha hayana umuhimu wa kuoneshwa hadharani, inawezekana kabisa kamati ikasema imewapatia zawadi maharusi wao na ikabaki kuwa siri na kama hundi, basi ikabidhiwe kwenye bahasha, lakini si hivi inavyofanyika kwenye sherehe nyingi,” anasema mshereheshaji huyo.
Akizungumzia hilo, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude anasema utamaduni huo unaoonekana kushika kasi hauishii kutengeneza migogoro kwa wahusika na familia tu, bali pia unatengeneza matabaka kwenye jamii.
Anasema katika jamii yenye mizizi ya ujamaa haipendezi kuonesha hadharani kwamba kuna watu wana fedha nyingi kupita kiasi, ilhali kuna wengine hawamudu hata mlo wa siku moja.
“Hili ni tatizo la kijamii na kama litafumbiwa macho basi tujiandae kwa madhara makubwa zaidi, haya maonesho yanayofanyika kwenye sherehe yanaweza kuleta athari kubwa, ikiwemo kujenga matabaka.
“Kwa hali yetu Tanzania, hakuna sababu ya kuonesha kwamba wewe una fedha nyingi kuliko wengine, tena hadharani, inaweza kuwasababishia hata changamoto za kiusalama walengwa kwa sababu watawindwa wakionekana wana fedha, pia inahamasisha watu kufanya uhalifu,” anasema na kuongeza:
“Inawezekana mtu hana uwezo wa kuwa na sherehe ya aina hiyo au kamati ya kumwezesha sherehe yake kujadiliwa, hapa anaweza kushawishika kufanya vitendo vya uhalifu, ikiwemo kujiingiza kwenye biashara haramu ili atafute fedha za kufanya harusi ya kukata na shoka au kujiweka karibu na wahalifu waweze kumsaidia kujenga heshima.”
Mkude anasema inapofikia hatua hiyo, ni hatari kwa jamii kwa kuwa watu watakuwa wanafanya vyovyote wanavyojisikia ili kutengeneza heshima na kutafuta kujadiliwa wanapokuwa na matukio yanayokusanya watu wengi.
Mtazamo wa kisaikolojia
Mwanasaikolojia, Christian Bwaya anasema kutoa ahadi hewa kwenye harusi kunachangiwa na mambo mengi, kubwa ikiwa ni matarajio ya jamii kwa watu kulingana na hadhi zao.
“Unapokuwa na nafasi fulani kwenye famii, au unaonekana kuwa na uwezo mzuri kifedha, watu wanatarajia utatoa zaidi.
“Wakati mwingine matarajio haya hayalingani na uhalisia wako. Kuliko kudhalilika na kuonekana una uwezo, mtu anaona ni bora atoe ahadi hewa kulinda hadhi yake”.
Kwa upande mwingine, tumeanza kuwa na shughuli za harusi zenye gharama kubwa kwa kutegemea michango ya watu.
“Tunataka mambo makubwa wakati hatuna uwezo. Siku hizi si ajabu kupewa kadi yenye kiwango kikubwa na unalazimika kutoa,” anasema.
Bwaya anasema katika mazingira kama hayo ya kupewa shinikizo la kutoa, unapotakiwa tena kutoa zawadi, ndiyo yanakuja hayo mambo ya zawadi hewa.