King Kiba, Zari katika vita dhidi ya corona

Wakati hatua zikiendelea kuchukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga la corona wasanii na watu maarufu wameonyesha ushiriki wao katika vita hiyo.

Katika kundi hilo wamo Ali Kiba au King Kiba na Zarina Hassan au Zari Boss Lady ambao ameamua kutumia mitandao ya kijamii kutoa somo dhidi ya ugonjwa wa corona au Covid-19

Wakati watu hao wakitumia umaarufu wao hali ya maambukizi inazidi kuwa mbaya, hadi jana jioni idadi ya watu wenye maambukizi ya virusi vya corona duniani kote ilifikia 1.6 milioni.

Kupitia mitandao ya kijamii, King Kiba mwenye wafuasi 5.2 milioni na Zari mwenye wafuasi 7.4 milioni wamejitoa katika vita dhidi ya gonjwa hilo wakiwa vinara kuwasisitizia watu kuzingatia maelekezo ya wataalamu na suala zima la usafi wa mikono ili kuzuia maambukizi mapya.

Mfalme wa Bongofleva, King Kiba kupitia mtandao wa Instagram, ametenga muda kwa ajili ya kuzungumza na watu 5.2 milioni kwenye ukurasa wake kuhusu maradhi hayo.

Kiba alisisitiza watu kuondoa tofauti zao katika kipindi hiki na kuungana pamoja katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao umevuruga mfumo mzima wa maisha.

“Tunatakiwa kuwa makini na kufuata maelekezo ya wataalamu. Lazima wote tuwe kitu kimoja kukabiliana na ugonjwa huu. Serikali yetu inajitahidi ila corona inahitaji elimu ya ziada.

“Kuna watu hawana elimu ya kutosha kuhusu hili na upotoshaji umekuwa mwingi, athari ya corona sio kukaa ndani tu kwani hata sisi wasanii imetuathiri maana hakuna shoo na mwisho wa siku tunaangalia usalama kwanza, pesa itatafutwa,” alisema King Kiba.

Alifafanua kwa sasa watu wajikite kwenye kuhakikisha afya za wote wanaowazunguka zinakuwa salama. Msanii huyo pia alieleza kuwa kutokana na watu kugubikwa na taarifa za ugonjwa kwa muda mrefu ameamua kutoa wimbo wa ‘Dodo’ ili kuwafariji katika kipindi hiki ambacho wengi wako nyumbani.

Kwa upande wake, Boss Lady ambaye pia ni mjasiriamali na mzazi mwenzake na msanii Diamond Platnumz, alivunja ukimya na kuzungumza na watu 7.4 milioni wanaomfuatilia katika ukurasa wake wa Instagram, kwa kuwahimiza kutotoka nyumbani kama hawana jambo la maana. “Kutulia nyumbani ni njia mojawapo ya kupunguza maambukizi mapya.

“Ukiambiwa kaa nyumbani ni vyema ukatii, kinyume na hapo hii corona itaendelea kuwepo hata mwaka mzima ni heri kuvumilia kwa muda mfupi ili tuweze kurudi kwenye maisha yetu ya kawaida,” alisema Zari.

Mwanamuziki Nandy yeye alitumia Instalive kuzungumza na watu 3.1 milioni wanaomfuatilia katika ukurasa wake wa Instagram kwa kuwasisitiza kuzingatia usafi wa mikono na kuepuka mikusanyiko ili kujiondoa kwenye hatari ya kupata maambukizi.

Ujumbe wa aina hiyo pia ulitolewa kwa watu 1.1 milioni wanaomfuatilia msanii Dully Sykes ambaye kwa upande wake aliweka msisitizo kwa watu wenye magonjwa mengine kuwa makini zaidi ili wasiambukizwe corona.

“Nasikia ukiwa na ugonjwa mwingine ukipata corona ndiyo changamoto zaidi, sasa nawasisitiza kama unajijua una matatizo yako ongeza umakini yaani ni bora uonekane mwoga ila wewe mwenyewe unajua unafanya hivyo kwa afya yako,” alisema Dully.