Kutajwa Grammy ni mtego mwingine

Ni mtego au kipimo kingine kwa muziki wa Bongofleva kufuatia waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy kuongeza kipengele kipya 'Best African Music Perfomance' ambacho kitahusisha aina mbalimbali za muziki kutoka Afrika. Kipengele hicho kitajumuisha muziki kama Bongofleva, Afrobeat, Afro-fusion, Afro pop, Alte, Amapiano, Genge, Kizomba, Chimurenga, High Life, Fuji n.k.

Baadhi ya wasanii wa Afrika waliowahi kushinda Grammy ni Angelique Kidjo (Benin), Ladysmith Black Mambazo, The Soweto Gospel Choir na Black Coffee (Afrika Kusini), Burna Boy, Wizkid na Tems (Nigeria) n.k. Recording Academy imeonyesha nia ya muziki wa Afrika, katika mahojiano yao na Diamond Platnumz Oktoba 2020, walisema staa huyo wa Bongofleva amebadilisha taswira ya muziki wa Afrika Mashariki.

Hata hivyo, fursa hiyo inakuja wakati wasanii wa Bongofleva wakionekana kutofanya vizuri zaidi kimataifa ukilinganisha na mataifa kama Nigeria na Afrika Kusini. Majukwaa kama BET na Billboard ambayo yanasifika duniani kwa kutangaza muziki, yameshatoa fursa kwa muziki wa Afrika, lakini Bongofleva bado haijafanya vizuri, hii ndiyo sababu fursa hii ya Grammy inaonekana kama mtego au kipimo kingine.

Mwaka 2010 waandaaji wa tuzo za BET walitambulisha kipengele kipya 'Best International Act; Africa' na 2018 kikabadilishwa na kuwa 'Best International Act', kwa ajili ya wasanii waliopo nje ya Marekani.

Lengo ni kuwatuza wasanii wa Afrika na baadaye wakaongeza wasanii wa mabara mengine, tangu wakati huo Bongofleva haijashinda licha ya kuwania mara tatu (Diamond) 2014, 2016 na 2021.

Huku wasanii wa Nigeria wakishinda tangu mwaka 2011 hadi 2014, wakarejea tena mwaka 2017 hadi 2021, huku Ghana ikishinda mwaka 2015 na Afrika Kusini mwaka 2016. Wakati wasanii wa Afrika wakishindwa kuingiza nyimbo zao kwenye chati kubwa duniani za Billboard Hot 100, Billboard 200 n.k, Machi 2022 Billboard walianzisha chati kwa ajili ya muziki wa Afrika, Billboard U.S Afrobeats Songs.

Hata hivyo, tangu wakati huo hakuna wimbo hata mmoja wa Bongofleva uliochomoza katika chati hizo. Akizungumzia hatua hiyo ya Grammy, Rapa Wakazi alisema bado kuna safari ndefu kufikia nchi ya ahadi, Bongofleva kuwekwa kwenye orodha haimaanishi ndio imetoboa, wasanii watahitaji kutoa kazi kali.

"Bado watashindanishwa na Wanigeria na wengine Afrika, bado watatakiwa kulipa Dola100 (Sh240,000) ili kuwasilisha kazi zao na kujadiliwa, huku wasaniii wetu huwa wanasema kuomba tuzo sio, wanataka wachaguliwe tu," anasema Wakazi.