KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kusoma, kusoma tena ni maisha ya mwandishi wa habari

Muktasari:

Kusoma ili kupata kipya. Kujikumbusha ili kutosahau. Kuuliza ili kupata nyongeza ya maarifa. Kufukua zaidi ili kujaza hazina ya maarifa, stadi na mbinu. Kutafuta kubaki hai kitaaluma.

Kwa mwandishi wa habari, darasa halifungwi. Maktaba hazijui kUfuli. Wanafunzi hawaendi likizo. Walimu hawachoki. Kuuliza na kujibiwa ndiyo mtindo wa maisha. Kusoma ni kama kawa!

Kusoma ili kupata kipya. Kujikumbusha ili kutosahau. Kuuliza ili kupata nyongeza ya maarifa. Kufukua zaidi ili kujaza hazina ya maarifa, stadi na mbinu. Kutafuta kubaki hai kitaaluma.

Desemba 2016 ulikuwa mwezi wa kusaidia au kuwezesha waadishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited (MCL) kujiandaa kwa kazi nyingi na bora kwa mwaka 2017.

Safari hii, aliyeongoza maandalizi ya waandishi alikuwa Meneja Uhusiano wa MCL. Katikati ya Desemba, kabla wengi hawajatawanyika kwenda “kula sikukuu,” alichomoa andishi muhimu na kumkabidhi kila mwandishi.

Ilikuwa hivi: Unapokea andishi. Unaweka saini kuonyesha umelipata. Unaondoka nalo. Unatakiwa kulisoma kwa makini na kutumia maudhui yake kuandaa habari kwa kuzingatia vigezo na masharti.

Andishi hili ni orodha ya maelekezo, na wakati huohuo vigezo vya kupima kazi ya mwandishi ya kuandika na kuhariri kile anachotaka kiwe habari.

Orodha hii ni muhimu kwa mwandishi. Anaweza kuitumia kujiuliza maswali, kujitafiti na kujitathimini. Ni orodha hii ambayo Meneja Uhusiano wa MCL aligawia waandishi ili kila mmoja awe na maelekezo sawa juu ya kutafuta taarifa na kuzihariri ili ziwe habari.

Kugawiwa kwa maelekezo na tathmini wakati wa sikukuu za mwisho na mwanzo wa mwaka; kulilenga kuwaambia waandishi wa habari kutotopea katika sherehe na kujisahau; bali kubaki kazini kifikra na kupima kazi za akili na mikono yao.

Hebu tuangalie yaliyo kwenye orodha waliyokabidhiwa waandishi wa habari. Hapa hatutafuata mtiririko wa namba. Tutakwenda kwa kuopoa.

Andishi linataka mwandishi ajiulize iwapo taarifa alizonazo zina uzito na thamani ya kuwa habari. Akijiridhisha basi aendelee kukusanya taarifa na kuandaa habari. Je, kile ambacho mwandishi ameandika na kinaitwa habari, kinajibu maswali yote muhimu – nini kilichopo au kimetokea, kuhusu nani au nini, lini, wapi, kwanini na vipi?

Andishi linataka uonyeshe umuhimu wa unachoandika na kutoa majibu kwa maswali makuu ya kimuktadha; kwa mfano juu ya wahusika wakuu, wanaonufaika, wasionufaika na mwelekeo wa unachoripoti.

Mwandishi anatakiwa kuhakikisha anachoandika kimo katika muktadha maalumu na historia yake inaeleweka ili wasomaji waweze kuunganisha matukio hata kutabiri yafuatayo.

Yote haya yanamhusu mwandishi na msanifu wa habari. Iwapo kuna ambayo mwandishi hakuweka; basi msanifu aone hivyo na ama ayaweke au amwagize mwandishi ayaweke; au andishi liwekwe kando kusubiri kupatikana kwa taarifa muhimu za kulifanya kuwa habari.

Orodha ya maelekezo na vigezo inauliza iwapo umeweka taarifa zote za kuthibitisha unachoandika; inauliza iwapo umeweka orodha ya vyanzo vyako vya taarifa – watu au vidhibiti na iwapo umejitahidi kuuliza wahusika au wadau wote katika suala unaloripoti.

Kwa miaka mingi kumekuwa na tatizo la waandishi kusema na kuamini kuwa kuna pande mbili katika kila kitu; kila suala. Hii siyo kweli. Wala hakuna pande nne “kama za dunia.”

Kila suala lina pande nyingi kadri anayetafuta taarifa anavyochimba. Mume aliyegombana na mke wake, siyo pekee wanaohusika katika ugomvi.

Kuna jirani aliyewaamua; mpitanjia aliyeshuhudia ugomvi ulivyoanza; mtoto anayekumbuka ugomvi ulianza jana au juzi; mjumbe anayekumbuka waliishafika mbele yake katika ofisi ya mtaa na mmoja wao akakiri kosa; majirani ambao hukatishwa usingizi kwa kelele za piga-nikupige na wengine.

Haitoshi kuuliza watu wawili na kuweka mikono mfukoni kwamba kazi imemalizika. Kuna pande nyingi.

Orodha ya maelekezo na vigezo ambayo ni kumbukizi maalum, ni moja ya miongozo kwa vyombo vya habari vilivyo chini ya Nation Media Group (NMG) ikiwemo MC.

Kumbukizi linauliza: Umetaja vyanzo vyako vya taarifa ili unachoandika kiweze kueleweka na kuthaminika? Umeelekeza habari yako kwa hadhira maalum na siyo jumlajumla na bila lengo? Wasomaji wako hawatakuwa na maswali muhimu ambayo hukujibu? Je, unachoandika ni cha kweli? Unakiandika kwa usahihi? Unaeleweka - lugha? Umesoma kazi yako na kuisahihisha kabla ya kuipeleka mbele ili iwe habari?

Mwandishi ni Mhariri wa Jamii wa vyombo vya habari vya Mwananchi Communications Limited wachapishaji wa magazeti ya The Citizen, Mwanaspoti na hili. Kwa maswali na hoja juu ya vyombo hivyo, wasiliana naye kwa simu: 0713614872 au 0763670229; e-mail: [email protected] au [email protected]