MAARIFA: Maajabu ya mmea wa Azolla katika kilimo na ufugaji

Muktasari:

Wafugaji nao wana kilio chao tena cha muda mrefu. Hawa wanalilia uhaba wa malisho na ndiyo maana katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakikwaruzana na wakulima.

Ukizungumza na wakulima wengi nchini, hawatasita kukutajia kero wanazopata katika upatikanaji wa pembejeo bora hasa mbolea.

Kero hiyo ni sehemu ya kilio chao cha muda mrefu.

Wafugaji nao wana kilio chao tena cha muda mrefu. Hawa wanalilia uhaba wa malisho na ndiyo maana katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakikwaruzana na wakulima.

Mtafiti wa masuala ya kilimo kutoka Kampuni ya Agriculture Media, Rafael Majivu ana ufumbuzi wa kufuta vilio hivi. Ufumbuzi huo ni mmea unaoitwa Azolla. Baada ya utafiti wa muda mrefu anasema wakulima na wafugaji, hawana budi kucheka.

Akizungumza katika semina ya fursa za kilimo cha kibiashara iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) iliyofanyika hivi karibuni alielezea faida za mmea huu unaomea kwenye madimbwi ya maji na mabwawa.

Azolla ni mbolea katika kilimo lakini pia ni chakula kwa mifugo na binadamu vilevile. Anasema kwa kutumia kiasi cha kutosha cha Azolla na kukiweka kwenye udongo wa shamba au bustani, mkulima atakuwa ameipatia mimea yake virutubisho vya kutosha.

Kuhusu mifugo, anasema: “Azolla ina virutubisho vyote vinavyohitajika na kufaa kwa chakula cha nguruwe, ng’ombe, samaki, kuku, sungura na wanyama wengineo.

Mmea huu pia husafisha maji ya bahari na kufaa kwa kunywa pamoja na kutakatisha hewa kwa kuondoa uchafu na hewa ukaa.”

Pia, anasema mmea huo unatumiwa baadhi ya kampuni za kimataifa kutengenezea mafuta ya magari na vilainishi vya mitambo. Matumizi mengine ni uzalishaji wa mafuta ya ndege na dawa za hospitali.

Mmoja wa wawashiriki wa semina hiyo, Atile Mputa, anasema hakuwa anafahamu faida za mmea huo, ingawa amekuwa akiuona kwa muda mrefu.

“Kando ya ziwa na hata kwenye mashamba ya mpunga mmea huu ni kawaida kuukuta. Hatujawahi kuutumia kama mbolea wala kusafisha maji. Ila kwa elimu hii nadhani mtazamo wangu umebadilika kuanzia leo,” anasema Mputa anayetokea Kyela jirani na mwambao wa Ziwa Nyasa.

Majivu anaeleza kuwa mmea huo pia ni chanzo kizuri cha nishati ya bayogasi inayoweza kutumika ya majumbani na viwandani, huku pia ukitoa malighafi ya kutengeneza bidhaa za plastiki.

Ili kuongeza tija, Majivu anasema mmea huo unaweza ukaoteshwa na kutumiwa kwa mpangilio mzuri kwa uzalishaji wa shamba la mifugo au mazao ya kilimo na kuongeza ufanisi kwa eneo linalotumika kwa kila mkulima.

“Ndani ya siku mbili mpaka tatu, Azolla hujizalisha mara tatu mpaka nne. Baada ya muda huo una uwezo wa kuendelea kuvuna kila siku na usiimalize kwenye bwawa ulilonalo wakati ukiboresha mbolea ya shamba lako au chakula cha mifugo yako,” anaeleza.

Kwa mtafiti huyu, mmea wa Azolla ni neema ya kujivunia kwa Watanzania kwa kuwa kama uwekezaji mkubwa utafanyika, Taifa linaweza kunufaika hasa katika harakati za kupambana na janga la umaskini.

“Zipo aina tisa za Azolla lakini mbili kati ya hizo zinapatikana Tanzania peke yake. Mataifa mengine wana aina chache za mmea huu, lakini hapa nchini zipo zote ila hizo mbili ni za kipekee kwa Tanzania. Ni baraka ya aina yake kwetu,” anasema.

Faida za mmea huo kwa wanyama, anaeleza ni pamoja na kutokuwa na hatari ya kubeba bakteria ambao wanaweza kusababisha maradhi kwao.

Faida nyingine husaidia kubadilisha virutubisho vilivyopo hewani ili vitumike kwa matumizi ya mimea, huku ukisafisha mazingira kwa kurekebisha hali ya joto.