Tunapofundisha masomo badala ya maarifa tutafika?

Muktasari:

Nadharia na masomo haviwezi kutuvusha kwenye umaskini wa akili na umaskini wa kipato. Tukiwajaza wananchi majuzuu ya nadharia na masomo ambayo hayawapi maarifa wala kuwafanya wawe wavumbuzi wa majibu ya matatizo yetu ni kutwanga maji kwenye kitu.

HOJA yangu kuu tangu wiki iliyopita ni hitaji la muhamo wa liwazo kwenye mfumo wa ufundishaji na elimu kwa jumla kama kweli tunataka kusonga mbele.

Ni dhahiri shahiri kuwa tunahitaji sasa kuachana na kuwafundisha watoto wetu masomo na nadharia na kujikita kufundisha ujuzi, maarifa na utambuzi.

Nadharia na masomo haviwezi kutuvusha kwenye umaskini wa akili na umaskini wa kipato. Tukiwajaza wananchi majuzuu ya nadharia na masomo ambayo hayawapi maarifa wala kuwafanya wawe wavumbuzi wa majibu ya matatizo yetu ni kutwanga maji kwenye kitu. Wenzetu walioendelea waligundua hilo mapema wakaachana na masomo sasa wanafundisha ujuzi, maarifa, uvumbuzi, utambuzi na ung’amuzi wa fursa za kimaendeleo na kuitafiti dunia.

Nimewahi kuandika kuwa wapo watu ambao hawajaingia darasani kabisa lakini wanaishi maisha mazuri kimifumo ya jamii zao bila kuwa na uhaba au upungufu wa mahitaji ya msingi kama maji, chakula na malazi. Wako babu zetu vijijini wana ujuzi na maarifa ya kutosha hata kutabiri hali ya hewa na majira ya misimu na wakachukua tahadhari lakini hawajui kusoma na kuandika.

Kiasili binadamu ni viumbe ambao Mungu ameweka ufahamu na weledi mkubwa bila kujali umezaliwa na nani. Ndiyo maana mtoto wa miezi minne hawezi kupeleka chakula sikioni; analenga ulipo mdomo bila kufundishwa. Kama Mungu hakuuweka weledi/umaizi hakuna mtu anayeweza kuuweka weledi huo.

Weledi asilia na umaizi ambao Mungu amempatia mwanadamu ndiyo kiungo kikuu cha mafanikio yake. Anachotakiwa kufanya ni kukuza vipawa hivyo, kuvipalilia vipawa hivyo ili vichanue na vitamalaki. Shule ziko kwa ajili ya kukuza na kuchagiza ujuzi, weledi, umaizi na vipaji vya binadamu ili vikue na vichanue siyo kukaririsha watu masomo au nadharia.

Wavumbuzi na wagunduzi wote hawakufundishwa darasani kuvumbua wala kugundua, ni akili yao ya kuzaliwa iliyosaidiwa na mazingira ya kutafakari na furaha ya ndani ya moyo.

Sasa, iweze leo tudharau asili ya akili na weledi wetu eti kwa sababu tu tuliachiwa masomo na wakoloni? Hata kama mtoto ana kipaji cha kuimba unalazimisha tena kwa kumchapa viboko ajue kanuni za pembe mraba? Unamlazimisha akariri tarehe ya kugunduliwa fuvu la mtu wa kale. Unamlazimisha akumbuke tarehe aliyofika Vasco da Gama ghuba ya uajemi na Rasi ya Tumaini jema, ili iweje? Jiulize wanaojua kuimba hawaishi? Wanaojua kucheza mpira hawaishi? Wanaojua kuchonga hawaishi? Wanaojua kujenga hawaishi? Wanaojua kuhubiri hawaishi? Wanaojua kufuma hawaishi? Wanaojua kutibu watu hawaishi?

Ujuzi, maarifa, utambuzi na ung’amuzi ndiyo kitovu cha mtalaa makini siyo nadharia. Jiulize kipi chenye manufaa kupata ujuzi kuhusu ufugaji bora na uvunaji wa gesi ama kujua idadi ya marais duniani? Kipi kina manufaa, kupata ujuzi wa kilimo bora au kujua vita vya kwanza vya dunia viliaza lini? Kipi kina manufaa kujua kanuni za ujenzi au kujenga? Kujua mbinu za ujasiriamali au kujua miyeyuko ya barafu huko Ulaya?

Elimu asilia ndiyo imefanya nchi zilizoendelea kutafakari aina ya maarifa wanayotakiwa kuwapa watoto wao ili waitawale dunia. Siyo kwetu maarifa hayatolewi kabisa, na msisitizo uko kwenye kukalili mada za masomo, ili kesho watukiwe shahada. Vyuo vikuu wanafanya bidii kukalili maandiko na nadharia za wanafalsafa wa kale-kisha wanatunukiwa digrii nyingi. Wanaitwa wasomi madaktari-pasipo ujuzi wala maarifa. Wakirudi kwenye jamii wanajikuta walichosoma hakifanani na hakiwasaidii kuyakabili maisha. Wanabaki kulalamika na kudai posho tu. Haya ndiyo malengo ya elimu?

Maarifa asilia waliwafanya babu zetu wasiojua kusoma na kuandika waweze kufanya biashara hadi nchi za jirani wakitembea kwa mguu bila kuwa na gari wala nyenzo-vivyo hivyo wamachinga wa leo. Lakini profesa wa biashara hawezi hata kuuza karanga.

Maarifa asilia ndiyo yaliyowafanya nchi za Ulaya watafsiri elimu sahihi iliyokuwa kwenye falsafa na teolojia zaa kale. Kuweka maarifa na ujuzi huo kwa lugha za jamii zao ili wayafahamu na kuyafanyia kazi kujiletea maendeleo. Kweli maendeleo yakafanyika!

Hata wanasayansi wengi waliogundua kanuni na fomula nyingi zilizotumika kutengenezea vitu kama magari, ndege hawakuwa na vyeti vingi. Wengine hakuwa na vyeti kabisa, bali walitumia muda wao mwingi kufikiri na kubuni kikamilifu hadi wakaibuka na manufaa hayo makubwa yaliyoibadili dunia hii.

Nadharia na masomo havitusaidii. Elimu ya asilia na maarifa tumizi ndivyo vitatusaidia kuondokana na umaskini wetu. Kubadili mitaala hukutusaidii, kurahisisha vigezo vya watu kupata digrii hakutusaidii, kuongeza idadi ya wasomi wa vyeti hakutusaidii na hata kujenga vyuo vikuu lukuki hakusaidii.

Kitakachotusaidia kama nchi ni kuachana na masomo tuliyoachiwa na wakoloni na kuanza sasa kuelimisha watoto wetu kwa elimu asilia na maarifa tumizi ili wawe wavumbuzi, wagunduzi, wabunifu na wenye maadili ya kuitafsiri dunia. Elimu asilia inawapa maadili ya rohoni watu kuwa watendaji siyo wapiga porojo. Elimu asilia inaibua vipaji na vipawa na kuvichepusha ili vitamalaki na kumsaidia mtu kuingiza kipato. Elimu asilia itawawezesha Watanzania kujua rasilimali zao na kuzitumia kupata nafuu ya maisha na utajiri. Ndiko kwenye siri ya mafanikio. Mungu atusaidie kung’amua hili.

0713-000027