Mbinu za kusoma na kusikiliza kwa ufahamu

Muktasari:

Ni vyema msomaji kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumsaidia kukumbuka.

Ufahamu ni dhana inayorejelea kujua na kulielewa jambo kwa usahihi ili kuweza kulielezea upya kwa pasipo kupoteza maana ya msingi. Hivyo, ufahamu wa mtu unaweza kupimwa katika kusikiliza jambo au kusoma.

Ufahamu upo wa aina mbili ambazo ni kwa njia ya kusoma na kusikiliza.

Ufahamu wa kusoma ni ule mtu anaoupata kwa njia ya kusoma habari, makala, jarida, kitabu au gazeti.

Ufahamu wa kusoma, msomaji anatakiwa kuzingatia kubaini mawazo makuu. Unaposoma habari yakupasa kubaini mambo ya msingi. Mada kuu inayoongelewa na hoja zingine zinazojitokeza. Kwa kuzingatia mambo hayo itarahisisha kuelewa habari hiyo kwa urahisi.

Pia, msomaji ni vyema azingatie alama za uakifishi. Hizi zitamwezesha msomaji kuelewa ujumbe wa habari hiyo na endapo hatazingatia alama za uakifishaji msomaji anaweza kupotosha maana iliyokusudiwa na mwandishi au mtunzi.

Kubaini na kuelewa maana ya maneno na misemo mbalimbali. Habari ambazo huwa zina maneno ya kisanaa ni muhimu kubaini maana ya maneno hayo katika muktadha wa habari hiyo.

Vilevile, msomaji anatakiwa kuwa makini na kile anachokisoma, kila kipengele anachokisoma inampasa akielewe vizuri.

Aidha, ufahamu wa kusikiliza hufanyika kwa njia ya kusikiliza habari fulani. Mtu anaweza kusikiliza kwa kusimuliwa, kusomewa au kutoka redioni au habari iliyorekodiwa.

Mambo ya msingi ya kuzingatia ili kufanikisha ufahamu wa kusikiliza ni haya yafuatayo:

Umakini wa hali ya juu na akili yote kuelekeza kwenye jambo linalozungumzwa. Macho kuelekeza kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema.

Ni muhimu kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji anaongeza jambo jipya, anatofautisha, anafafanua au anahitimisha hoja.

Ni vyema msomaji kuandika baadhi ya mambo anayoona kuwa ni ya muhimu ili kumsaidia kukumbuka.

Zingatia ishara mbambali za mwili kama vile kurusha mikono, kutingisha kichwa, kutingisha mabega au hata kupepesa macho. Ishara hizi huwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kupata maana katika mazungumzo.

Mathalan, kufupisha habari ni kuandika upya habari uliyoisoma kwa maneno machache lakini bila kupotosha ujumbe wa habari ya kwanza.

Mbinu hizo za ufahamu ndizo zitamwezesha mwanafunzi kufupisha habari. Habari hiyo huwa na sifa zifuatazo; lazima iwe fupi kuliko habari ya mwanzo.

Pia, huwa na ujumbe uleule uliokuwa katika habari ya mwanzo, hujumuisha mawazo makuu yaliyodondolewa kutoka kwenye habari ya mwanzo. Mawazo hayo yapangiliwe katika mtiririko wenye mantiki.

Ili kuweza kufanikiwa kufupisha habari kwa ufanisi hatua ni vyema kuisoma au kuisilikiza habari kwa umakini ili kuielewa vizuri.

Kutambua na kubaini mawazo makuu yanayojitokeza katika kila aya, kuyaunganisha mawazo makuu na kuandika au kuelezea ufupisho wa habari hiyo kwa maneno yako mwenyewe bila kupotosha maana ya habari ya kwanza, kuhesabu idadi ya maneno ya ufupisho ili kuyapunguza ikiwa yanazidi idadi uliyoambiwa kutokana na maelezo ya swali ulilopewa. Pia hakikisha hujaacha taarifa yoyote muhimu.

 

Mwandishi ni mhakiki wa lugha wa gazeti hili.