Omumwani: Shule ya wakulima wa kahawa iliyokombolewa na Serikali

Rais John Magufuli alipotembelea Shule ya Sekondari ya Omumwani. Kulia ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Rais Magufuli alitoa uamuzi ambao haukutarajiwa na wengi kwa kutangaza shule hiyo kuchukuliwa na Serikali kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Jumuiya ya Wazazi kupitia chama anachokiongoza cha CCM.

Ziara ya takriban dakika 20 iliyofanywa na Rais John Magufuli katika Shule ya Sekondari Omumwani ya mjini Bukoba, ilifuatiwa na uamuzi mgumu ulioifanya kuandikisha historia mpya tangu kuanzishwa kwake miaka 50 iliyopita.

Rais Magufuli alitoa uamuzi ambao haukutarajiwa na wengi kwa kutangaza shule hiyo kuchukuliwa na Serikali kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Jumuiya ya Wazazi kupitia chama anachokiongoza cha CCM.

Maswali aliyokuwa anauliza Rais Magufuli wakati akikagua miundombinu ya shule yaliashiria kuna jambo kubwa litafuata. Ndivyo ilivyokuwa wakati akihutubia mkutano wa kuhitimisha ziara yake katika Shule ya Sekondari Ihungo.

Akiwa Omumwani alihoji idadi ya vyumba vya madarasa vilivyokarabatiwa kupitia kamati ya maafa. Aliingia ndani na kunusa kitu kwenye kuta na baadaye kuhoji kama hiyo rangi ni mpya au ilikuwepo tangu zamani.

Aliuliza kama umeme umewekwa na kamati ya maafa au ulikuwepo.Alitaka kujua kama kuna jengo lolote lilikuwa limeathiriwa na tetemeko la ardhi na kukarabatiwa na kamati ya maafa na hata kupima urefu wa tanki la maji na kuhoji kama ni sehemu ya kazi ya kamati hiyo.

Alizungumza na vibarua na kuwauliza kama walikuwa wanalipwa kwa kazi ya jasho lao. Aliwauliza maswali ni matofali mangapi wanatumia kwa siku na hata kushuhudia kazi ya ujenzi iliyokuwa ikiendelea shuleni hapo.

Ili kupima kiwango cha ushirikishwaji, Rais Magufuli alitaka ajibiwe na Mkuu wa Shule hiyo, Godfrey Nestory na siyo mjumbe yeyote wa kamati ya maafa ambayo ilikuwa tayari imewasilisha taarifa kwa maandishi.

Rais Magufuli alimuuliza Nestory ana kiwango gani cha elimu ili kujua kama ana sifa za kuajiriwa serikalini. Alihoji kwa nini shule hiyo isichukuliwe na Serikali, kauli iliyojibiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene kuwa kuna mazungumzo yanaendelea.

Asili ya Omumwani

Shule ya Omumwani ni alama ya jasho la wakulima wa kahama wa Mkoa wa Kagera waliokubali kukatwa sehemu ya malipo ya mauzo ya zao hilo, ili kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwa ajili ya watoto wao.

Neno ‘Omumwani’ kwa tafsiri ya lugha ya Kihaya ni mbuni ambao hutoa matunda ya kahawa ambayo imekuwa nguzo ya uchumi kwa wakulima wengi wa mkoa huo na wakulima wengi walipata nguvu ya kugharimia masomo ya watoto wao kutokana na bei nzuri ya kahawa wakati huo.

Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1966 na kuwa chanzo cha baadhi ya viongozi wengi waliopo maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kunufaika na elimu kupitia uamuzi wa wakulima waliokubali kuichangia kupitia mauzo ya kahawa.

Shuleni kuna shamba la mibuni linalohuisha historia ya shule hiyo iliyotokana na mchango wa wakulima wa kahawa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera (KCU) kila mkulima wakati ule alikubali kuchangia nusu senti kwa kila kilo ya kahawa utaratibu uliodunu hadi miaka ya 1970.

Baada ya hapo wakulima walipitisha uamuzi mpya wa kuchangia Sh3 kwenye kilo ya kahawa hadi hapo utaratibu huo ulipobadilika kutokana na mabadiliko ya kimfumo na baadaye Omumwani kuangukia mikononi mwa Jumuiya ya Wazazi wa CCM.

Watu maarufu

Ni shule ya kwanza ya wazazi kuanzishwa hapa nchini ambapo usajili wake wa namba S0339 unathibitisha ukongwe wake miongoni mwa shule za sekondari 3,452 zilizokuwa zimesajiliwa na kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015.

Historia ya shule inawataja viongozi mbalimbali na watu maarufu walionufaika na uamuzi wa wakulima wa kahawa na kufanikiwa kupata elimu yao kupitia shule hiyo iliyopo kwenye miinuko ya mji wa Bukoba.

Miongoni mwa orodha ndefu ya waliosomea hapo ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani Willison Masilingi ambaye pia amewahi kushika nyadhifa za uwaziri na ubunge Jimbo la Muleba Kusini kwa miaka 15.

Pia, katika orodha hiyo yupo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM ngazi ya Taifa, Abdalah Bulembo na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Mujuni Kataraiya.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Kagera, Chrisant Kamugisha ambaye pia alisomea Omumwani anasema ujenzi wa shule hiyo uliwezekana kwa kuwa wakulima walikuwa na sauti moja na hawakutawaliwa na ubinafsi.

Mwanafunzi huyo wa zamani ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba anasema zamani kulikuwa na ari kubwa ya wananchi kujitolea kwenye masuala ya kijamii ikiwamo elimu na miradi mbalimbali.

‘’Ni kama ushindi shule hiyo kuchukuliwa na Serikali baada ya kuingia kwa vyama vingi mambo mengi yalitawaliwa na ubinafsi. Zamani watu walijitolea na baadaye ukaja ulaji, hatua iliyochukuliwa na Rais Magufuli ni muhimu na ya kupongezwa,’’ anasema Kamugisha.

Ufaulu

Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa miaka minne mfululizo katika shule ya sekondari ya Omumwani yanaonyesha kuwepo kwa anguko kubwa kielimu na zilihitaji hatua za dharura ili iweze kusimama tena.

Kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne yaliyopo kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani (Nacte)mwaka 2012 jumla ya wanafunzi 91 walifanya mtihani ambapo waliopata kati ya daraja la kwanza na tatu ni wanafunzi sita na 54 kupata daraja sifuri.

Pia, mwaka 2013 wanafunzi 106 walifanya mtihani na waliopata kati ya daraja la pili na tatu ni 13, huku 36 wakipata daraja sifuri na hali haikuimarika hata kwa mwaka uliofuata wa 2014 waliofanya mtihani ni 82 na 38 kupata daraja sifuri.

Hadi shule hiyo inatangazwa kuchukuliwa na Serikali ilikuwa imebaki na jumla ya wanafunzi 49, huku wasichana 32 wakipelekwa shule ya bweni ya wasichana Rugambwa iliyopo Manispaa ya Bukoba.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Godfrey Nestory wavulana 17 waliokuwa wanasomea Omumwani wako Sekondari ya Maruku na baadhi yao shule ya kutwa ya Nshambya na wote wanasubiri taratibu za kuwahalalisha kusomea shule za Serikali.

Awali, wanafunzi hao walihamishwa kwa dharura ili kuwapa nafasi wanafunzi wa sekondari Ihungo waliohamishiwa hapo ili kupisha ujenzi wa shule yao inayojengwa upya baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi la Septemba 10 mwaka jana.