Tehama kwa walimu nchini haikwepeki

Mwakilishi Mkazi na  Mkurugenzi wa Unesco nchini, Zulmira Rodriuguez (kushoto),  akizungumza na Mratibu wa Tehama wa Unesco, Faith Shayo  wakati wa makabidhiano ya  viwango vya ushindani vya Tehama kwa walimu. Picha na Florence Majani

Muktasari:

Kabla ya sayansi na teknolojia, yalikuwepo mapinduzi ya kwanza ambayo ni ugunduzi wa lugha ya kuandika. Ya pili ni yale ya uvumbuzi wa maandishi ya kuchapisha mnamo karne ya 15 na ya tatu ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Mapinduzi ya teknolojia yamebadilisha mambo mengi. Yamebadili mwenendo wa maisha, utendaji wa kazi, shughuli za kijamii, siasa, uchumi na hata elimu.

Kabla ya sayansi na teknolojia, yalikuwepo mapinduzi ya kwanza ambayo ni ugunduzi wa lugha ya kuandika. Ya pili ni yale ya uvumbuzi wa maandishi ya kuchapisha mnamo karne ya 15 na ya tatu ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Mapinduzi ya sayansi na teknolojia yamepenya katika kila eneo na sasa imebainika kuwa ili kuimarisha sekta ya elimu nchini walimu hawana budi kujifunza Tehama ambayo itawasaidia katika ufundishaji lakini pia kukuza ufahamu wao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu ya Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na walimu wa shule za msingi hadi vyuo vikuu, wameunda viwango vya ushindani katika Tehama kwa ajili ya walimu.

Viwango hivyo vimelenga kuwandaa walimu kujifunza Tehama ili waweze kuwafundisha wanafunzi katika ubora unaotakiwa.

Unesco inasema walimu wote wanaofundisha na walio masomoni wanatakiwa kusoma Tehama, ili waweze kushindana vyema katika kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia teknolojia hiyo.

Mwakilishi Mkazi na Mkuu wa Unesco, Zulmira Rodriguez anasema walimu wa ngazi zote na wale walio masomoni wanatakiwa kusoma na kuwa na uelewa wa Tehama ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuwafundisha wanafunzi wao.

“Walimu wanahitaji teknolojia hii ili wawasaidie wanafunzi kutumia teknolojia, watatue matatizo katika ufundishaji na warahisishe kazi,” anasema.

Anasema kwa kuwa jamii haiwathamini walimu, hata wanafunzi nao hawawathamini walimu, hivyo ujuzi wa Tehama utakuwa chachu ya kuithaminisha taaluma hiyo.

Rodriguez anasema walimu wakipata

 

ujuzi wa Tehama wataboresha ufundishaji wao na hata wanafunzi watapata elimu bora na inayoendana na wakati.

“Elimu itakuwa ni ya furaha, ufundishaji utarahisishwa na walimu watakuwa watu wa kwanza kutoa taarifa kwa wanafunzi badala ya wanafunzi kupata taarifa au elimu kupitia mitandao,” anasema.

Kamishna wa Elimu nchini, Profesa Eustella Bhalalusesa anasema Serikali inauangalia mustakabali wa watu wake katika masuala ya ujuzi, utaalamu na uvumbuzi na ndiyo maana imetambua umuhimu wa mfumo bora wa elimu.

“Kwa hali hiyo walimu wanatakiwa kukabiliana na changamoto na fursa za utandawazi ambazo ni pamoja na kukua kwa sekta ya Tehama. Matumizi haya ya Tehama yanasaidia ufundishaji na mchakato wa ujifunzaji,” anasema.

Anaongeza kuwa matumizi ya Tehama yanafanya elimu iwe jambo la kuvutia na wanafunzi hulifurahia.

Anasema ili walimu wawe na uwezo wa kufundisha wanafunzi Tehama wanatakiwa wawe na viwango vya kiushindani katika teknolojia.

“Tehama inatoa fursa ya elimu eneo lolote wakati wowote lakini pia nafasi sawa ya kushirikiana na kuwasiliana na wengi,”anasema.

Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kupatikana baada ya walimu kupata elimu ya Tehama ni kiwango cha elimu kukua kutokana na mwingiliano wa teknolojia katika kujifunza na ufundishaji.

Pili, kuongeza kiwango cha walimu kitaaluma kwa kutumia Tehama. Pia mazingira ya kujifunza yatarahisishwa kwa kutumia teknolojia hiyo.

Unesco kwa kushirikiana na wadau wa elimu na serikali ya China walizindua viwango vya ushindani katika Tehema kwa walimu ambavyo vitatoa elimu na ujuzi unaotakiwa kutumika kwenye Tehama. Viwango hivyo vitasaidia walimu kufanya kazi yao ufundishaji kwa urahisi zaidi.

Akizungumzia kuhusu Tehama kwa walimu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Ralph Masenge anasema nivyema kuhakikisha walimu wa vyuo vikuu wanakubali viwango vya ushindani katika Tehama na kuvitumia.

“Hili ni jukwaa muhimu zaidi katika kuimarisha mfumo wa elimu, Tehama itatumika kujenga uwezo wa walimu,” anasema.

Lakini Rodriguez anasema ni lazima kuhakikisha walimu wanaojifunza Tehama wanafuatiliwa kujua kama wamepata ujuzi huo.

Anaongeza kuwa ni vyema ikawepo aina ya mafunzo ya Tehama kwa walimu ambayo yanapatikana kwa urahisi kwa mfano kwa njia ya mtandao.

Mwalimu wa shule ya msingi Kimandolu, Sarah Mvungi anasema iwapo zana kama kompyuta zitakuwepo shuleni, basi Tehama itakuwa mkombozi mkubwa katika elimu.

“Lakini si kompyuta tu, bali lazima tuwe na mawasiliano ya intaneti, yatakayotuwezesha kupata tovuti zenye mada au masomo tunayofundisha,” anasema

Mvungi anasema wanafunzi wa sasa si kama wa zamani, kwani wengi wanajifunza kila kitu kupitia mitandao jambo ambalo wakati mwingine linawafanya walimu wawe nyuma kama hawatumii mitandao hiyo.

Lakini anatoa angalizo kuwa miundombinu ya Tanzania kama upatikanaji wa umeme na vifaa bado ni tatizo nchini, hivyo huenda mafunzo hayo yakabaki vichwani tu na si katika utekelezaji.

Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Msingi Sokon 11, Arusha, Victor Kasembe anasema Tehama itawanyanyua walimu na kuwaweka katika hadhi ya juu, itawarahisishia kazi na kuwaweka katika mtandao mpana wa habari.