Wahitimu Weruweru waionyesha jamii njia kujali shule walizosoma

Mwenyekiti wa  umoja wa wanafunzi  waliosoma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru,  Balozi Mwanaidi Maajar  akizungumza jana jijini Dar es salaam katika kikao kilichowakutanisha baadhi ya wanafunzi  waliosoma  shule  hiyo, kushoto ni Katibu wa umoja huo,  Bertha Somi.  Picha zote  na Aika Kimaro

Muktasari:

Hata Ulaya shule zinasaidiwa na wanafunzi waliowahi kusoma katika shule hizo. Kwa wahitimu wa Weruweru, wanataka kujenga jamii ya watu wanaozijali shule zao.

Ni watu wangapi wanaozikumbuka shule zao walizopitia kunoa bongo?, Jibu ni watu wachache, ndio maana shule nyingi nchini hasa walizosoma watu maarufu, wakiwemo wenye uwezo mkubwa kifedha ziko katika hali ya kusikitisha.

Hata hivyo, utamaduni na mwamko wa kuzikumbuka shule, sasa vinaanza kujengeka miongoni mwa Watanzania.

Kwa mfano, badala ya kuendelea kujitolea tu katika matukio kama vile harusi na mengineyo, wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru, wameamua kubadili mtazamo.

Kwa dhamira moja wameamua kukusanya nguvu kuisaidia shule hiyo kongwe ambayo wanawake wengi maarufu nchini wakiwemo viongozi katika kada mbalimbali walipitia hapo katika safari ya kusaka elimu.

Sio tu wana umoja wao, wanawake hao pia wameanzisha kampuni (Weruweru Alumni Foundation Limited), huku wakilenga kukusanya Sh500 milioni zitakazotumika kukarabati miundombinu ya shule hiyo pamoja na ujenzi wa bweni.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Balozi Mwanaidi Maajar, aliyehitimu shuleni hapo mwaka 1971, anasema pamoja na mambo mengine wana azma ya dhati ya kurudisha fadhila kwa shule yao iliyochangia kuwapa msingi bora wa maisha.

“Wakati tunasoma pale, ilikuwa ni shule nzuri sana, watu waliosoma pale kwa kweli tulifaidika kwa mengi. Ndiyo maana tumeona wakati shule hii ikiwa inatimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, watu tuliosoma pale lazima tufanye kitu,” anasema na kuongeza:

“Hata kwa shule za Ulaya, nyingi zinasaidiwa na wanafunzi ambao walipita katika shule hizo. Lengo la kukutana hapa ni zaidi ya Weruweru, tunataka kujenga jamii ya watu wanaoweza kujali shule zao.”

Anasema ili kutimiza dhamira yao, kampuni waliyoanzisha itakuwa chachu ya kuwakusanya pamoja wanafunzi waliosoma shuleni hapo.

“Hii kampuni siyo kwa ajili ya miaka 50 pekee, itadumu kwa miaka mingi ijayo. Lengo ni kuhakikisha kuwa Weruweru inasonga mbele zaidi,” anaeleza.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo ambaye naye ni moja ya matunda ya Weruweru, Rosalia Firmin, anaamini umoja wa wanafunzi na kampuni yao vitasaidia kuboresha shule hiyo anayosema pamoja na kuendelea kufanya vizuri kitaaluma, inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu.

“Tunataka kuona watoto wanaopita pale wote wanapata fursa ya kuendelea na elimu ya juu,” anabainisha.

Mhitimu mwingine wa shule hiyo ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba anaikumbuka shule yake kuwa miongoni mwa shule zilizokuwa vinara katika utoaji taaluma bora.

“Miaka ile tulikuwa ni wasichana wachache tuliopata elimu, kwa hiyo ni muhimu sasa turudishe fadhila zetu kwa jamii na shule yetu,” anasema na kuongeza kuwa wanafunzi wengi enzi zake waliipenda shule hiyo kutokana na kuwa na mazingira yaliyovutia na taaluma bora.

“Mtu ukiwa likizo ulitamani shule ifunguliwe ili urudi, tulikuwa tunasoma bure, mazingira yalikuwa mazuri, chakula kizuri na kila kitu kilikufanya upende shule…’’ anafafanua.

Anasema umoja waliouanzisha una nafasi kubwa ya kurudisha mazingira ya shule hiyo kama yalivyokuwa awali na kufanya wanafunzi wanaosoma hapo kuipenda shule yao na hivyo kutimiza ndoto zao kielimu.