MAONI: Zinahitajika hatua zaidi kuwalinda tembo wetu

Muktasari:

Maadhimisho hayo yatazikutanisha Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi Wanyamapori (WWF) ofisi ya Tanzania ambako watatoa matamko na kushiriki mijadala ya namna ya kuwaokoa tembo dhidi ya ujangili. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: Tuiunganishe Dunia pamoja kumwokoa tembo.

Leo ni siku ya tembo duniani. Hii ni siku ambayo Watanzania wanaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha na kwa nchini, maadhimisho yatafanyika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Maadhimisho hayo yatazikutanisha Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi Wanyamapori (WWF) ofisi ya Tanzania ambako watatoa matamko na kushiriki mijadala ya namna ya kuwaokoa tembo dhidi ya ujangili. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: Tuiunganishe Dunia pamoja kumwokoa tembo.

Pamoja na mambo mengine malengo ya kuadhimisha siku ya tembo kitaifa ni kujenga uelewa na kuchochea hamasa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mnyama huyu na wanyama wengine na kutunza uhifadhi wa wanyama, kujadili kwa kina madhara ya ujangili kiikolojia, kiutamaduni na kutoa mapendekezo hatua za kuchukua kuzuia tatizo hilo.

Tayari makundi ya waandishi wa habari na wanaharakati watetezi wa wanyama, wamejitosa kukomesha ujangili ili kusaidia maliasili hii muhimu iendelee kuwapo vizazi na vizazi. Wanahabari sita vjana kutoka YOUTUBE nchini Ujerumani wamewasili nchini kwa ajili ya kampeni ya kuisaidia Tanzania kupata fedha za kuhifadhi pori la akiba la Seleous na kutangaza utalii duniani kwa kurusha picha mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kupitia mtandao huo ambao unafuatiliwa na watu milioni tatu duniani.

Aidha, kundi la pili la wanahabari wakongwe wa magazeti kutoka vyombo mbalimbali vya kimataifa nchini Ujerumani nao wamewasili nchini wakiongozwa na mwakilishi wa shirika la WWF kwa ajili ya kusaidia kutafuta fedha kwa wafadhili duniani ili kuokoa hifadhi na wanyamapori wetu wakiwamo tembo ambao wao huwaona kupitia kwenye filamu tu tofauti na sisi ambayo neema imejaa tele na ni ya kujivunia.

Maadhimisho haya yanatokana na mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa kuzuia biashara ya wanyamapori na viumbe walioko hatarini kutoweka (Convention on International Trade in Endangered Species – CITES) uliofanyika mwaka 2010 katika Jiji la Doha, Qatar.

Tanzania inasifika kwa kuwa na utajiri mkubwa wa wanyamapori barani Afrika na ni nchi ya pili ulimwenguni kuwa na rasilimali nyingi asili.

Tunazo hifadhi nyingi zinazotuingizia fedha nyingi za kigeni zikiwa na wanyama mbalimbali wakiwamo tembo. Baadhi ya hifadhi hizo ni Serengeti, Manyara, Ruaha, Mikumi, Ngorongoro, Tarangire, Katavi na pori la akiba la Selous.

Wito kwa Watanzania ni kwamba tunapoadhimisha siku hii, sote tukumbuke kwamba ni wajibu wetu kuzuia ujangili dhidi ya tembo unaoendelea nchini.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Tawiri mwaka 2014, idadi ya tembo inazidi kupungua nchini kutoka 103,422 mwaka 2009 hadi tembo 43,330.

Hali hii ni mbaya na kwamba ujangili usipodhibitiwa basi huenda tembo katika miaka michache ijayo watatoweka nchini kutokana na watu wanaowauwa tembo ili kujipatia pembe ambazo mahitaji yake yanazidi kuongezeka duniani kote, hasa katika nchi za Asia. Biashara hii inakadiriwa kuwa yenye thamani ya dola milioni 165 hadi 188 kila mwaka.

Hivi karibuni Serikali ilianzisha Operesheni Tokomeza Ujangili lakini ilijaa kasoro. Bila shaka Serikali itakuwa imejifunza kutokana na makosa yale iandae operesheni nyingine kabambe ili kudhibiti mianya yote inayotumiwa na majangili kujipenyeza hadi kwenye hifadhi na mapori ya akiba.

Pia, Serikali inaweza kusitisha kwa muda fulani ikiwezekana hata miaka 10 utoaji wa leseni kwa vitalu vya uwindaji wanyamapori ambazo baadhi zinadaiwa kutumika kufanyia ujangili wa tembo.

Vilevile, hatua nyingine zinazopaswa kuchukuliwa na ni pamoja na kulinda shoroba za wanyamapori hususan tembo, kupunguza migogoro kati ya wananchi na hifadhi, kufanya tafiti na kushirikisha wadau mbalimbali katika uhifadhi wa tembo.

Aidha, ni wajibu wa Watanzania wote kushirikiana kuwafichua watu wanaofanya biashara ya meno ya tembo ili wachukuliwe hatua za kisheria. Majangili hawatoki kusikojulikana bali wanatoka miongoni mwetu. Ni jamaa zetu; ndugu au marafiki. Tuwadhibiti.

Joyce Joliga ni Mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwa namba 0767 /0713 59 55 63