Huyu ndiye Stella dereva wa malori ya masafa marefu

Muktasari:

  • Tafsiri ya jumla ni kwamba wanawake wengi wanapenda fani ambazo si za kutumia nguvu nyingi, wakati wengine wanapendelea kufanya majukumu yao ya kiasili ikiwamo kulea watoto kwenye familia.

Dar es Salaam. Katika nchi nyingi za Bara la Afrika, ikiwamo Tanzania imezoeleka kuwa kuendesha gari la masafa marefu ni fani ya wanaume. Pia, imejengeka imani kuwa ni fani ambayo wanawake hawaiwezi.

Tafsiri ya jumla ni kwamba wanawake wengi wanapenda fani ambazo si za kutumia nguvu nyingi, wakati wengine wanapendelea kufanya majukumu yao ya kiasili ikiwamo kulea watoto kwenye familia.

Japokuwa hii dhana ya kwamba wanaume pekee ndiyo wana uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya udereva inapingwa vikali na baadhi ya watu akiwamo Stella Aladini (43) ambaye ni dereva wa malori.

Stella ni miongoni mwa madereva wanawake wachache ambao wameamua kujishughulisha na fani ya udereva wa masafa marefu.

Achilia mbali uwezo wake wa kuendesha malori, awali aliwahi kuendesha mabasi makubwa yajulikanayo kwa lugha nyepesi ‘mabasi ya mkoani’.

Akiwa kama dereva wa jinsia ya kike, Stella anasimulia kwamba ni miaka 20 sasa tangu ameanza fani ya udereva.

Kwa sasa ni mwajiriwa wa Kampuni ya ZH-Poppe Ltd yenye maskani yake jijini Dar es Salaam ambayo inajishughulisha na kazi ya kusafirisha mizigo ikiwamo mafuta ya kuendeshea mitambo kutoka Tanzania kwenda nchi za jirani kama Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Malawi.

Stella anasimulia kwamba tangu akiwa mtoto alikuwa na ndoto ya kuwa dereva mzuri wa mabasi na malori, hivyo alikuwa anatamani siku moja atimizie ndoto yake.

Anasema ‘Mungu si Athumani’ hivi sasa anajivunia kuwa derema mzuri kwa kuwa amefanikiwa kutimiza ndoto ya maisha yake.

Kwa fani yake ya udereva wa malori, amepata fursa ya kutembea sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Anasema fani ya udereva kwake anaichukulia kama zilivyo fani nyingine kwa mfano kufanya kazi katika taasisi za fedha ambazo zinaajiri idadi kubwa ya watu nchini.

“Nilianza fani yangu ya udereva tangu mwaka 1998, enzi hizo nilikuwa naendesha lori la kusafirisha mifuko ya saruji kutoka Songwe kuelekea Iringa. Japokuwa sikufanya kazi kwenye hiyo kampuni kwa mda mrefu kwa sababu nililazimika kurudi shule ya udereva kujifunza zaidi ili kuongeza ujuzi wangu,” anasema Stella ambaye ameolewa na kwa sasa ni mama wa watoto wawili.

Baada ya kumaliza mafunzo yake, Stella aliajiriwa na kampuni nyingine ya mabasi ya abiria ambako alifanya kazi hiyo kwa miaka kumi baadaye aliamua kuachana na kazi hiyo na kurudia fani yake anayoipenda ya kuendesha malori.

Stella anasimulia zaidi kwamba hajawahi kuwa muoga wa kuendesha magari kwa umbali mrefu kama ambavyo madereva wengi wanawake wanashindwa kwa kuhofia usalama wa maisha yao, huku wakiwapa nafasi zaidi wanaume kufanya hivyo.

Matukio ya kutisha

Kama ilivyo kawaida kwenye kazi yoyote hazikosekani changamoto, ndivyo ilivyo kwa Stella, anaeleza kwamba katika fani yake ya udereva wa masafa marefu amekuwa anakumbana na changamoto nyingi zinazotishia uhai wa maisha yake ikiwamo kutekwa, kuibiwa, kuteswa na makundi ya waasi nchini DRC.

“Mara ya kwanza nilitekwa maeneo ya Igunga wakati naendesha basi la abiria kutoka Kigoma. Nikiwa njiani nikaona barabara imezibwa na mawe makubwa, pembeni kulikuwa na gari dogo limeegeshwa ghafla kutoka kwenye gari hilo wakajitokeza watu wawili wamebeba bunduki na kuanza kutushambulia.

“Risasi mbili zilinipata, mguuni na mkononi, nilikuwa nasikia maumivu makali sana,” anasema Stella.

Anasimulia zaidi kuwa baada ya majambazi kulishambulia basi kwa risasi, yalivamia na kuanza kuwapora abiria vitu vya thamani kama simu za mkononi, saa na fedha taslimu hatimaye wakatokomea msituni baada ya askari kuchelewa kufika eneo la tukio.

Hata hivyo, tukio la kupigwa risasi si tukio pekee la kusikitisha ambalo Stella amewahi kukumbana nalo.

“Nilitekwa tena maeneo ya Bukoba wakati naendesha basi la abiria kutoka Bukoba kuelekea Arusha. Lakini kwenye tukio hili nilitekwa na madereva wenzangu wa kampuni nyingine, tuliporwa mali na kuteswa,” anasimulia.

Haikuishia hapo, Stella anasema alitekwa tena na kikundi cha waasi akiwa anaelekea nchini DRC ambako alikuwa anasafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kupeleka mjini Lubumbashi.

“Hakuna usalama kabisa. Waasi nchini Congo wana tabia ya kuteka magari, kuvunja madirisha na kupora mali za madereva wa Tanzania. Muda mwingine wanateka madereva na kudai fedha nyingi kutoka kwa wamiliki wa malori ili waweze kuwaachia.

“Kitu cha kushangaza ni namna ambavyo askari nchini humo hawachukui hatua zozote kudhibiti vitendo hivyo. Kwa kifupi wanaona hawaguswi kabisa na kinachotokea kwa madereva wa Tanzania,” anasimulia. Licha ya kutokea kwa matukio makubwa ya kuhatarisha uhai wake, Stella anakiri hajawahi kufikiria kuachana na udereva na kusisitiza kuwa anaipenda kazi yake na kinachomtokea ni mapito tu na changamoto kama zilizopo kwenye kazi nyingine.

“Sikati tamaa hata kidogo, haya ndiyo maisha niliyoyachagua hivyo inanipasa kuwa imara na jasiri kukabili changamoto za barabarani,” anasema.

Changamoto mipakani

Changamoto nyingine ambayo anakutana nayo akiwa kwenye safari zake ni sekeseke la kuvuka mipaka ya Tanzania kwenda Congo, Burundi na Malawi kutokana na ukubwa wa foleni za magari mpakani, huku wakati mwingine Stella akilazimika kukaa mpakani kwa zaidi ya siku kumi.

Stella ambaye muonekano wake wa nje ni mrefu, mweusi na mwembamba, ni miongoni mwa madereva wengi wa malori ambao wako hatarini kuugua magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu kutokana na ukosefu wa huduma muhimu za maji na choo sehemu za mipakani.

“Tunalazimika kununua chupa za maji mijini ambazo tunazitumia kipindi cha foleni tukishafika mpakani,” anasimulia.

Kuhusu suala la kuchagua dereva mzuri kati ya mwanaume na mwanamke, Stella anasisitiza wanawake ndiyo wazuri kushinda wanaume kwa kuwa wako makini zaidi barabarani.

“Wanawake ni madereva wazuri zaidi ya wanaume ukizingatia hata kwenye ajali nyingi za barabarani huwezi kusikia mwanamke amehusika, au kusababisha ajali, siku zote tuko makini kuzingatia alama na sheria za barabarani,” anasema.

Tanzania kama ilivyo nchi nyingine duniani, ajali za barabarani zinaongoza kwa vifo vya watu ukiachilia mbali idadi ya vifo vinavyosababishwa na magonjwa.

“Binafsi sijawahi kusababisha ajali yoyote tangu nimeanza udereva. Kujiamini na kujitambua nikiwa barabarani ndiyo siri kubwa ya mafanikio yangu,” anasema.

Sifa na umaarufu

Sifa na umaarufu wa Stella unaanzia eneo lake la kazi, wafanyakazi wenzake wanasifia utendaji wake na kumuita mwanamke wa mfano.

Mukuya Lukosi (40), ambaye wanafanyakazi pamoja anamwelezea kama mwanamke jasiri.

Naye katibu mkuu wa umoja wa madareva, Abdallah Lubala anaiomba Serikali kuzalisha wakufunzi wa kutosha ambao watatumika kutoa elimu ya vitendo na nadharia kwa madereva wengi nchini, lengo likiwa ni kuboresha huduma za usafirishaji.

“Mazingira ya fani ya udereva siyo rafiki kwa wanawake, hivyo inawakatisha tamaa kujiunga kwenye fani,” anasema.

Pia, anataja mishahara midogo kuwa changamoto nyingine ambayo inawakwamisha wanawake wengi kujiunga na udereva na kwamba, madereva wengi wa malori wanalipwa maishara midogo kuanzia Sh450,000 kwa safari moja kusafirisha mzigo nje ya nchi.