Watanzania changamkieni fursa za mazao ya mizizi

Zao la muhogo pichani. Zao hilo linaweza kuwatoa kimaisha wakulima wengi kama watalima kwa njia za kisasa na kuchangamkia masoko ndani na nje ya nchi. Picha na Maktaba

Muktasari:

Thailand inaongoza kwa kuuza mihogo nje ya mipaka yake. Asilimia 80 ya mihogo inayouzwa kwenye soko la kimataifa inatoka nchini humo, huku Vietnam na Indonesia zikifuata; kila moja ikiwa na asilimia nane. Kiasi kinachobaki kinatoka Afrika, Asia na Amerika Kusini

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na ardhi yenye rutuba, inayoruhusu mazao ya kila aina kustawi ikiwamo yale yatokanayo na mizizi. Mazao hayo yapo mengi kulingana na maeneo, lakini kwa hapa nchini yenye nafasi kubwa ni viazi vitamu na mihogo.

Viazi vitamu kwa Tanzania hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma.

Zao jingine katika kundi hilo ni mihogo. Asilimia 60 ya kilimo chake duniani kinafanywa kwenye nchi tano; Nigeria, Brazil, Thailand, Indonesia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Thailand inaongoza kwa kuuza mihogo nje ya mipaka yake. Asilimia 80 ya mihogo inayouzwa kwenye soko la kimataifa inatoka nchini humo, huku Vietnam na Indonesia zikifuata; kila moja ikiwa na asilimia nane. Kiasi kinachobaki kinatoka Afrika, Asia na Amerika Kusini

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), mihogo ni zao la tatu kwa kuwa na kiwango kikubwa cha wanga nyuma ya mchele na mahindi. Ni chakula kikuu cha baadhi ya mataifa ya Afrika, Asia na Amerika Kusini.

Takwimu zinaonyesha Tanzania ipo katika nafasi ya nne nyuma ya Nigeria, Ghana na DRC kwa kilimo cha mihogo barani Afrika.

Fursa zilizopo

Awali wakulima wengi walikuwa wanachukulia mazao ya mizizi kama ya akiba hasa kwenye vipindi vya njaa, lakini kwa sasa yanalimwa kibiashara huku yakileta  heshima na kuinua kipato cha wakulima.

Mazao hayo yana sifa kubwa ya kuvumilia ukame. Hivyo, ni kawaida kupatikana hata kipindi ambacho mazao mengine yameadimika.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Dk Hussein Mansoor anasema kilimo cha mazao yatokanayo na mizizi kina manufaa makubwa tofauti na wengi wanavyofikiria.

Anasema kwa muda mrefu mazao ya mihogo na viazi yamekuwa hayapewi kipaumbele na wakulima kutokana na kile wanachoamini kuwa hayana biashara tofauti na ilivyo kwa mazao mengine.

“Tunalalamika njaa kwa sababu wengi tunaamini mahindi ndiyo chakula, ukweli ni kwamba mazao ya mizizi ni chakula  bora tena chenye afya tele. Mihogo na viazi vitamu ni mazao yenye  soko kubwa kwa sasa,” anasema. 

Anasema duniani kote, mazao yatokanayo na mizizi yamepanda thamani na mahitaji yanaongezeka kila kukicha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rum-Zahrain inayojihusisha na kilimo na usindikaji wa mihogo, Rukia Liumba anasema zao hilo lina manufaa makubwa na limekuwa chanzo kikubwa cha uchumi.

Rukia anamiliki kiwanda kinachotengeneza unga bora wa muhogo ambao husambazwa kwenye masoko mbalimbali nchini.

Katika kurahisisha biashara yake, Rukia ana shamba ambalo anatumia kulima mihogo anayoitumia kiwandani kwake.

“Nalima mwenyewe, nimeajiri watu wanaofanya kazi ya kulima, kumenya na kutengeneza mihogo hadi kufikia kuwa unga,” anasema.

“Naweza kusema ni biashara yenye faida endapo Serikali itaamua kuipa kipaumbele. Mimi nauza chenga za muhogo, unga bora na hata mbegu za kisasa za zao hili. Nimesikia hata samaki wanaofugwa kwenye mabwawa wanakua vizuri wakila unga wa muhogo.”

Anasema mkulima aliyejikita kwenye zao hilo anakuwa na uhakika wa kupata chakula na fedha endapo ataamua kuuza mazao yake.

Mbali na  hilo, unga unaotokana na muhogo unaweza kutengeneza bidhaa za kuoka kama mikate, keki, biskuti na   tambi.

Viazi vitamu

Yusuph Dramani ambaye ni mtafiti wa viazi kutoka taasisi ya utafiti ya kimataifa ya zao hilo kutoka Ghana,  anasema viazi vitamu hutumika kama chakula kwa kutayarishwa katika njia mbalimbali, kulingana na utamaduni wa eneo husika.

Pia, unga wa viazi vitamu hutumika kutengeneza vyakula kama keki, maandazi, kalimati na tambi.

“Uzuri wa kilimo cha viazi vitamu ni kwamba huchukua muda mfupi kukomaa, hivyo kumlipa mkulima mapema. Kwa kawaida huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi minne tangu kupandwa kutegemeana na hali ya hewa,’’ anasema.

Anasema viazi vinaweza kuvunwa kidogo kidogo kwa kutumia mikono, vijiti, jembe, mashine ya kukokotwa na ng’ombe kadri vinavyohitajika.