Mghwira: Zuio la mikutano limewaongezea umaarufu wapinzani

Waziri Mkuu wa Mstaafu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akizungumza na wananchi kwenye mnada wa ng'ombe wa Lusaunga, Biharamulo, mkoani Kagera jana. Na Mpigapicha Maalum

Muktasari:

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Mghwira ambaye alikuwa mgombea pekee wa kiti cha urais mwanamke katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anasema utafiti aliofanya kwenye mikoa kadhaa umeonyesha wananchi wanaendelea kuviunga mkono vyama vya upinzani licha ya kutofanyika kwa mikutano ya hadhara.

Wakati wanasiasa wakiendelea kutumikia agizo la kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa lililotolewa na Rais John Magufuli, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amesema zuio hilo limewakuza zaidi wapinzani.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu hivi karibuni, Mghwira ambaye alikuwa mgombea pekee wa kiti cha urais mwanamke katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anasema utafiti aliofanya kwenye mikoa kadhaa umeonyesha wananchi wanaendelea kuviunga mkono vyama vya upinzani licha ya kutofanyika kwa mikutano ya hadhara.

“Wananchi wanaelewa mchango wa vyama vya siasa na kuwa kazi zake zimesaidia sana kuuhabarisha umma juu ya mambo mbalimbali ya uendeshaji nchi na kumsaidia Rais kujua mambo yaliyoibuliwa na vyama hivi, ambayo pengine siyo rahisi kwake ama wasaidizi wake kuyajua,” anasema Mghwira.

“Kwa hiyo mtazamo wa wananchi ni dalili kuwa umetujenga upinzani zaidi kuliko kubomoa. Kwa kuwa Watanzania siyo watu wa vurugu siyo rahisi kuliona hili, lakini ukikutana na raia mahali ambapo hawana hofu ya kutoa maoni, utagundua wanapenda vyama vyote vifanye kazi kwa usawa,” anasisitiza.

Anasema amebaini kuwa wananchi wengi wana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo muhimu yanayopatikana katika vyama vya siasa.

Swali: Ukiwa kiongozi wa chama cha upinzani unaionaje ndoto ya upinzani kuchukua nchi miaka ijayo? Dalili zipo au hakuna? Kama hakuna wapinzani wanakosea nini?

Mghwira: Uwezekano wa vyama vya upinzani kushika uongozi wa nchi upo mkubwa. Vyama vinakua na vinaanza kujipanga kushika nafasi mbalimbali za uwakilishi. Watumishi wa umma ni walewale kwa kawaida na ndiyo sababu hawatakiwi kuwa na upande wa wazi wa kisiasa

japokuwa hapa kwetu ni wazi kuwa watumishi wa umma kwa kiwango kikubwa na hasa walioshika nafasi nzito ni makada wa chama. Pengine ipo hivyo hata kwa upinzani ukishika madaraka. Kwa hiyo la msingi ni kulinda utumishi wa kisheria na taratibu bila ubaguzi.

Dosari ya vyama vya upinzani mpaka sasa bado ni vikundi zaidi. CCM ni chama, siyo kundi la kina fulani. CCM ilianza kumomonyoka zaidi baada ya kuunda ‘mtandao’ uliomwingiza Rais wa Awamu ya Nne madarakani.

Huo mtandao ulikuwa hatari kwa uhai wa chama. Uliweka wigo wa sisi na wao, ukawa na viashiria vya ubaguzi dhidi ya yeyote nje ya mtandao. Hii haikuwa nzuri na mpaka sasa ni sehemu ya ufisadi mkubwa unaoendelea kulitafuna Taifa.

Kwa hiyo, ukubwa wa CCM unalingana na upungufu wake. Ni ajabu kwa ukubwa wake na kubebwa na Serikali kwa miaka yote, bado imejijengea ukuta na jamii halisi ya Watanzania kwa kuendekeza rushwa na ufisadi vinavyolitafuna Taifa. Imeacha itikadi yake ya awali bila kutangaza itikadi ya sasa.

Chadema ni chama, kundi kubwa. Hakijinasibu kwa itikadi yake. Siyo watu wengi wanajua kama Chadema ni chama cha mrengo wa kulia, kati ama kushoto. Kinasimamia nini hasa.

Ukisikiliza viongozi ni kama wanaharakati wa mrengo wa kushoto, kati ama kulia kati, lakini hawasemi hivyo kwa hiyo haijulikani. Wawakilishi wake na hasa wabunge, kila mmoja ana msimamo wake. Wengi pia hawana msimamo wa kimaendeleo unaoeleweka.

Migogoro isiyoisha kati ya chama tawala na upinzani unatunyima fursa ya kufanya siasa halisi za ujenzi wa Taifa, za kukosoana kisera na kiitikadi pamoja na kuibua mijadala lukuki ya maana. Hii ni hatari kwa siasa za nchi.

Ni mpaka pale vyama tutakapojinasibu kwa itikadi zetu tutajipa fursa ya kukua zaidi, kujiimarisha na kuusaidia umma kutuelewa na kutupa iliyo haki yetu. Ninaamini changamoto hizi ni kwa vyama vyote na kwa hiyo chama chochote kinaweza kushika uongozi wa nchi wakati wowote. Nafikiri wanachi wanachotaka ni mtu yeyote na chama kinachoweza kuwaletea maendeleo.

Swali: Ukiwatazama wanasiasa wa Tanzania unaona wapo wenye nia ya dhati ya kuiongoza nchi au kutafuta masilahi binafsi?

Mghwira: Nafikiri wapo wote wenye nia na wasio na nia halisi ya kuiokomboa nchi. Ni kiasi cha kuwapima pale wanapopewa nafasi.

Kwa hiyo, waliokwisha kuwapo tunajua kwa kiasi nia yao ya ndani. Siasa ni wakati mwingine sanaa tu ya maneno. Hili wananchi wanatakiwa kulijua na kulipambanua vyema na kutoa haki kwa usawa. Kipimo cha uzalendo wa mtu ni utumishi wake kwa umma.

Swali: Unatamani siku moja chama chako cha ACT- Wazalendo kiungane na vyama vingine nchini ili kuwa na upinzani wenye nguvu zaidi?

Mghwira: Muungano siku zote ni nguvu, lakini usiwe muungano wa kuvunja chawa. Waswahili wanasema vidole viwili huvunja chawa, napenda kuuliza kwa nini uwe na chawa?

Huu siyo wakati wa kuendekeza chawa. Na hatuhitaji vidole kuvunja chawa, tunahitaji vidole kwa kazi za ubunifu, umahiri na umakini. Kwa hiyo, vyama vikijikita katika itikadi zao, vikajenga nguvu yao kiitikadi itakuwa rahisi kuungana kwa sababu za kimantiki na si kama tu mkumbo ama mapambo ya muungano.

Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ungebaki na hoja ya Katiba hata bila itikadi ulikuwa na uwezekano wa kuleta muungano halisi ambao ungeibua mijadala ya kiitikadi na hatimaye kufikia ukamilifu wa kujenga siasa za hoja. Kwa sasa hatuna uzoefu wa muungano halisi uliozaa matunda chanya.

Labda niseme katika kuungana itikadi ni muhimu, lakini vyama viangalie uwezekano wa kupima itikadi zilizopo na kujiunga nazo badala ya kuanzisha kitu kipya.

Hii inawezekana endapo vyama vilivyopo vitaonyesha uwezekano wa kuwavutia wanasiasa wachanga na kuwapa fursa ya kujaribu maarifa yao ya kisiasa. Kwa sasa muungano wa vyama ni lazima usukumwe na hoja za msingi za kuliinua Taifa. Katiba bado ni hoja muhimu, lakini isichukuliwe kwa kupokonya hoja kutoka makundi ya kijamii na kuifanya kuwa ya vyama vya siasa pekee. Ije kama hoja mtambuka inayomgusa kila mtu na yenye masilahi mapana ya nchi.

Swali: Jambo gani linalofanywa na Rais John Magufuli ambalo kama chama chako kingekuwa madarakani kingelifanya pia?

Mghwira: Rais alipopewa cheti cha ushindi, ACT- Wazalendo tulimpa ilani yetu. Lengo lake ilikuwa kumpa majukumu yaliyopo ndani ya ilani yetu kama ishara ya kutaka ushirikiano katika uongozi wake na kujenga umoja wa kitaifa.

Katika hotuba ya kutambua ushindi wake, niliombwa kuzungumza kwa niaba ya wagombea wengine. Kati ya mambo niliyomwambia siku ile ilikuwa pamoja na kurejesha na kuukamilisha mchakato wa Katiba mpya, kurejesha nidhamu katika usimamizi wa shughuli za Serikali na utumishi wa umma na kuinua uchumi kwa kupiga vita rushwa, ufisadi, ubadhirifu na uhujumu wa mali za umma, kati ya mengine.

Mpaka sasa Rais Magufuli ameonyesha dhamira katika suala la rushwa, ingawa anatumia utaratibu tofauti na ule ambao ACT- Wazalendo tuliupendekeza, lakini ameleta hofu ya kuendesha mambo kwa kutumia rushwa, upendeleo na ubaguzi.

Sisi tulitaka suala la rushwa liachiwe watuhumiwa. Mtu akituhumiwa kwa rushwa na akapinga, aachwe athibitishe mwenyewe kwa nini asishutumiwe. Mzigo wa kuthibitisha uwe kwake.

Kwa hiyo, mapambano dhidi ya rushwa ni misimamo inayofanana, lakini utekelezaji wake ni tofauti.

Mapendekezo ya ACT- Wazalendo yalikuwa katika kesi za aina hiyo, watuhumiwa wafunguliwe mashtaka mara moja na huko wathibitishe kuwa hawapaswi kushutumiwa.

Changamoto hapa ni imani na vyombo vya usimamizi wa sheria na kutoa haki. Kama Mahakama na polisi ndiyo washutumiwa wakuu wa rushwa na ufisadi ni vigumu kuamini uamuzi wao katika kesi za aina hii.

Kwa kuwa Rais alitangaza kuunda Mahakama ya Mafisadi ingekuwa rahisi kwake kuwafungulia mashtaka moja kwa moja na kuhakikisha Mahakama hiyo inatenda kazi zake kiufanisi.

Kwa kifupi hili ni moja ya eneo ambalo utekelezaji wa Serikali hii unafanana na mapendekezo yetu ACT – Wazalendo.