Miaka 60 ya mafanikio ya Tanzania kuhifadhi wakimbizi

Je, umewahi kujiuliza inakuwaje mtu akaondoka katika nchi yake alikozaliwa na kukulia akakimbilia nchi nyingine kuomba hifadhi? Hivyo ndivyo inavyokuwa. Ni hali inayoweza kumkuta mtu yoyote duniani.

Tanzania imekua ikipokea wakimbizi kwa kipindi cha miongo sita sasa kutoka nchi za jirani kama vile Rwanda, Burundi, Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Somalia, nchi za Kusini mwa Afrika na mashariki ya mbali.

Katika kipindi chote hatua kadhaa zimechukuliwa ili kuwawezesha wakimbizi kupata hifadhi na pia haki za msingi kama kupata mahitaji muhimu, huduma za afya na elimu katika kipindi chote wanachokua wakipata hifadhi nchini.

Kwa upande mwingine pia Tanzania imetoa wakimbizi waliokimbilia nchi nyingine kuomba hifadhi, wakiwemo waliotoka Kisiwani Pemba na kukimbilia Mombasa nchini Kenya mwaka 2001 baada ya vurugu za kisiasa nchini.

Mpaka mwaka 2019 Tanzania inakuwa imetimiza miaka 60 ya kupokea na kuhifadhi wakimbizi nchini. Katika kipindi chote hicho, kumekuwa na mafanikio na changamoto kadhaa.

Miongoni mwa mafanikio yaliyojitokeza ni hatua ya Serikali kwa kutumia sheria ya “Non-Citizen Employment Regulation Act” inayotoa mwongozo wa ajira kwa watu wasio raia wa Tanzania kutoa ajira kwa baadhi ya wakimbizi. Sheria hiyoinampa nafasi mkimbizi anayekidhi vigezo kuweza kuajiriwa kupewa kibali cha kufanya kazi, kibali hicho hutolewa bure.

Miongoni mwa wakimbizi walionufaika na kibali cha kufanya kazi kinachotolewa kupitia sheria hiyo ni John Ebengo ambaye ni raia wa Jamhuri ya ya kidemokrasia ya Kongo aliyeajiriwa kama ameajiriwa kama mwalimu wa somo la kifaransa. Akieleza jinsi alivyoingia kwenye ukimbizi, Ebengo anasema mwaka1996 nchi yake ilinguia kwenye vita ya vya wenyewe kwa wenyewe, kusababisha yeye na familia yake kukimbilia Tanzania katika Mkoa wa Kigoma na kupokelewa kama wakimbizi.Vita hivyo iliyoanzihwa na makundi ya waasi kwa ajili ya kuung’oa utawala wa aliyekuwa Rais wan chi hiyo, Mobutu Seseseko aliyetawala nchi hiyo kwa miaka 31, ilipewa jina la Africa’s First World War ilianza mwaka 1996 na kusababisha machafuko yaliyosababisha vifo na idadi kubwa ya watu kukimbilia nchi jirani kama Tanzania kutafuta hifadhi.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 5.4 aliuawa katika vita hiyo.

“Nina mke na watoto 14, kitaaluma ni mwalimu na wakati huo wa vita nilikuwa nimeajiriwa na Serikali eneo la Kivu Mashariki. Vita ilianza taratibu mwaka 1996, lakini kuna siku ilichachamaa, na niliporudi nyumbani sikuikuta familia yangu, majirani wakaniambia kuwa familia yangu walikua wameshaanza kukimbilia Tanzania kwa kupitia ziwa Tanganyika. Sikuwa na jinsi ila na mimi kukimbia” anasema Peter. Anaendelea kusimulia kuwa alitumia usafiri wa feri kuingia Tanzania kupitia ziwa Tanganyika.

“Nilipofika Tanzania nilikuta familia yangu imeshapokelewa kwenye kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu mkoani Kigoma. Tumekuwa tukiishi kambini tangu wakati huo (1996) mpaka sasa,” anasema.

Anasema baada ya kuishi katika kambi za wakimbizi mkoani humo kwa miaka kadhaa, Ebengo aliamua kutumia haki yake kuomba ajira kwa kufuata utaratibu wa kuomba kibali kwa mkuu wa kambi. “Nilikwenda kwa mkuu wa kambi na kujaza fomu kisha nikapelekwa kwa mkuu wa idara ya wakimbizi mkoani humo kisha nikaruhusiwa. Lakini kabla ya hapo nilishaanza kutafuta ajira kwenye shule mbalimbali hadi nilipopata kazi,” anasema.

“Mwaka 2012 niliajiriwa shule binafsi iliyopo Mbezi, na baada ya hapo nimekua nikiendelea kufundisha somo la kifaransa kwenye shule mbalimbali hadi mwaka huu ninapomaliza mkataba wangu wa kazi,” anasema.

Tangu wakati huo, Peter anasema amekuwa akirejea kambini kusalimia mke na watoto na kuwapelekea mahitaji mengine. “Mke na watoto hawana ajira yoyote na wamekuwa kusubiri misaada toka kwa mashirika yanayohudumia wakimbizi, na chochote ninachopata niwapelekee,” anasema.

Aidha, anaishukuru Tanzania kwa kutoa hifadhi ya wakimbizi kwa kipindi chote hicho. “Sheria za Tanzania ni nzuri sababu zinalinda, kuthamanisha utu na usalama wa wakimbizi,” anasema

“Licha ya fursa zinazotolewa na mashirika yanayohudumia wakimbizi, bado idadi ya wanaochukuliwa ni ndogo mno,” anasema. Alipoulizwa kama ana mpango wa kurejea Jamuhuri ya Kidemokasia ya Kongo, anasema: “Mpango utakao jitokeza ndiyo huo nitaambatana nao, ila kwa sasa Kongo bado hakuna amani, “anafafanua.


Kuhusu wakimbizi

Kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi ya 1998, mkimbizi ni mtu yoyote aliyekwenda nje ya nchi yake kwa sababu ya hofu ya maisha take kuwa hatarini kutokana na rangi yake, dini, utaifa au kuwa mwanachama wa kikundi cha kijamii au kuwa na maoni ya kisiasa yaliyo tofauti na utawala wa nchi husika. Masuala ya wakimbizi yamekuwa yakiongozwa kisheria duniani ikiwa pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa wakimbizi wa mwaka 1951, Itifaki ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1967, tamko la Cartagena la mwaka 1984, itifaki za Maziwa makuu za mwaka 2009 na mkataba wa Kampala kuhusu wakimbizi wa ndani wa mwaka 2009. Akifafanua zaidi kuhusu dhana ya ukimbizi hivi karibuni katika mkutano wa wadau uliofanyika jijini Dar es Salaam, Profesa wa Sheria Khoti Kamanga anawagawa wakimbizi katika makundi mawili ambayo ni wale waliolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na hali mbaya ya usalama. Kundi la pili anasema ni wanaotafuta hifadhi za kisiasa, wakimbizi, wanaorudi nyumbani na walioyakimbia makazi yao wakiwa ndani ya nchi.Anataja pia makundi ya wapigania uhuru miaka ya 1950 hadi 1970 katika baadhi ya nchi za Afrika Ikiwemo Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe, Namibia na Angola waliopewa hifadhi nchini.


Changamoto

Licha ya historia hiyo ya Tanzania kuhifadhi wakimbizi, Profesa Kamanga anasema anasema bado historia hiyo haijaandikwa kwa ufasaha ili ijulikane ipasavyo.

“Kwa nchi zilizoendelea kama Uingereza, Canada na Ujerumani, wamewekeza rasilimali kubwa kwenye historia. Leo ukitaka kufanya utafiti kuhusu historia ya wakimbizi, utalazimika kuomba taarifa za Tanzania kutoka kwenye nchi zilizoendelea. Sisi tunashindwa kuwa na historia ya kutosha kwa sababu ya uwekezaji mdogo katika utafiti. Utafiti ni gharama kubwa unahitaji uwekezaji wa kutosha,” anasema Profesa Kamanga

Lakini pia kuna changamoto za kisheria, kwa Tanzania, Sheria ya Wakimbizi haijatungiwa kanuni tangu ilipotungwa mwaka 1998.

Akifafanua suala hilo, mkurugenzi wa shirika la Diginity Kwanza, Janemary Ruhundwa anasema kutokuwepo kwa kanuni kunaweka ugumu wa utekelezaji wa masuala ya wakimbizi ikiwa pamoja na kuwapa haki zao.