Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muna Love : Asimulia kuhusu mtoto,kuokoka, maisha na michoro mwilini

Muktasari:

  • Pia, ni mmoja wa watu waliopata umaarufu kupitia tasnia ya filamu na kazi za ujasiriamali ikiwamo kuandaa matamasha ya burudani ya muziki.

Munalove ni jina maarufu nchini hususani katika mitandao ya kijamii na masuala ya burudani.

Pia, ni mmoja wa watu waliopata umaarufu kupitia tasnia ya filamu na kazi za ujasiriamali ikiwamo kuandaa matamasha ya burudani ya muziki.

Hivi karibuni amejikuta akiwa masikioni mwa watu kutokana na kuamua kwake kukata shauri na ‘kuokoka’.

Gazeti hili limefanya mahojiano ya kina na mwigizaji huyo wa zamani kujua mengi kuhusu yeye ikiwamo hilo la kuokoka, kufuta tattoo na kuachana na uigizaji.

Nasra: Tueleze Munalove jina lake halisi ni lipi?

Munalove: Jina halisi la Munalove nililopewa na wazazi wangu ni Rose Alphonce, na jina la Muna nililipata wakati nikiwa katika tasnia ya uigizaji kwenye kundi la Shirikisho Msanii Afrika.

Hata hivyo, Love lilikuja kuongezeka wakati nilipofunguliwa ukurasa wa Instagram na wadogo zangu na kujikuta Munalove ndio limeshika zaidi.

Sababu ya wao kutaka niongeze na kuwa Munalove waliona namna gani nilivyokuwa na upendo na watu bila kujali sura, dini kabila au kipato.

Nashukuru pamoja na maamuzi yao hayo, limenisaidia katika kuniingizia fedha kupitia shughuli mbalimbali ambazo nimekuwa nikizifanya katika kuendesha maisha.

Swali: Umetangaza kuwa umeokoka, ni nini kilichokusukuma kuchukua hatua hiyo?

Jibu: Ni kweli kabisa mimi nimeokoka na nilikata shauri tangu mwaka jana baada ya mtoto wangu wa pekee Patrick kupitia mitihani mikubwa iliyomfanya kunishauri niokoke.

Nakumbuka ilikuwa Julai mwaka juzi mtoto wangu alipoanza kuumwa mguu kama utani na baada ya kwenda hospitali iligundulika kuwa amesagika ‘joint’ ya mguu wake wa kulia.

Katika kuugua huko alianza kwa kutambaa lakini awali sikuamini kama ni kweli kwani huko nyuma alikuwa akinisumbua kumtaka mdogo wake hivyo nikaona kama ananiigizia.

Lakini kwa siku tatu mfululizo mtoto, aliendelea na hali hiyo na nilipojaribu kumfokea alijikaza kutembea lakini kwa kuchechemea na ilifika mahali akashindwa kabisa hata kushuka kitandani.

Hapo ndipo nilipoamua kwenda kumfanyia uchunguzi hospitali na ndipo alipogundulika kuwa na tatizo la joint ambapo niliambiwa mifupa ilikuwa ikisagika na kuhisi kwamba huenda kuna siku alidondoka jambo ambalo sikumbuki kwa kweli na niliwabishia kuwa hajawahi kupatwa na tukio hilo.

Katika matibabu hayo nilihangaika hospitali mbalimbali na mwisho wa siku nikaishia Moi ambako huko alifanyiwa operesheni takribani tano ndani ya miezi tisa na mwisho ilikuwa awekewe madini fulani ya plastiki kwa ajili ya kumsaidia kuweza kutembea.

Madini hayo yaliyokuwa yatoke nchini Marekani nilielezwa kuwa yanauzwa sio chini ya Sh50 milioni, lakini kwa Moi niliambiwa huenda wangenisaidia niipate walau kwa Sh25 milioni.

Hata hivyo, wakati tukiwa tunasubiria hilo, mtoto kila wakati alikuwa ananisisitiza kwa nini nisiokoke kwani kwa kufanya maamuzi hayo ndio ingekuwa pona yake.

Pia alinitaka nimuitie mchungaji kumuombea na kupenda kusikiliza mara kwa mara nyimbo za dini hali ambayo ilikuwa inanifanya nimuone kama kachanganyikiwa kutokana na dawa nyingi alizotumia.

Nakumbuka nyimbo alizokuwa anapenda kuzisikiliza Zaidi ni Sitabaki Kama Nilivyo ya Joel Lwaga, Siteketei ya Angel Bernard na Yahwe ya msanii Jimmy wa Nigeria.

Katika kumpata wa kumuombea nilijikuta navizia wachungaji katika makanisa yaliyopo pale Muhimbili, na kufanikiwa kumpata mmoja ambaye alienda kumuombea na kuanzia hapo hali ya Patrick ilianza kubadilika ambapo alikuwa akisema hasikii maumivu tena.

Hata ilipofika muda tukaruhusiwa kurudi nyumbani na kutakiwa asishushe mguu chini hadi miezi sita ipite, lakini ajabu aliusha na kukanyaga ndani ya mwezi mmoja na wakati wote alipokuwa akitembea alikuwa akitaja jina la Yesu.

Kama haitoshi alikuwa anataka nimpeleke kanisani na hata alipofika huko alikuwa akimuhoji mchungaji maswali ya kiutuzima ya Mungu ambapo niliambiwa nimfutishe kwa kuwa ana kitu kikubwa ndani yake.

Kutokana na mwanangu kupitia mapito hayo hadi kupona kwa kweli sina budi kuendelea kumtumikia Mungu kwa kuwa nimeiona nguvu yake kwenye ugonjwa wa mwanangu ambapo saa yoyote nilikuwa nimeshakubali kupokea taarifa mbaya kutoka kwa madaktari.

Swali:Nini anachojutia cha kidunia

Jibu:Kati ya mambo ambayo najutia ni pamoja na picha zilizoacha sehemu kubwa ya maungo yangu nilizokuwa narushia kwenye mitandao ya kijamii kwani pamoja na kuzifuta bado kuna watu wanazo ambapo baadhi yao nimekuwa nkiwaomba wazifute.

Wakati kwa upandewa tattoo anasema yupo mbioni kuzifuta, na tayari kashaanza mawasiliano na wataalam nchini Thailand kuweza kumsaidia kuzifuta ambapo ya shingoni tu itamgharimu sio chini ya sh1.6 milioni.

Katika kubadilika kwangu huku hata marafiki niliokuwa nao awali najaribu kuwapunguza kwa asilimia 90 ambapo kati yao wapo walionanga kwa kubadilika kwangu lakini hii hanimpi shida kwa kuwa najua kilichomfanya niwe hivyo na nitaendelea kushikilia msimamo wangu.

Swali: Vipi mtoto , utaendelea kumtupia mitandaoni?

Jibu: Ndio mtoto wangu nitaendelea kumrushia mitandaoni kama kawaida na kumvalisha vizuri kwani natafuta kwa ajili yake japo atajitahidi kumlea katika njia inayompendeza Mungu.

Pia wasanii wapunguze kucheza scene za mapenzi na waangalie zaidi maisha magumu wanayopitia watu ili yawe funzo kwa wengine waliokata tamaa kwani kukaa kwangu hospitlai muda mrefu nikumuuguza mtoto wangu nimeayaona mengi kwa watu waliokuwa wanakuja kutibiwa hapo.

Swali:Uliingiaje kwenye filamu na ujasiriamali?

Jibu: Sanaa ya uigizaji niliianza kipindi cha kuchukua picha za kutengenezea video ya sauti ya Manka iliyoimbwa na Crazy GK, ambapo mimi pamoja na wenzangu tulitakiwa kucheza kama video queen.

Baada ya kuonekana hapo, msanii Beka kutoka kundi la Shirikisho Msanii Afrika alikuja kunichukua nijiunge na kundi lao lililokuwa limesheheni wasanii maarufu kama kina Mama Kawele, Masinde, marehemu Kashi na wengineo.

Hata hivyo, baada ya tasnia ya maigizo kugeukia kwenye filamu nako niliweza kuigiza chache ikiwemo Born to Suffer, Siri ya Mapenzi na Hukumu ya Tunu ambapo ilipofika 2007 nikaachana na kazi ya kuigiza na kuingia kwenye biashara.

Katika biashara nilianza kwa kupeleka nguo katika maofisi ya watu, baadaye nikapata wazo la kufungua duka na ilivyonichanganyia nami nikaanza kusafiri kwenda nje ya nchi kuchukua mzigo wangu kwa kushikwa mkono na wanawake wafanyabiashara ambao walianza siku nyingi kazi hiyo.

Biashara pia ndio iliniwezesha kufungua kampuni ya Muna Enterprises ambapo mbali na kuandaa shughuli mbalimbali pia nimekuwa nikishona nguo za wafanyakazi wa makampuni mbalimbali na shule.

Hata hivyo, sasa hivi nataka nibadili biashara na kuhamia kwenye za kukodisha vifaa mbalimbali vya kwenye shughuli za mikutano, semina, makongamano na matamasha mbalimbali.

Pia, katika uandaaji wa matamasha sasa hivi nimehamia kwa wasanii wa injili ambapo malengo yangu ni kuona matamasha ya aina hii yanakuwa makubwa kama yale ya Fiesta.

Kuhusu kufuta tattoo

Amesema mpaka sasa ana michoro mitano kwenye mwili wake huo ambapo wa shingoni pekee ambao ndio Mkubwa kuliko yote ameshaulizia bei yake na kuambiwa atapaswa kutoa sh1.5 milioni.

“Tayari nimeshaulizia kwa wataalam nchini Thailand ambao wanaweza kunifuta hizi tatoo bila kupata madhara yoyote, wameniambia nitapaswa kuwalipa sio chini ya sh1.5 milioni, lakini nimewaambia nataka nizitoe zote kwa pamoja ambazo hizi ndogondogo zitakuwa sio chini ya sh1.2 milioni.

“Hivyo ukiangalia zote hapo sio chini ya sh5 milioni japo bado tupo kwenye mazungumzo ya kuona namna gani wanaweza wakanipungizia bei,’amesema Munalove.