NDANI YA BOKSI: Bado hatujawakaribisha kitaa kisanaa Babu Seya, Papii Kocha

Mitaa ya Sinza ilikuwa shangwe tupu. Machimbo ya Abajalo na maeneo ya jirani. Mitaa ambayo Babu Seya na Papii Kocha kabla ya kwenda jela miaka 16 iliyopita waliishi hapo. Mitaa ya Van Damme na wahuni wengi tu. ‘Of kozi’ na vimwana wa viwango vya kimataifa hawakosekani. Sinza tena utaongea nini? Kwa wajanja.

Ni baada ya taarifa kuzagaa kuwa wameachiwa kutoka ndani ya gereza la Ukonga Daslama mjini. Nani alitegemea? Hakuna! Baada ya miaka mingi ya kuwakosa kitaa na kwenye jukwaa la burudani. Wino wa kalamu iliyoshikwa na Rais John Magufuli unasababisha tabasamu pana kwenye uso wa Babu Seya na mwanaye Papii Kocha wako huru.

Haya sasa hivi tuko nao tena mtaani baada ya kusota jela kwa kosa walilohukumiwa nalo.

Wamekaa muda mrefu sana huko jela na maisha ya jela wanayajua zaidi kuliko hata ya mtaani kwa sasa. Kuna vitu vingi vimekuja na kutoweka wakiwa ndani ya kuta za gereza. Wakati wanatoka miaka mitatu iliyopita walikuta kila kitu kikiwa tofauti.

Hawa watu wameenda jela facebook ikiwa haijazaliwa, Email zilikuwa yahoo na Hotmail, hii ya kuishia na gmail.com haikuwepo, BBM imekuja na kuondoka wakiwa jela. Kifupi BlackBerry hawazijui.

WhatsApp na Instagram, walikuwa wanasikia kwa watu tu walioingia jela na kukutana nao. Hawajui kitu kifupi ni binadamu waliokuwa wajanja na kugeuka washamba.

Kwenye jiji la Dar es Salaam, asilimia 90 ya majengo makubwa na mazuri yamekuja na kusimama wakiwa jela. Mitaa mingi wataishia kuulizia watu tu kuwa hapa ndo wapi?

Kitu pekee ambacho kitawasaidia ni kwamba walirudi mitaani wakiwa wapya. Wapya kwenye mioyo ya mashabiki wao wa kipindi kile. Lakini kizazi hiki cha Bongofelva, hawawajui hawa watu. Ni watu wachache sana wanaotumia Instagram kwa sasa wanaojua ubora wa Papii Kocha Mtoto wa Mfalme. Ukweli ni kwamba wana kazi ya kuwaaminisha watu.

Kwanza wale mashabiki wao wa zamani kuwa bado wako vyema na kuwaaminisha mashabiki wa dunia ya sasa. Kwamba Papii na baba yake walikuwa habari ya mjini kweli kwa ubora wao lakini Papii kama atarudi mtaani na zile swaga za kutegemea pesa za kurusha majina ya Mapedeshee ajue tu kwamba hivi sasa hakuna Pedeshee Ndala wala Papaa Mutu ya watu.

Naamini wameshaondoa lile wenge la kijelajela watulie na wajipange. Wasome mchezo ukoje, ili wajue wanaingia kitaa na muziki wao.

Kuna wazushi kibao watajitokeza na maneno meengi kana kwamba wana mpango wa kuwasaidia. Hao ndiyo watakao au wanaofanya wajute hata kurudi uraiani. Kama mipango itakuwa ya pupa na upoyoyo.

Miaka zaidi ya 10 nje ya ulingo usichukulie poa. Lazima mtulize vichwa msiingie kiboya mkiamini katika akili za wadau wa zama zile za muziki. Hao walishajifia kiakili na kimawazo, hawana lolote. Kuna watu wapya na mashabiki wapya.

Msipokuwa makini mtajikuta mnarudi mtaani na kuishi maisha ya shida kuliko jela mlikokuwepo.

Ni wakati wa kuvuna pesa baada ya kusota jela kwa muda mrefu. Lakini kama mliingia kibwege na wahuni kuwasainisha kijinga mikataba ya hovyo. Amini nakuambieni mtaishia kunufaisha familia za wengine. Kitu kitakachofanya mjutie na kukosa raha ya kuwepo huru mitaani. Na hili naliona, miaka inakatika sisikii siyo tu mipango, hata simulizi za nini kinachofuata. Babu Seya na Papii wana bahati jela wapo watu wasiokuwa na kosa kama lao. Lakini wanasota miaka na miaka wakisubiri hukumu na wengine upelelezi tu.

‘Ene wei’ hakuna jambo gumu kama mtu aliyekuwa kileleni akashuka na kutaka kurudi tena kileleni. Sijui lakini ni ngumu muda ukikuacha hauna urafiki wala huruma na wewe. Angalia ubora wa Papii katika kuchezea koromeo. Tazama ubora wa Babu Seya katika utunzi, uimbaji na upigaji gitaa. Lakini bado wameshindwa kurudi ‘on top’.

Kitu katili zaidi duniani ni muda haujawahi kuwa na huruma na mtu. Babu Seya na Papii hakuna lingine zaidi ya muda kuwaacha. Kama sauti, majina, utunzi na bado wanapumua. Kwa nini huoni balaa lao kama la miaka mingi nyuma enzi zile nyakati zimewalia denge pindi walipokuwa jela na huku nyuma kupoteza kumbukumbu zao zote.

Natamani kumuona Mama na Mwana tunaimba na kucheza. Yule Seya wa viwalo ambaye alifanya Jiji litikisike na runinga zipate moto huku masikio yakishindwa kuchoshwa na mirindo ya sauti zao. Na zaidi pesa za watu zikiteketea kwa viingilio kwenye shoo zao ule muda ambao Papii aliibeba dansi kwenye mabega yake. Kila mtoto mzuri akitaka kuwa jirani yake, dunia imepinduka. Kwa kiwango ambacho siyo tu hajui atoe nyimbo gani, bali haelewi aanzie wapi. Hapa ndipo akili za watu wenye upeo wa burudani zilipohitajika, lakini ardhi nayo ina yake yenyewe. Imeendelea kumeza akili zote zenye akili duniani. Papii Kocha afanye nini msela ametoka jela ila hajatoka kimuziki tena.

Pengine ‘taimingi’ ilikuwa mbovu baada ya kutoka jela. Kwa sasa inabidi itumike akili iliyovuka akili ya kawaida ya binadamu kumrudisha Papii. Anaweza kuwa ana rundo la nyimbo na hazina ya mashairi kichwani lakini tazama wale kaka zake aliowaacha nyuma yake pale Fm Academia wana hali gani? Kama wao waliokuwa uraiani pia wamekata ringi kisanii itakuaje kwa yeye?

Yawezekana muziki wa dansi kwa ujumla wake umeyumba lakini hiyo si sababu kwa kuwa Papii alishaanza ‘Ukristiani Bela’ tayari kabla ya jela. Alikuwa na ‘singo’ zake kibao tu. Alianza kukimbiza kitambo akiwa ‘solo atisti’. Kabla ya kwenda jela alijitegemea bila kutegemea uwepo wa bendi wala kikundi lakini hii leo nyakati hizo zimeshamtupa. Kuna watu wanalazimisha upende kitu bila kulazimishwa ubora na utimamu wa kile wafanyacho ndiyo sumu inayokupindua kutoka katika dunia hii kwenda dunia nyingine. Papii alifanya wale machizi wa Hip Hop wamhusudu katikati ya mizuka ya Bongofleva ile ngumu ngumu. Papii hakuhitaji kufanya uhuni ili apendwe na wahuni. Hakuhitaji apake nywele rangi na kutoboa sikio kama siyo kusuka ili totozi za mjini zimuelewe. Alikuwa yuleyule alivyo na kuendelea kuteka watu kisanaa jela ikamtenga na watu wake. Jela ikatukosesha fujo na kelele zake zilizosikika kila kona, kuanzia mitaani mpaka kwenye vipindi redioni. Uliza watu.

Papii anabaki kuwa mfano wa mtu aliyetendewa ukatili na muda. Tunatenganishwa kinguvu na kipaji cha ajabu kwa sababu ya muda. Alianza kukimbiza akiwa bado kinda sana kwenye bendi ya FM Musica. Jina lake likazidi kupaa kisanaa kadri siku zilivyosonga. Miaka ya 2000 mwanzoni alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa SmoothVibes, chanzo cha THT.

Wacha maisha yaendelee. Lakini muda ni kitu cha msingi sana katika kila jambo. Hakuna binadamu aliyefanikiwa kwenye kila jambo bila kujali muda. Na wengi waliofeli maisha ni wale ambao walijenga uadui na muda. Walioko jela pia kinachowatesa zaidi ni muda kuliko kulala kwa shida wala mbu. Kila jambo ni wakati.

Baba na mwana wametoka jela wapo mtaani toka 2017 lakini bado wamekosa ‘linki’ na mtaa. Tulifurahi walipotoka jela na kuungana nasi lakini wameungana nasi kiupeo tu na kihisia, kisanaa bado wapo jela. Wameshindwa kurudi kwenye kilele chao, tuliwakaribisha kwa shangwe ya kuonana tena. Ila bado tunapaswa tuwakaribishe mtaani kisanaa.