Ndani ya Boksi: Krismasi hii wazee wa kubeti ndio viumbe pekee wenye matumaini

Krismasi kabla haijafanyika imekosa mvuto kwa kiwango cha juu sana. Watu hatuna kitu lakini madukani vitu vimejaa. Kuanzia Kariakoo mpaka Buza kule kwa Mpalange. Tatizo ukame wa faranga. Mifuko imekauka kama Januari imeshafika.

Any way. Krismasi itafanyika hata kama mifuko imekauka kama mabua ya kiangazi. Tuendelee kujipukutisha na kidogo tulichonacho tukisubiri 'stresi' za Njaanuari. Nguvu tunayotumia kustarehe ndani ya sikukuu hizi, ndio chanzo cha kilio cha January. 'Meri Krismasi' bandugu na jamaa.

Kadiri siku zinavyosogea binadamu pekee wenye matumaini nchi hii ni wale maofisa wa kazi za ubashiri (kubeti wazee wa mikeka). Hawa ndio viumbe ambao hufurahia kunapokucha ili aende ofisini akabeti, basi. Kisha aanze kujipa moyo wa kibwege kuwa atakuwa milionea punde.

Kinachotufanya tusukume siku zisonge ni kwa sababu kuna vitu vinatufariji. La sivyo wengi tungekuwa wenyeji wa ahera kwa kujitanguliza au kutangulizwa na msongo wa mawazo. Wenye ajira na wasio nazo wote laini moja, hatuchekani. Kila uingizacho kinaishia kulipa madeni na kuvimbisha tumbo.

Kwa wenyeji wa Dar na miji mingine mikubwa. Kuna vitu vingi vya kuondoa mawazo vichwani mwetu. Hapa Dar moja ya vivutio ni pamoja na upandaji bodaboda kwa kina dada. Unajikuta katikati ya lindi la mawazo mazito ya maisha. Huna hili wala lile. Huoni mbele wala nyuma.

Naongelea sisi wazee wa kuondoka 'homu' bila kitu na kurudi bila kitu lakini uko njwiii. Wale ambao ili ule lazima udamke mapema kwenda mjini bila kujua cha kufanya lakini unaendelea kuvuta kibwegebwege tu hewa ya Mwenyezi Mungu. Wazee wa kutegemea macho zaidi.

Kila unachowaza unajipa jibu kuwa ni vigumu kutekelezeka. Unawaza utakula nini na utafikaje kesho. Unaelekea kukata tamaa kabisa, mara ghafla bodaboda inapita mbele yako ikiwa imebeba 'Pisi Kali'. Mkao wa pisi juu ya boda unageuka kuwa pumbazo na burudisho la nafsi.

Mawazo ya njaa njaa yanakata ghafla. Unakenuakenua meno kama punguani. Unaangalia ufundi wa uumbaji wa Mungu baba Mwenyezi. Kwa viumbe hawa uzao wa Beyonce, Hamisa, Delila, Zalisa, Eva, Nandy kama siyo Irene Uwoya. Pisi huvutia kwenye bodaboda kuliko posho za ubunge.

Ukienda Lusaka au Lilongwe hapo, ukaangalia usafiri wa bodaboda namna unavyotumiwa bila 'mekanizimu' ya kutosha kwa virutubisho vya nafsi. Kina Gigy Money wa huko wakikaa kwa bodaboda, utadhani punda wamebeba mizigo wanapita katikati ya jiji. Hamna kitu.

Hawako 'romantiki' kabisa na usafiri wa bodaboda. Wanapanda kama vile wanaungama dhambi zao za uzinzi pale Kawe. Endapo wao ndio wangekuwa waanzilishi wa usafiri huu, bila shaka ungekosa soko kabisa. Kuna haja ya kuwapelekea semina elekezi ya namna ya kupanda kwa mtindo wa kurutubisha nafsi za wakware mitaani.

Daslama picha za ngono zimepungua mitaani na mitandaoni. Kwa sababu bodaboda zinapunguza mambo mengi. Ukiwaona kwa bodaboda unaweza kudhani wimbo wa Diamond ule wa 'Jeje'. Wanajibinua kama wanaanika mbaazi. Huvutia kuliko ajira ya 'yunisefu'.

Lakini yote kwa yote, mambo ni magumu. Usishangae bingwa mmoja kumiliki pisi nyingi kuliko idadi ya wafanyakazi wake. Kwa sababu masela wengi kitaa tumekata ringi kinoma. Hatuna mawe ya kutosha kiasi cha kumiliki, kutunza na kuzifanyia 'sevisi' kila wiki pisi za mjini.

Matokeo yake pisi nazo zinaenda kujiangusha kwenye 18 za watu walewale wenye nafuu ya kipato. Wengine wenye maisha ya kutegemea mboni za macho na kinywa kujenga undugu na neno bosi, tajiri, kiongozi, mkurugenzi. Tunaishia kuwaita shemeji.

Kama huna mawe mjini hapa kila pisi utaiita shemeji. Pisi hazitaki maneno mengi wala mvuto wa mwili na sauti. Pisi zimegeuka kuwa kama droo za benki, zinawaza kuingiza na kuhifadhi pesa tu kutoka kwa masela sisi, uzao wa Adam au Samson kama siyo Goliath.

Zunguka mjini hivi sasa, nenda mitaani huko. Sura za masela zina ndita nyingi kuliko matairi ya mabasi ya mwendokasi. Kwa sababu ya ukosefu wa uzito mifukoni, na sikukuu kubwa kama hii ya keshokutwa ndio inaleta 'stresi' mkurabita. Kifupi tuna wakati mgumu sana.

Kitambo hicho tuliumizwa sana na nauli za bodaboda ama taksi za mitandaoni. Lakini kwa sasa hivi hata akija kwa daladala maumivu ni yaleyale tu. Ukimuona mtu anatimba mjini kila siku mpe pongezi, maana nauli za daladala na bodaboda kwa sasa hazina tofauti.

Watu wengi wamekata tamaa sana. Wenye matumaini ni wale wazee wa kubeti. Ambao kutandika mikeka ndiyo ajira yao rasmi. Ndio binadamu pekee ambao wanaamini kwamba unaweza kulala hohehahe na kuamka tajiri mkubwa. Wengine wote hatuna hamu.