Nitegemeo la masupastaa kwa kuwaandikia mistari

Muktasari:

  • Mwananchi imepata fursa ya kukutana na msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia Mungu amemjalia kipaji ambacho ni cha hadhi ya juu kuliko watu wanavyofikiria.

Wachache wanalitambua hili kwamba hadi wale wakongwe kuna muda wanapungukiwa busara za kuandika mashairi na hivyo kuomba msaada ili kuendelea kupeta kimuziki. Ndio hivyo basi.

Mwananchi imepata fursa ya kukutana na msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye pia Mungu amemjalia kipaji ambacho ni cha hadhi ya juu kuliko watu wanavyofikiria.

Kwao nyumbani, Temeke, mkoani Dar es Salaam, wazazi wake wanamuita Omary Ally Mwanga. Lakini kutokana na kipaji chake ambacho kwa sasa kinamueka mjini, ameamua kuwa na jina jingine maarufu kama Marioo.

Marioo ndio nani?

Marioo (22) mtoto wa tatu kati ya wanne kwa Mzee Ali, anaeleza kwamba kwao nyumbani, hakuna mtu hata mmoja ambaye anaimba wala kwenye sanaa yeyote ile.

“Sio tu nyumbani bali ukoo mzima, hatuna muigizaji wala muimbaji. Imetokea tu kwamba mimi Mungu kanipa hiki kipaji na ninashukuru,” Marioo.

Ameanza muziki mwaka 2014 akiwa shuleni.

Anasema haikuwa rahisi kuwa jinsi alivyo kwa sasa lakini pia kuna ladha za watu mbalimbali zimechangia kwa hatua fulani.

Anasema studio chini ya prodyuza na meneja wake, Abbah Process huwa anafanya muziki.

“Mara nyingi utanikuta studio tukipiga stori na washikaji zangu, au tunaandaa vitu vikali,” anasema Marioo.

Shukurani zake za dhati ziende kwa mashabiki na wadau wengine ambao waligundua kipaji chake kwenye tasnia ya sanaa na hivyo kumfikisha alipo.

Unaandikia wasanii mashairi?

Marioo, anakubali kwamba yeye mbali na kuwa na uwezo wa kuimba muziki wa kisasa maarufu kama Bongo Flava,amekuwa akitunga mistari na kuwakabidhi wasanii wa hadhi kubwa.

Amemtaja Christian Bella na wimbo wake wa Pambe, Nabembea ya Ditto, Bado ya Mwasiti, Sawa ya Msami, Wasikudanganye ya Nandy ambayo ilimpa umaarufu Marioo na pia muimbaji mwenyewe, Nandy.

“Mimi kuandika mashairi sio kazi ngumu, ilikuja tu kama fursa na mimi nikaitumia ndo maana nimetangulia kusema Mungu ni mkubwa. Napokea simu za watu wengi sana hususan wasanii na mameneja wao kwamba niwaandikie, na mimi naona faraja kwa hilo,” anasema Marioo.Aidha anafafanua kwamba, mwanzoni alianza kuandika bila malipo wala kutarajia kitu chochote ila kadri siku na uhitaji ulivyokuwa mkubwa, ikabidi kuwepo na menejimenti ambayo inamsimamia na hivyo, kwa sasa suala hilo limekuwa ni la kibiashara zaidi.

Anajuaje kwamba haya mashairi ni bora kwa msanii yupi?

Anasema hilo halimsumbui kwa kuwa mara nyingi wakati anaandika, anaendana na beat hivyo inakuwa ni rahisi kutambua kwamba msanii fulani anaimba mtindo huu na yule fulani ni miondoko fulani.

Malipo?

Anafafanua kwamba kwa kila mashairi anayoyaandaa kwa ajili ya msanii, gharama ni Sh1 milioni.

Je, wewe unaimba?

Marioo, anasema anaimba ingawa hakutaka kuanza kuimba kipindi hiki kutokana a malengo au mipango yake binafsi.

Wimbo wake wa kwanza uliotambulika kam Dar Kugumu, ambao aliuachia mapema mwaka huu ulibamba na kupokelewa vizuri kinyume na matarajio yake.

Dar Kugumu, ni wimbo ambao nimeurekodi mwaka 2015, na kuuachia mwaka huu ingawa video yake nimeifanya huuhuu mwaka chini ya muelekezi Adam Juma,” anasema.

Wimbo ambao unaufurahai/chukia?

“Mimi katika mashairi yangu yote ambayo naandika, sitegemei kwamba wimbo ukifanya vizuri au vibaya kuna shida. Muziki siku zote ni njia mbili ipo ya kuhit na ya kutokuhit,” anasema Marioo.

Mfano mzuri ni wimbo wa Giggy Money, Nampa Paa, ambao ulitungwa na Marioo lakini kwa bahati mbaya, Baraza la Sanaa nchini (Basata) liliufungia.

Nini siri yako kwenye gemu?

Marioo anasema siri kubwa katika kuyafikia mafanikio ni bidii sanjari na nidhamu katika kazi.

“Kuwa na nidhamu, daima kuna manufaa yake. Mimi kwa mfano wimbo wangu wa Dar Kugumu, nimefanya video bure bila hata shilingi mia. Adam Juma aliamua tu kunisaidia baada ya kugundua kipaji changu na pia nidhamu kazini,” Marioo.

Wito wako?

Anaahidi mashabiki wake wakae mkao wa kusubiri vitu vya moto ambavyo tayari vimepakuliwa na vingine vipo jikoni vinamaliziwa.

“Kwa vijana wenzangu, msikate tamaa, kama unahisi una kitu ambacho kinaweza kikawa chenye manufaa ya halali, tafuta njia sahihi na naamini utafika mbali. Mifano ipo na sio kitu kigeni,” anahitimisha.