Sababu Bongofleva kuporomoka YouTube

Muktasari:
- Baada ya kuongoza kwa miaka miwili mfululizo kusini mwa Jangwa la Sahara, mwaka 2022 unaoelekea kwisha, muziki wa Bongofleva umeporomoka upande wa kuvutia idadi kubwa ya watazamaji katika mtandao wa YouTube.
Baada ya kuongoza kwa miaka miwili mfululizo kusini mwa Jangwa la Sahara, mwaka 2022 unaoelekea kwisha, muziki wa Bongofleva umeporomoka upande wa kuvutia idadi kubwa ya watazamaji katika mtandao wa YouTube.
Mtandao wa YouTube ulioanzishwa Februari 14, 2005 huko San Mateo, California, Marekani umekuwa maarufu duniani kote kwa kucheza video, huku wazalisha maudhui kama wasanii wakilipwa mamilioni ya fedha.
Kwa mwaka 2020 video ya wimbo wa Diamond Platnumz ‘Jeje’ ndio iliongoza kwa kutazamwa zaidi YouTube, ikimaliza mwaka na watazamaji zaidi ya milioni 40. Msanii wa Nigeria, Simi ndiye alishikilia nafasi ya pili kupitia video ya wimbo wake ‘Duduke’ iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 29.
Mwaka 2021 wimbo wa Zuchu ‘Sukari’ ulipata watazamaji zaidi ya milioni 62, huku akifuatiwa na Wizkid kupitia wimbo wake ‘Essence’ uliopata watazamaji zaidi ya milioni 53.
Hata hivyo, mwaka 2022 upepo umebadilika sana, Bongofleva imeshindwa kuingiza hata video moja katika 10 bora ya zilizotazamwa zaidi YouTube katika ukanda huo.
Video ya ngoma ‘Calm Down’ yenye watazamaji zaidi ya milioni 275 ndiyo imeongoza Afrika, huku remix ya ngoma hiyo ikichukua nafasi ya pili kwa kuangaliwa mara milioni 160.
Watazamaji video za miondoko ya Bongofleva mtandaoni pia wameshuka hapa nchini, kulinganisha data za mwaka 2020 na 2021.
Data za mwaka 2020
1. Jeje - Diamond Platnumz (milioni 40).
2. Gere - Tanasha X Diamond Platnumz (milioni 22).
3. Teamo - Rayvanny ft. Messias Maricoa (milioni 21).
Data za mwaka 2021
1. Sukari - Zuchu (milioni 62).
2. Mbosso - Baikoko ft. Diamond Platnumz (milioni 30).
3. IYO - Diamond Platnumz (milioni 17).
Data za mwaka 2022
1. Mtasubiri - Diamond Platnumz ft. Zuchu (milioni 23).
2. Mi Amor - Marioo X Jovial (milioni 20).
3. Naogopa - Marioo ft. Harmonize (milioni 16).
Mathalani Diamond ambaye ndiye msanii anayeongoza kutazamwa YouTube kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa na watazamaji zaidi ya bilioni 1.9, video alizotoa mwaka huu hazijapata watazamaji wengi ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Katika EP yake, First of All (FOA) yenye nyimbo 10, alitoa video saba, ila ni video mbili tu zilizofikisha walau watazamaji zaidi ya milioni 10 hadi sasa. Vigumu kusikia video ya muziki wa Bongofleva ikipata watazamaji milioni 1 ndani ya saa chache au chini ya saa 24 kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
Video ya wimbo wa Diamond Platnumz ‘Waah!’ iliyotoka Novemba 30, 2020 ndio yenye rekodi ya kuvutia watazamaji wengi YouTube kwa muda fupi, ndani ya saa nane tangu kuachiwa ilipata watazamaji milioni 1.
Ni miaka miwili sasa tangu rekodi hiyo kuwekwa, sio Diamond mwenyewe wala yeyote ndani ya Bongo aliyefanikiwa kuivunja.
Akizungumza na gazeti hili, mtaalamu wa mitandao ya kijamii, MxCarter ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya kusambaza muziki ya Slide Digital, anasema kushuka kwa idadi ya watazamaji kunaweza kuwa bei ya bando.
“Ingawa napata mashaka kuhusu bando, kwani hapa nchini ni nafuu na ndiyo maana muziki wetu ulikuwa unatazamwa sana kuliko nchi nyingine ambazo huduma hiyo ipo juu.
“Pia inaweza kusabishwa na promosheni ambayo msanii aliifanya mwaka jana na mwaka huu ni tofauti,” anasema MxCarter.
Kuhusu madai kuwa wasanii kwa sasa wamewekeza kwenye mauzo ya audio tu kuliko video, MxCarter anasema kwa nchi ambazo muziki wao umepiga hatua, audio ni kitu kikubwa kuliko video.
“Ndio maana kwa wasanii wengi video ni chache lakini albamu ni nyingi, wanawekeza zaidi huko kutokana unawekeza kidogo lakini unapata zaidi, na pengine mtu anafanya video moja au mbili kwa ajili ya kutangaza ile albamu.
“Hiyo inaweza kuwa na ukweli kwamba ‘audio streaming’ inalipa kuliko video kwa sababu unakuta audio moja umelipa bei ya juu kabisa milioni tatu na bei ya kawaida ni milioni moja kurekodi, lakini inaweza kukuingizia zaidi ya hiyo fedha, tofauti na video, unaweza kufanya moja kwa milioni 15 lakini isirudi,” anasema MxCarter.
Kwa upande wake meneja vipaji na mtendaji wa kibiashara katika muziki (Talent Manager and Music Business Executive), Sandra Brown anasema inaweza kuwa ni kweli au sio kweli kulingana na biashara ya msanii ilivyokaa, kuna wasanii wanaonufaika zaidi YouTube kuliko ‘streaming platforms’, na kuna wanaonufaika zaidi na ‘streaming’ kuliko YouTube.
“Japo kibiashara na kidunia katika mitandao tunayoitumia kusikiliza na kupakua muziki ambayo si ya kwetu, ni kwamba ‘streaming’ ina thamani kubwa, ina fedha zaidi kuliko watazamaji wa YouTube,” anasema Sandra ambaye amewahi kuwa Meneja wa Mbosso.
Anasema ni nafuu kutengeneza audio kuliko video, kwa hiyo msanii akipima anaona anawekeza kidogo anapata kingi.
“Kwenye video unawekeza kingi unapata kidogo, hata msanii mwenye mtaji mdogo akiniomba ushauri mimi nitamwambia awekeze kidogo apate kingine, kuliko kujaribu kitu kisichomlipa kulingana na uwekezaji.
“Kama utawekaza milioni 20 kwenye video, jua hiyo ni fedha ambayo inatoka, hairudi, unafanya hivyo ili kuitangaza bidhaa ambayo ni audio, kwa hiyo kwenye muziki video ni kwa ajili ya soko, audio ni bidhaa.”
Anafafanua “Audio ni bidhaa, itakayotengeneza fedha kupitia mirabaha, kampuni za usambazaji, kwa hiyo msanii anakuwa na njia kama tatu au nne za kuingiza fedha kupitia sauti bila picha, ila video utawekeza zaidi, uipeleke kwenye TV uwapoze watu wawili watatu, uje tena mtaani ufanye hivyo kwa kweli ni gharama,” anasema Sandra.
Kuhusu kushuka kwa idadi ya watazamaji katika video za muziki Bongo, Sandra anasema kwake anaona ni tabia za mashabiki kubadilika, utajua wanataka kusikiliza nini bila kuzungumza nao. “Kwa Tanzania kushuka kwa watazamaji mtandaoni pamoja na mambo mengine, pengine kazi tunazotoa mashabiki wanaanza kutovutiwa nazo, pili inawezekana video tunazotoa hazitafsiri mvuto ambao shabiki anataka kuuona, tatu pengine watu wanataka kuona kitu tofauti.
“Msanii kama unategemea watazamaji mtandaoni utakuwa kwenye wakati mgumu zaidi, kwa sababu watu wapo kwenye mitandao ya kijamii kuliko kuangalia video. Mtu ataangalia video YouTube pale tu wimbo utakapokuwa mkubwa sana, kama ni hizi nyimbo ambazo kila mtu anafanya inakuwa ngumu sana kumshawishi,” anasema Sandra Brown.
Staa wa Kings Music, Alikiba katika Podcast ya Swahili Radio, alikaririwa akisema mashabiki wasishangae kuona wasanii wanauza tu muziki (audio), maana ndipo wanaingiza fedha.
Alisisitiza bajeti ya video ni kubwa na faida inachelewa, Kiba alisema video moja inaweza kugharimu Dola35,000, wastani wa Sh55.2 milioni, huku video ya chini ikiwa ni Dola20,000, wastani wa Sh31.6 milioni, hivyo watu wanatakiwa kuelewa kuwa muziki unaelekea kuhamia kwenye audio kimauzo kutoka mauzo ya video YouTube.